Kiswahili By-Liner
Tamko La Waziri Wa Mambo Ya Nje Hillary Clinton Kuhusu Maadhimisho Ya Siku Ya Wanawake Duniani
Machi 8, 2009
Katika ziara yangu huko China miaka kumi na moja iliyopita, nilikutana na wanaharakati wanawake walionieleza kuhusu jitihada zao za kuinua hali za wanawake katika nchi zao. Walieleza bayana kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake, zikiwemo ubaguzi katika ajira, huduma duni za afya, ukatili wa majumbani na sheria zilizopitwa na wakati zinazokwamisha maendeleo ya wanawake.
Wiki chache zilizopita, nilikutana tena na baadhi ya wanawake hao wakati wa ziara yangu ya kwanza barani Asia kama Waziri wa Mambo ya Nje. Wakati huu, nilisikia maendeleo yaliyofikiwa katika muongo uliopita. Hata hivyo, pamoja na hatua muhimu iliyopigwa, wanawake hao wa Kichina walieleza kuwa bado kuna vikwazo vingi na hali ya kutokuwepo usawa inayowakabili, kama ambavyo inavyowakabili wanawake wengi sehemu mbalimbali duniani.
Nimesikia taarifa kama hizo katika kila bara, ambapo wanawake wanajitahidi kutafuta fursa za kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi zao. Wakati tukiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, tarehe 8 Machi, tunapata fursa ya kutathmini maendeleo tuliyoyafikia na changamoto zilizo mbele yetu. Pia tunapata fursa ya kutafakari nafasi na wajibu muhimu wa wanawake katika kusaidia kutatua changamoto nyingi na ngumu zinazoikabili dunia yetu katika karne ya 21.
Changamoto zinazoikabili dunia yetu hivi leo ni kubwa na ngumu sana kuweza kutatuliwa bila ushiriki kamilifu wa wanawake. Kuimarisha haki za wanawake sio tu ni wajibu wetu wa kudumu, bali pia ni muhimu katika kutuwezesha kukabiliana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaoikabili dunia kwa sasa, kuongezeka kwa ugaidi na silaha za kinyuklia, migogoro katika maeneo mbalimbali duniani inayotishia maisha ya familia na jamii pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake kwa afya na usalama wa dunia.
Utatuzi wa changamoto zote hizi unatutaka tutumie jitihada na rasilimali zote tulizonazo. Hatuwezi kuzitatua kwa kuchukua hatua nusu nusu. Lakini kwa bahati mbaya sana, mara nyingi nusu ya dunia inawekwa kando katika utatuzi wa changamoto hizo.
Leo hii, wanawake wengi zaidi wanaoongoza serikali, biashara na mashirika yasiyo ya kiserikali kuliko ilivyokuwa katika vizazi vilivyopita. Lakini, taarifa hizi nzuri bado zina upande mwingine usio mzuri. Bado wanawake ndio wanaochukua sehemu kubwa zaidi ya watu duniani walio masikini, wenye njaa na wasio na elimu. Bado wanawake wanakabiliwa na ubakaji kama sehemu ya mbinu za kivita na wananyonywa vibaya na watu wanaofanya biashara haramu ya usafirishaji watu, biashara inayohusisha mabilioni ya dola.
Mauaji ya wanawake yanayofanywa na jamaa zao, eti kwa minajili ya kulinda heshima ya familia hizo (Honor killings), ukatwaji wa viungo vya mwili, ukeketaji na vitendo vingine vingi vya ukatili dhidi ya wanawake bado vinavumiliwa katika maeneo mengi duniani. Miezi michache iliyopita, msichana mmoja huko Afghanistan, wakati akienda shuleni, alivamiwa na kundi la wanaume waliommwagia tindikali usoni na kumpofua kabisa macho yake, kwa sababu tu ya kupinga msichana huyo asipatiwe elimu. Hata hivyo jitihada za vitisho dhidi ya msichana huyo na familia yake zimegonga mwamba. Binti huyo alisema, “Wazazi wangu wameniambia kuwa niendelee tu kuja shuleni hata kama wakiniua.”
Ujasiri wa binti huyo na dhamira yake thabiti ya kuendelea kupata elimu ututie nguvu na kutuhamasisha sisi sote – wake kwa waume – kuendelea kujitahidi kwa kadri tuwezavyo kuhakikisha kuwa wasichana na wanawake wanapata haki na fursa wanazostahili.
Hivi sasa tukiwa katika mgogoro wa kifedha wa kimataifa, ni lazima tukumbuke na tuzingatie matokeo ya tafiti nyingi yanayotueleza kuwa: Kuwasaidia wanawake katika miradi ya uwekezaji yenye tija kubwa huwezesha kujengwa kwa uchumi imara, jumuiya imara ya kiraia, jamii yenye afya njema na amani na utulivu zaidi. Hali kadhalika, kuwekeza kwa wanawake ni njia ya kusaidia vizazi vijavyo kwani wanawake hutumia sehemu kubwa ya mapato yao kwa chakula, matibabu na elimu ya watoto wao.
Hata katika nchi zilizoendelea, bado wanawake hawajaweza kupata fursa na nguvu sawa za kiuchumi. Wanawake katika nchi nyingi bado wanaendelea kupata ujira mdogo zaidi kuliko wanaume wanaofanya kazi zinazofanana – tatizo ambalo Rais Obama ameanza kuchukua hatua za kulipunguza kwa kusaini Sheria ya Malipo ya Haki iitwayo “Lilly Ledbetter Fair Pay Act”, sheria itakayoimarisha uwezo wa wanawake kupinga malipo yasiyo ya haki.
Ni lazima wanawake wapate fursa ya kufanya kazi na kupata ujira wa haki, wapate fursa ya mikopo na kuanzisha biashara. Wanawake wanastahili usawa katika Nyanja za siasa, wakiwa na haki sawa na uhuru katika upigaji kura, kuiwajibisha serikali yao na hata kugombea nyadhifa mbalimbali. Aidha, wanawake wana haki ya kupata huduma bora za afya, wao na familia zao, wana haki ya kupeleka watoto wao, wa kike na wa kiume shuleni. Hali kadhalika, wana wajibu wa nafasi muhimu katika kuimarisha amani na utulivu duniani. Katika maeneo yaliyoathiriwa na vita, ni wanawake ndio mara nyingi hupata njia za kuweza kutatua tofauti zilizopo baina ya makundi yanayogombana na hatimaye kufikia mwafaka.
Ninaposafiri duniani kote katika wadhifa wangu mpya, nitazingatia kukutana tena na wanawake niliokutana nao hapo awali katika kila bara – wanawake ambao wamefanya jitihada kubwa bila kujali vikwazo wanavyokabiliana navyo, katika kubadilisha sheria ili waweze kumiliki mali, kuwa na haki katika ndoa, kwenda shuleni, kuhudumia familia zao na hata kuhudumu katika majeshi ya kulinda amani.
Aidha, nikishirikiana na viongozi wenzangu katika mataifa mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni ya kibiashara na hata watu binafsi, nitakuwa mitetezi mkubwa katika kuwekea msukumo mambo haya. Kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wanapata fursa sawa ya kujiendeleza kwa kadri ya uwezo wao, sio tu ni suala la utoaji haki, bali pia ni suala la kuimarisha amani ya dunia, maendeleo na ustawi wa vizazi vijavyo.




