Jumanne Januari 23, 2007 mwanasiasa mkongwe Mzee Rashid Mfaume Kawawa, alitunukiwa tuzo ya kumuenzi Dk. Martin Luther King inayojulikana kama Martin Luther King Jr. Drum Major for Justice Award, kwa mchango wake mkubwa kwa taifa la Tanzania, kabla na baada ya uhuru wa nchi hii. Mzee Kawawa alitunukiwa tuzo hiyo na Balozi wa Marekani nchini Michael L. Retzer. Tuzo ya Drum Major for Justice Award ilianzishwa ili kumuenzi Dk. Martin Luther King, Jr. Dk. King alikuwa mtu mashuhuri katika nyakati za historia ya hivi karibuni. Hotuba na mihadhara yake ilichochea dhamira ya kizazi kizima. Harakati na maandamano aliyoyaongoza yalileta mabadiliko muhimu katika mfumo wa maisha nchini Marekani, kupitia ujasiri na msimamo wake thabiti wa kujitoa. Msimamo huu ndio uliongoza harakati za kupigania haki za raia kwa miaka kumi na mitatu. Uongozi wake wenye haiba ya kuvutia uliwatia moyo wanaume na wanawake, vijana na wazee, nchini Marekani na ulimwenguni kote.
|