Kiswahili Editorial
Missile Defense In Eastern Europe
March 5, 2007
Marekani imekuwa ikichukua hatua za kusaidia washirika wake wa Ulaya Mashariki kujikinga dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya masafa marefu kutoka Iran. Katika mashauriano na washirika wa NATO na Russia, Marekani imependekeza kusambaza kinga za mizinga Ulaya Mashariki. “Nadhani kila mtu anaelewa,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleezza Rice, “ukitilia maanani ongezeko la kitisho cha Iran kwamba kuna haja ya kuwa njia za kupambana na tatizo hilo, na kwamba tunazungumzia kitu cha muda mrefu ili kuweza kuwa na mfumo wa ulinzi dhidi ya mizinga ya mashambulizi.”
Mshauri wa Usalama wa Taifa, Stephen Hadley, alisema kama Iran inaendelea kutengeneza mizinga ya masafa marefu na inafanikiwa katika kutengeneza silaha za nuklia, Ulaya itahitaji namna fulani ya ulinzi. “Hili ni jambo la busara kufanya,” alisema, ni jambo ambalo Ulaya haina budi kulifuatilia, jambo ambalo Russia haina budi kulifuatilia pia.”
Pendekezo la mfumo wa ulinzi dhidi ya mizinga linataka kusambazwa kwa mashine kumi za kinga katika nchi ya Poland na rada katika Jamhuri ya Czech. Serikali ya Russia imeeleza wasiwasi kuhusu kuweka vifaa hivyo Ulaya Mashariki. Lakini Waziri Rice amesema, “haiwezekani” kuwa mashine hizo “ni tishio kwa Russia au zitadhalilisha uwezo wa Russia katika kujikinga.”
Katika matamshi ya hivi karibuni, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Sean McComack alisema pendekezo la mpango huo halisababishi kitisho chochote kwa Russia.
”Mpango wa kinga ya mizinga na kuenezwa kwake hakuilengi Russia kwa namna yoyote ile. Badala yake zinalenga kulinda Marekani na washirika wake dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya mizinga kutoka mataifa ya kihuni kama vile Iran.”
Marekani inaendelea kuwa tayari kushirikiana na Russia katika maswala ya kinga za mizinga. Wakati huo huo, inabaki kuwa katika maslahi ya Marekani, Russia, na Ulaya kushirikiana katika maswala kama kupambana na ugaidi, uenezaji wa silaha za nuklia, na hatari inayosababishwa na mataifa ya kihuni kama Iran.




