Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Kiswahili Editorial

Afghanistan Economic Development

March 5, 2007

Rais George W. Bush anasema Afghanistan imefanya maendeleo makubwa tangu kuangushwa kwa utawala wa Taleban mwaka 2001.

“Chini ya utawala wa Taleban, wanawake walizuiliwa kufanya kazi katika ofisi za serikali. Hivi leo, bunge la Afghanistan linajumuisha wanawake 91 na Rais Hamid Karzai amemteua mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Gavana wa Jimbo. Chini ya Taleban, biashara huru ilikandamizwa. Hivi leo, uchumi wa Afghanistan umeongezeka mara mbili tangu ukombozi. Afghanistan imevutia uwekezaji wa kigeni wa karibu dola milioni 800 toke wakati huo. Chini ya Taleban, kulikuwa na watoto laki tisa waliokuwa wanaokwenda shule. Lakini hivi leo, kuna zaidi ya watoto milioni tisa ambao wako shule, watoto milioni moja na nukta nane kati ya hao ni wasichana.”

Habiba Sarabi ni mwanamke wa kwanza Gavana wa jimbo la Bamyan, anasema wanawake wana jukumu kubwa katika uchumi wa Afghanistan. Katika jimbo letu anasema wanawake wana biashara ndogo ndogo za kuwapatia kipato na waendesha biashara zao katika maduka kwenye masoko ya umma pamoja na wanaume.

Huku wanawake wakibadili tamaduni zao na kuvunja miiko ya zamani, anasema Shukria Barakzai, mbunge katika bunge la Afghanistan. Anasema maendeleo ya uchumi ni changamoto kubwa kwa Afghanistan, ambako asilimia 60 ya watu wanaishi chini ya kiwango cha umaskini, na hawana ajira na wanalipwa ujira mdogo mno.

Rais Bush anasema Marekani na washirika wa NATO wanashirikiana na serikali ya Afghanistan kusaidia uchumi wa Afghanistan.

“NATO inasimamia timu 25 za ujenzi kote nchini humo. Timu hizi zitasaidia kujenga mabomba kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, kuboresha uzalishaji umeme, kutoa fursa ya mikopo midogo midogo. Wazo ni kuhamasisha biashara, na kufungua milango ya ajira.”

Marekani na mataifa mengine yamejenga zaidi ya kilometa 6,430 za barabara nchini Afghanistan tangu mwaka 2001. Na tutajenga kilometa nyingine 1,609 za barabara mwaka huu wa 2007, anasema Bwana Bush. Marekani ina nia ya dhati huko Afghanistan, anasema.

“Naliomba bunge kuidhinisha dola bilioni 11 nukta nane katika kipindi cha miaka miwili ijayo kusaidia demokrasia changa kukua. Nimeamuru ongezeko la majeshi ya Marekani nchini Afghanistan. Tumeongeza muda wa kuwabakisha wanajeshi wetu 3,200 nchini humo hivi sasa kwa miezi minne zaidi, na tutapeleka kikosi cha kuchukua nafasi yao ili kuhimili shughuli hapo baadaye,” anasema Bwana Bush.

Mafanikio nchini Afghanistan, anasema Rais Bush ni “muhimu sana kwa usalama wetu.”