Kiswahili Editorial
Chinese Activist Arrested
February 20, 2007
Serikali ya China imemzuia mtetezi wa harakati za kupambana na ukimwi Gao Yaojie kusafiri kuja Marekani kupokea zawadi. Dr. Gao, ambaye ana umri wa miaka 80, amezuiliwa nyumbani kwake katika mji wa kati ya China, Zhengzhou tangu Februari mosi. Dr. Gao alifahamishwa mwezi Oktoba kuwa atapewa tuzo na kundi la Vital Voices Global Partnership, kundi la wanawake lisilo la kifaida. Alikuwa amepanga kuhudhuria sherehe hizo pamoja na wanawake wengine watatu wa China ambao pia wanapewa zawadi katika shereza za March 14 katika kituo cha Kennedy hapa Washington.
Dr. Gao alianza kupata umaarufu baada ya kusaidia kutoa siri za mpango wa kuuza damu katika eneo la China ya kati katika miaka ya 1990. Katika mpango huo, maelfu ya wakulima waliambukizwa virusi vya H-I-V vinavyosababisha ukimwi. Waendesha mpango huo mara nyingi walikuwa wakitumia sindano chafu. Dr. Gao alitumia miaka kadha kusafiri katika vijiji kwenye jimbo la Henan, akitoa maelezo kuhusu ukimwi, akisaidia yatima na kutoa madawa. Anasifiwa kwa kusaidia kuilazimisha serikali ya China kupambana na kuenea kwa H-I-V.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imekabiliana na kuenea kwa ukimwi waziwazi. Serikali imepiga marufuku uuzaji wa damu na ubaguzi dhidi ya watu wenye virusi hivyo. Hata hivyo, wafanyakazi wa maswala ya ukimwi wanakabiliwa na usumbufu na maafisa wa serikali za mitaa ambao hawataki kupata sifa mbaya.
Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa China kumzuia Dr. Gao kusafiri kwenda kupokea tuzo. Mwaka 2001 alizuiliwa kuja Washington kupokea tuzo la kimataifa la ukimwi. Na mwaka 2003, Dr. Gao hakuruhusiwa kupokea zawadi ya huduma ya umma huko Phillipines.
Inasikitisha kwamba licha ya kuenea kwa HIV-ukimwi China, maafisa wangali wanajaribu kumzuia Dr. Gao asisafiri. Uhusu wa kusafiri na kuzungumza ni haki ya msingi. “Hakuna yeyote,” anasema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Tom Casey “anayestahili kuadhibiwa kwa sababu tu ya kueeleza maoni yake, kueleza wasiwasi wake kuhusu sera za serikali, na kupigania haki palipofanyika makosa.”




