Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Kiswahili Editorial

Gates in Pakistan

February 20, 2007

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates alikutana na Rais wa Pakistan Pervez Musharraf kujadili ushirikiano dhidi ya magaidi wa al-Qaida na waasi wa Taleban wanaofanya shughuli zao katika eneo la mpaka wa Pakistan na Afghanistan. Bw Gates alisema Pakistan ni mshirika mkubwa wa vita dhidi ya ugaidi.

“Nadhani kuwa Pakistan ina umuhimu mkubwa. Inapata hasara kubwa kwa wananchi wake wanaofariki, na kifedha pia katika kupigana katika mipaka. Siku zote kuna namna ambavyo wote tunaweza kuboresha hali, ikiwa ni pamoja na NATO na Marekani, na Afghanistan.”

Waziri Gates alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la mashambulizi katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan, hasa kutokea majimbo ya Pakistan ya Waziristan ya Kaskazini na Kusini. Alimshukuru Rais Musharraf kwa juhudi zinazoonyeshwa na Pakistan katika kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa kikabila wa Waziristan kuzuia mashambulizi ya kuvuka mpaka ya magaidi wa Taleban na al-Qaida.

Serikali za Afghanistan na Pakistan, pamoja na NATO na jumuiya ya kimataifa zinashirikiana kuratibu mkakati mzuri zaidi katika maeneo ya mpakani. Mkakati huo utatilia maanani upungufu wa vikosi vya usalama, umasikini, kukosekana na fursa za elimu kwa watoto na fursa za ajira kwa watu wa eneo hilo. Marekani hivi karibuni imeomba zaidi ya dolla billioni kumi na pointi sita kutoka bunge la Marekani kushughulikia maswala hayo. Serikali za Afghanistan na Pakistan, pamoja na jumuiya ya kimataifa, zina nia ya dhati ya kuboresha maisha ya watu wa Afghanistan na Pakistan wanaoishi katika maeneo ya mpakani.

Waziri Gates anasema yeye na Rais Musharraf walijadiliana kuhusu tishio la ufukura katika maeneo hayo, na kwamba wameona kuna nia kutoka pande zote ya kuboresha hali ya utekelezaji wa sera na kuelewa kuwa kuna fursa nzuri ya kugeuza mambo katika eneo hilo.

Waziri Gates alisema Marekani ilifanya makosa baada ya Soviet Union kuondoka Afghanistan. Tuliitelekeza Afghanistan, alisema, na hivyo kutoa nafasi kwa wenye sera kali kuchukua udhibiti wa nchi hiyo. Marekani, alisema, haitafanya kosa hilo tena, na kwamba ipo Afghanistan kwa muda mrefu.