Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Kiswahili By-Liner

Close Window Tom Vilsack <br>Waziri wa Kilimo wa Marekani
Tom Vilsack
Waziri wa Kilimo wa Marekani

Njaa Haina Mipaka

Aprili 21, 2009

Tom Vilsack – Waziri wa Kilimo wa Marekani

Wiki iliyopita nilishiriki katika mkutano wa kwanza kabisa wa Mawaziri wa kilimo katika historia ya nchi za G 20. Kilichowakutanisha mawaziri hao kutoka katika nchi hizo tajiri zaidi duniani ni azma yao ya pamoja ya kutokomeza njaa na kuboresha kipato na hali ya maisha ya watu katika nchi masikini zaidi duniani. Benki ya Dunia inakadiria kuwa takriban watu milioni 150 wamenaswa katika lindi la umasikini uliokithiri kutokana na athari za kuporomoka kwa uchumi duniani, kupanda kwa bei ya vyakula na bei za mafuta. Jambo hili limepunguza uwezo wa watu masikini duniani kupata chakula wanachohitaji ili kuweza kuwa na afya bora na hivyo kuendesha shughuli za uzalishaji na hivyo kumudu kukimu mahitaji yao ya siku hadi siku.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Obama, huko jijini London alikutana na viongozi wa nchi za G 20 ili kuanzisha jitihada za pamoja za jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi duniani. Ni katika mkutano huo ndipo Rais Obama alipotangaza kuwa ataliomba Bunge la Congress kuongeza mara mbili msaada wa fedha utolewao na Marekani kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya kilimo katika nchi masikini hadi kufikia zaidi ya dola za Kimarekani bilioni moja ifikapo mwaka 2010. Wiki moja baadaye, Katika Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Msaada wa Chakula uliofanyika huko Kansas City, nilitangaza kutoa nyongeza ya Dola za Kimarekani milioni 80 ili kugharimia Miradi minne zaidi ya kutoa chakula mashuleni na lishe kwa watoto (McGovern-Dole International for Education and Child Nutrition Projects) inayotarajiwa kutoa chakula kwa watoto 655,000 barani Africa.

Kwa nini hatua hizi ni muhimu? Kwa pamoja, hatua hizi zinaunda mchakato wa kuwasaidia watu kupata uhakika wa chakula kwa ajili ya leo na kesho yaani siku za baadaye. Hivi sasa tunasaidia katika kuwawezesha watu kukidhi mahitaji yao ya muda mfupi kwa kupitia programu za utoaji misaada ya chakula. Historia nzuri ya Marekani ya utoaji wa msaada wa chakula ilianza baada ya Vita Kuu ya II ya Dunia. Kwa zaidi ya miaka 10, Marekani imetoa takriban nusu ya misaada yote ya chakula iliyotolewa na wafadhili. Wakati ambapo Marekani ikiendelea kuwa mtoaji mkubwa zaidi wa msaada wa chakula, hasa kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na wakulima, mashirika ya kujitolea, vikundi vya watumia bidhaa na wazalishaji wa Marekani na hata raia wa kawaida ambao wangependa kuchangia mafanikio ya Marekani na watu wengine, tunatakiwa pia kuwasaidia watu kujenga uwezo wa kujilisha wao wenyewe katika siku zijazo.

Hivi sasa tunakabiliwa na hali ambayo uzalishaji wa mazao ya kilimo ni mdogo kuliko mahitaji yaliyopo. Kwa ombi hili kwa Bunge la Congress, Rais Obama ameonyesha azma yake ya dhati ya kutatua mzunguko usiokwisha wa tatizo la umasikini na njaa linalowazingira zaidi ya watu bilioni moja duniani kote. Hatua ya Rais itazisaidia nchi zinazoendelea kuongeza uzalishaji wao kwa eneo na kuleta ustawi miongoni mwa watu wa vijijini. Kwa maana hiyo tunatoa nyenzo ambazo watu wanazihitaji ili kujikwamua kutoka katika umasikini na njaa

Janga la utapiamlo na njaa halijui mipaka ya nchi. Katika mkutano wa wiki iliyopita wa mawaziri wa kilimo wa G 8 niliwaambia mawaziri wenzangu, kama ninavyowaeleza raia wetu kuwa, utawala huu umedhamiria kwa dhati – na kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kuwa chakula salama, cha kutosha na chenye ubora kinapatikana kwa Wamarekani wote na kwa watu wote duniani.