Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili By-Liner > Marekani Kuendeleza Jitihada za Kutokomeza Kifua Kikuu
Skip Left Section Navigation

Kiswahili By-Liner

Close Window Larry André ni Naibu Balozi wa Marekani nchini Tanzania
Larry André ni Naibu Balozi wa Marekani nchini Tanzania

Marekani Kuendeleza Jitihada za Kutokomeza Kifua Kikuu

Machi 24, 2009

Na: Larry André

Pamoja na maendeleo yaliyofikiwa hivi karibuni, bado ugonjwa wa Kifua Kikuu umeendelea kuwa tatizo kubwa la kiafya duniani, ambapo watu milioni 9 huambukizwa na zaidi ya watu milioni 1.6 hupoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huu kila mwaka. Pamoja na VVU/UKIMWI na Malaria, Kifua Kikuu ni mojawapo kati ya magonjwa matatu makuu ya maambukizi yanayoongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani. Aidha, takriban asilimia kumi ya wagonjwa wote wa Kifua Kikuu wameambukizwa pia VVU na kwamba Kifua Kikuu ni chanzo kikuu cha vifo vya wagonjwa wa UKIMWI. Ndiyo maana Shirika la Afya Duniani (WHO) limetenga tarehe 24 Machi kuwa siku ya kimataifa ya Kifua Kikuu. Lengo la siku hii ni kuelimisha na kuuhamasisha umma kuchukua hatua za kukabiliana na Kifua Kikuu. Watu wa Marekani wamedhamiria kwa dhati kabisa kushirikiana kikamilifu na watu wa Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa huu mbaya.

Mbali na Kifua Kikuu kuwa tatizo la afya ya jamii, ugonjwa huu ni changamoto kubwa ya kimaendeleo kwani huwaathiri watu wengi walio katika umri wa kufanya kazi. Kifua Kikuu husababisha sio tu vifo vingi, bali pia husababisha mzigo mkubwa wa kiuchumi kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla. Wakati ambapo kwa kawaida matibabu ya Kifua Kikuu hutolewa bure, matokeo ya utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia hivi karibuni, yanaonyesha kuwa gharama za vipimo, maabara, usafiri, chakula na gharama nyingine za kumtunza mgonjwa huchukua kati ya asilimia 8 mpaka 20 ya kipato chote cha kaya kwa mwaka.

Japokuwa tiba ya Kifua Kikuu imekuwepo kwa karibu miaka hamsini sasa, mara nyingi ugonjwa huu huenea kwa kasi na kusababisha vifo katika jamii kutokana na kutokubainika kwake mapema, matibabu yasiyo sahihi na hata wagonjwa kukosa matibabu kabisa. Kwa bahati mbaya, watu masikini ndiyo hukabiliwa zaidi na tatizo la ukosefu wa huduma bora za matibabu. Kifua Kikuu ni ugonjwa utokanao na umasikini. Aidha, ugonjwa huu huchangia pia kuongeza umasikini. Kwa hali hiyo Kifua Kikuu huziathiri familia nyingi masikini katika nchi zinazoendelea.

Marekani imekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya Kifua Kikuu, ambapo watu wa Marekani wamesaidia mipango ya kudhibiti Kifua Kikuu katika zaidi ya nchi 40 ikiwemo Tanzania. Kwa kushirikiana na mipango ya kitaifa ya kudhibiti Kifua Kikuu, Serikali ya Marekani imekuwa ikisaidia katika kuinua ubora wa huduma ya matibabu kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu chini ya usimamizi maalumu (Huduma ya DOTS), kuboresha maabara; kutambulisha teknolojia mpya ya uchunguzi wa ugonjwa huu pamoja na kushirikiana na WHO na wabia wengine katika kufanya utafiti na ufuatiliaji kuhusu vimelea sugu vya Kifua Kikuu.

Tanzania ni nchi ya 14 katika orodha ya nchi 22 zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa Kifua Kikuu duniani, ikikadiriwa kuwa na wastani wa wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu 120,000 kila mwaka toka mwaka 2004. Hata hivyo kutokana na kuimarika kwa ubora wa huduma zitolewazo na ufuatiliaji wake, kiwango cha kufanikiwa kwa matibabu kimeongezeka taratibu kuelekea kiwango cha kimataifa kilichowekwa na WHO cha asilimia 85. Japokuwa kiwango cha kubaini maambukizi mapya ya Kifua Kikuu kimeongezeka nchini Tanzania, bado kiwango hicho kipo chini, kikiwa ni asilimia 46 tu ikilingwanishwa na lengo la kimataifa la asilimia 70.

Janga la VVU/UKIMWI limechangia kuongezeka kwa Kifua Kikuu nchini Tanzania kwa asilimia 60 na kwamba nusu ya wagonjwa wapya, watu wazima wanaougua Kifua Kikuu wanaishi na VVU. Inatarajiwa kuwa mipango ya kupanua huduma za matibabu kwa Watu wanaoishi na VVU ambao pia wana Kifua Kikuu utasaidia sana kupunguza vifo na kuboresha mfumo wa utoaji taarifa, kuhakikisha ufuatiliaji mzuri wa matibabu na hatimaye kupunguza kiwango cha wagonjwa kukatisha matibabu.

Mwaka 2005, watu wa Marekani walianza shughuli ya kusaidia udhibiti wa Kifua Kikuu kama sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuboresha afya ya jamii nchini Tanzania. Msaada huu unalenga kuimarisha uwezo wa watendaji, kuanzisha na kuimarisha huduma za matibabu ya pamoja ya Kifua Kikuu na VVU/UKIMWI (TB-HIV/AIDS integrated activities), kuinua ufahamu wa jamii kuhusu Kifua Kikuu na uhusiano wa Kifua Kikuu na VVU na kuihamashisha jamii ili kupunguza unyanyapaa. Katika mwaka uliopita pekee, jumla ya vituo 570 vinavyotoa huduma za udhibiti wa Kifua Kikuu na VVU/UKIMWI, katika mikoa 14 ya Tanzania vilipatiwa misaada kutoka kwa Watu wa Marekani.

Ili kutimiza malengo hayo, tunaelekeza jitihada zetu katika shughuli zifuatazo:

  • Kusaidia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma ili kuratibu na kuboresha shughuli za pamoja za kudhibiti Kikua Kikuu na UKIMWI

  •  

  • Kutambulisha teknolojia mpya na mfumo wa utunzaji na usimamizi wa takwimu katika maabara ili kuboresha uwezo wa kubaini maambukizo ya Kifua Kikuu na Kifua Kikuu Sugu (Multi-drug resistant TB) hususan katika Maabara Kuu za Kifua Kikuu.

  •  

  • Kutayarisha vifaa na zana mbalimbali za kutolea elimu na taarifa ili kuinua ufahamu wa jamii na mabadiliko ya kijamii kuhusu Kifua Kikuu.

  •  

  • Kupunguza unyanyapaa na kusambaza vifaa na zana za ushauri nasaha kuhusu Kifua Kikuu

  •  

  • Kuihusisha jamii katika jitihada za udhibiti wa Kifua Kikuu kwa kutoa mafunzo kwa wafamasia binafsi, waganga wa jadi na wahudumu wa afya wa vijiji ili kuweza kubaini dalili za Kifua Kikuu na kusaidia kujenga uweza wa jamii kubaini dalili hizo.

  •  

  • Kuimarisha mfumo wa rufaa katika mipango iliyopo ya matibabu ya Kifua Kikuu na UKIMWI na kuongeza idadi ya wagonjwa wa Kifua Kikuu wanaopima VVU.

  •  

  • Kuimarisha utaalamu wa kuendesha na kusimamia mfumo wa utoaji matibabu kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu chini ya usimamizi maalumu ( DOTS) na kukuza ushirikiano wa watoa huduma katika sekta binafsi na sekta ya umma

  •  

  • Kuongeza uwezo wa taifa wa kukabiliana na Kifua Kikuu Sugu ( MDR-TB)



  • Katika mwaka huu wa fedha, watu wa Marekani, kupitia Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID), Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) na Global Fund, wametoa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 10 kwa ajili ya kusaidia jitihada za kudhibiti Kifua Kikuu nchini Tanzania.

    Kutokana na jitihada hizo mafanikio kadhaa yamepatikana. Mafanikio hayo ni pamoja na:

  • Kuanzishwa kwa Kamati ya Taifa ya Mpango wa Pamoja wa Kudhibiti Kifua Kikuu na VVU/UKIMWI na kuandaa rasimu ya sera ya taifa ya kusimamia shughuli za pamoja za udhibiti wa Kifua Kikuu na VVU/UKIMWI

  •  

  • Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, zaidi ya watu 30,000 walipewa ushauri nasaha, kupimwa kama wana vimelea vya Kifua Kikuu na kupatiwa majibu yao. Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya wagonjwa 15,400 wa Kifua Kikuu walipatiwa matibabu.

  •  

  • Kupanua shughuli za Mpango wa Pamoja wa Kudhibiti Kifua Kikuu na VVU/UKIMWI na kuajiri Waratibu wa Shughuli za Pamoja za Kudhibiti Kifua Kikuu na VVU/UKIMWI

  •  

  • Kupitia mitaala ya vyuo na taasisi za umma na binafsi zinazotoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ili kujumuisha vipengele kuhusu Kifua Kikuu

  •  

  • Kuendesha shughuli za kuhamasisha umma kwa kupitia vyombo vya habari na wawezeshaji kutoka katika jamii zenyewe

  •  

  • Kuhusisha Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (APHFTA) na kusaidia uratibu wa shughuli za kudhibiti Kifua Kikuu na UKIMWI za sekta binafsi na sekta ya umma ili kuhakikisha kuwa kuna matumizi mazuri na yenye ufanisi ya rasilimali zilizopo, ikiwemo fedha.



  • Haya ni mafanikio makubwa, lakini changamoto bado ipo. Na tunajua nini kinachotakiwa kufanyika. Mpango wa Kimataifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu wa 2006 hadi 2015(The Global Plan to STOP TB 2006 – 2015), unatupatia mwongozo muhimu kuhusu yale tunayotakiwa kuyashughulikia. Watu wa Marekani tumedhamiria kwa dhati kufanya kazi na wabia wetu, pote nchini Tanzania na dunia nzima, katika kuongeza jitihada za kukabiliana na Kifua Kikuu.

     


    Larry André ni Naibu Balozi wa Marekani nchini Tanzania