Kiswahili By-Liner
Ni Muda wa Dunia Kuchukua Hatua
March 25, 2009
Na Barack Obama
Tunaishi katika wakati ambapo changamoto za kiuchumi za kimataifa haziwezi kushughulikiwa kwa hatua nusu nusu au na jitihada za nchi moja moja pekee. Hivi sasa viongozi wa Kundi la nchi 20 (G-20) wana wajibu wa kuchukua hatua kubwa, inayoshughulikia masuala yote kwa kina na inayoratibiwa kwa pamoja na sio tu kufufua uchumi bali pia ya kuanzisha zama mpya za shughuli za kiuchumi zitakazohakikisha kuwa mwanguko huu wa uchumi hautokei tena.
Hakuna atakayeweza kupinga kwamba tunahitaji kuchukua hatua za haraka. Tatizo la mikopo mibaya na kuporomoka kwa imani ya watu kwa mabenki na mfumo mzima wa fedha limetapakaa bila kujali mipaka ya nchi huku athari zake zikiigusa kila kona ya dunia yetu. Kwa mara ya kwanza katika kizazi hiki, uchumi wa dunia umeporomoka na biashara imeshuka.
Fedha nyingi, kiasi cha Matrilioni ya dola, zimepotea, mabenki yameacha kutoa mikopo, makumi ya mamilioni ya watu watapoteza ajira zao duniani kote. Ustawi wa kila nchi upo mashakani, hii ikiwa ni pamoja na uimara wa serikali na hali ya maisha ya watu, hususan katika nchi zilizo masikini zaidi duniani.
Mwanzo na mwisho, tumejifunza kuwa mafanikio ya uchumi wa Marekani yameungana na hayatenganishiki na uchumi wa dunia. Hakuna mstari unaotenganisha hatua tunazoweza kuzichukua kufufua uchumi wetu ndani ya mipaka yetu na zile zinazoweza kuchangia kuuimarisha uchumi huo zinazotakiwa kuchukuliwa nje ya mipaka yetu.
Kama watu wa nchi nyingine hawawezi kununua bidhaa, ni wazi kuwa masoko yataporomoka — tayari hivi sasa tunashuhudia kupungua kwa kiwango kikubwa zaidi kwa mauzo ya bidhaa za Marekani nje ya nchi, katika miongo minne iliyopita, jambo ambalo moja kwa moja linasababisha Wamarekani kupoteza ajira zao. Na iwapo tutaendelea kuziachia taasisi za fedha duniani kufanya mambo yao kwa ubinafsi, ulafi na bila kuwajibika kikamilifu tutaendelea kubaki katika mzunguko usio endelevu wa kupanda na kuporomoka kwa uchumi. Ni kwa sababu hiyo Mkutano ujao wa London ni muhimu sana katika jitihada za kufufua uchumi wetu ndani ya Marekani.
Ujumbe wangu upo wazi: Marekani ipo tayari kuongoza jitihada za kimataifa za kufufua uchumi, na kwa hakika tunatoa wito kwa wabia wetu kuungana nasi, kuchukua hatua zinazopaswa kwa haraka tukiwa na lengo la pamoja. Tayari kazi kubwa imefanyika, lakini bado tuna kazi kubwa mbele yetu.
Uongozi wetu, unajengwa katika msingi mmoja mkuu ambao ni rahisi kueleweka: Tutachukua hatua thabiti za kuukwamua uchumi wa Marekani kutoka katika mgogoro huu wa sasa na kufanya mageuzi makubwa katika mifumo yetu ya udhibiti. Hatua hizi zitaimarishwa na hatua sahihi za udhibiti zitakazochukuliwa na nchi nyingine. Mathalan, Marekani inaweza kusaidia jitihada ya kufufua uchumi wa dunia na kurejesha imani ya watu kwa taasisi na mfumo mzima wa fedha duniani; na iwapo Mkutano wa London utasaidia kuchukuliwa kwa hatua thabiti za pamoja, basi jitihada zetu za kufufua uchumi zitakuwa na mafanikio, na migogoro ya kiuchumi inayoweza kujitokeza baadaye kuweza kuepukwa.
Ni lazima jitihada zetu zianze kwa kuchukua hatua thabiti za kuchochea ukuaji wa uchumi. Tayari Marekani imeshapitisha Sheria ya Kufufua Uchumi na Kuongeza Mitaji (the American Recovery and Reinvestment Act) — ambayo ni mojawapo ya hatua kubwa ya kusaidia kutengeneza nafasi za ajira na kuweka msingi wa ukuaji uchumi kwa kizazi hiki.
Nchi nyingine wanachama wa Kundi la Nchi 20 nazo pia zimechukua hatua mbalimbali za kusaidia kufufua na kuimarisha taasisi na mifumo ya kifedha (fiscal stimulus). Ni lazima hatua hizi ziimarishwe zaidi na kuendelezwa hadi hapo imani ya watu itakaporejea na mahitaji/matumizi ya watu yatakaporejea katika hali ya kawaida. Tunapopiga hatua kwenda mbele, ni lazima tuzingatie azma na dhamira yetu ya pamoja ya kukuza biashara na uwekezaji kwa njia huru na wazi kabisa huku tukikataa hali ya kila nchi kulinda masoko yake dhidi ya bidhaa na huduma kutoka nchi nyingine (protectionism), hali ambayo inaweza kuongeza mgogoro uliopo.
Pili, tunatakiwa kurejesha utoaji wa mikopo – mikopo ambayo inategemewa sana na wafanyabiashara na hata walaji. Nchini Marekani tunafanya jitihada za dhati za kuimarisha mfumo wetu wa fedha. Jitihada hizi ni pamoja na kuhakikisha kuwa Mabenki yetu makubwa yanatoa mahesabu ya mizania yao kwa ukweli, uadilifu na usahihi. Tunaamini kuwa jambo hili litayawezesha mabenki hayo kutoa mikopo itakayowasaidia Wamarekani kununua bidhaa, kubaki katika nyumba zao na kukuza biashara zao.
Jambo hili ni lazima liendelee kuimarishwa na hatua zitakazochukuliwa na wabia wetu ambao ni wanachama wa Kundi la G-20. Kwa pamoja tunaweza kuwa na mpango wa pamoja unaosisitiza uwazi, uwajibikaji unaolenga katika kurejesha hali ya utoaji na upatikanaji wa mikopo jambo ambalo huwezesha ukuaji wa uchumi wa dunia. Hali kadhalika, nchi wanachama wa G-20 pamoja na taasisi za kimataifa zinaweza kutoa fedha za kusaidia kuinua biashara ya kimataifa na kuongeza ajira.
Tatu, tuna wajibu wa kiuchumi, kiusalama na kimaadili wa kutoa misaada kwa nchi na watu masikini na walio katika hatari zaidi ya kuathiriwa na mgogoro huu. Tutakapowaacha watu hao peke yao, mateso yatayosababishwa na mgogoro huu yatakuwa makubwa zaidi, na mafanikio katika jitihada za kufufua uchumi wetu yatachelewa kwa sababu masoko ya bidhaa zetu yatapungua na Wamarekani wengi zaidi watapoteza kazi zao.
Nchi wanachama wa G-20 ni lazima zichukue hatua za haraka za kutoa rasilimali ili kuzuia kuyumba na kuanguka kwa masoko katika nchi changa (emerging markets), kuongeza uwezo wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wa kukabiliana na dharura mbalimbali na kuyasaidia mabenki ya maendeleo ya kanda kuongeza kasi na kiwango cha utoaji wa mikopo. Wakati huo huo, Marekani itasaidia uwekezaji mkubwa katika suala la uhakika/usalama wa chakula ili watu masikini sana waweze kukabiliana na kipindi kigumu sana kinachokuja mbele yetu.
Wakati ambapo hatua hizi zinaweza kutusaidia kujikwamua kutoka katika mgogoro wa sasa wa kiuchumi, hatuwezi kukubali kurejea katika hali yetu ya awali. Ni lazima tukomeshe hali ya ulafi na hila za wafanyabishara na vyombo vya fedha za kujitajirisha haraka haraka(reckless speculation)na tabia ya kutumia zaidi ya mapato yetu. Aidha, ni lazima tukomeshe hali ya kuwepo mikopo mibaya na isiyolipika, mabenki yanayojiendesha bila kanuni imara na kukosekana kwa hali ya kuona mbali, mambo ambayo hutupeleka katika kuwa na ukuaji usio endelevu wa uchumi.
Ni hatua za pamoja za kimataifa pekee ndizo zitakazoweza kudhibiti hali ya kutokuwajibika kwa taasisi za fedha iliyotuweka katika mgogoro huu. Ni kwa sababu hiyo, nimeona ni vyema nitumie kikamilifu fursa hii kupendekeza kwenu mageuzi makubwa katika mfumo wetu wa udhibiti na usimamizi.
Taasisi zetu zote za fedha — katika soko la mitaji la Marekani (la Wall Street) na duniani kote — zinatakiwa ziwe na mtazamo thabiti wa kuangalia hali ya baadaye (strong oversight) na kuongozwa na busara na hekima katika shughuli zao. Aidha, ni lazima masoko yote yajiwekee viwango na utaratibu ambao makampuni yatatoa taarifa zao kwa uwazi na uadilifu. Hali kadhalika ni lazima pawe na taratibu nzuri zinazosimamia mitaji na hivyo kuwalinda wawekezaji dhidi ya migogoro ya kiuchumi katika siku zijazo. Ni lazima tupige vita na kukomesha mifumo ya utoroshaji fedha na ukwepaji kodi (offshore tax havens)pamoja na ile inayowawezesha watu kuingiza fedha haramu katika mfumo halali wa fedha(money laundering).
Ni lazima tuwe na kanuni madhubuti zitakazohakikisha uwazi na uwajibikaji na kuwabana wale wote watakaotumia vibaya nafasi na fursa zao. Ni lazima sasa siku za watendaji (katika taasisi za kifedha) kujilipa malipo makubwa yasiyodhibitiwa zifikie ukingoni. Badala ya kuwa na mifumo ya utoaji mafao na marupurupu inayotupeleka chini, ni lazima sasa tuwe na taratibu zilizo wazi za kutoa motisha kwa tabia njema zinazoimarisha jitihada zetu za kwenda juu.
Ninaelewa kuwa Marekani ina sehemu yake ya lawama katika hali hii mbaya inayotukabili sote hivi leo. Lakini pia ninafahamu kuwa hatuhitajiki kuchagua kati ya mfumo holela na usio na huruma wa Kibepari na ule kandamizi wa uchumi unaosimamiwa na dola. Wowote kati ya mifumo hiyo miwili hautakuwa sahihi na utakaowasaidia watu wetu au watu wengine wowote.
Mkutano huu wa nchi wanachama wa G-20,unatoa fursa ya aina mpya ya ushirikiano wa kiuchumi wa kimataifa. Huu ni wakati wa kufanya kazi pamoja kufufua na kuendeleza ukuaji wa uchumi utakaotokana na masoko huru na imara yatakayochochea na kuimarisha ubunifu,kusaidia ujasiriamali na kupanua fursa.
Mataifa ya dunia yanategemeana. Marekani ipo tayari kuunga mkono na kusaidia jitihada za kimataifa za kuongeza ajira na kujenga uchumi endelevu. Kwa pamoja, tunaweza kujifunza kutokana na mgogoro huu wa kiuchumu na hivyo kuleta ustawi imara usiotetereka kwa karne ya 21.
Barack Obama ni Rais wa Marekani.




