By-Liner
Nguvu ya Sera Nzuri
20 Agosti, 2009
Na: Karl Fickenscher
Hali ya kuporomoka kwa uchumi duniani imezilazimisha serikali na taasisi mbalimbali duniani kwa mara nyigine tena kuangalia kwa undani manufaa yanayopatikana kutokana na misaada ya kimataifa. Inapokuja katika suala la kutoa misaada ya maendeleo kwa nchi mbalimbali duniani, Marekani inaendelea kutekeleza dhamira yake ya dhati kufanya hivyo kwa namna ambayo itawezesha kufikiwa kwa matokeo endelevu na kuleta mabadiliko ya kudumu katika maisha ya masikini. Kwa kuzingatia dhamira hii, Mfuko wa Serikali ya Marekani wa Changamoto za Maendeleo ya Milenia (MCC) umekuwa ukiimarisha uwajibikaji katika utoaji wa misaada ya kimataifa kwa kushirikiana na nchi ambazo nazo zina dhamira ya dhati ya kutekeleza sera nzuri za siasa, uchumi na kijamii.
Sera nzuri ni msingi wa kupatikana kwa matokeo endelevu ya jitihada za kuondoa umasikini na kukuza uchumi. Nchi inahitaji kuwa na sera nzuri ili kulinda utawala wa sheria, haki za kisiasa, chaguzi huru na za haki na misingi mingine ya utawala bora na wa kidemokrasia pamoja na ushiriki wa jumuiya huru za kiraia. Aidha, nchi inahitaji kuwa na sera nzuri ili kuimarisha afya na elimu ya raia wake wote ikiwa ni pamoja na wasichana na wanawake. Hali kadhalika, nchi inahitaji sera nzuri ili kujenga mazingira mazuri ya kibiashara, kuongeza fursa za ajira na kushiriki katika shughuli za kibiashara. Ni lazima kuwa na sera zinazotekelezeka ili kudhibiti rushwa.
Ni kwa sababu hiyo, MCC inashirikiana na serikali zilizodhamiria kutawala kwa haki, zikiwekeza katika afya na elimu ya watu wake na kupanua uhuru wa kiuchumi. MCC hutumia vigezo 17 vya kisera – vilivyoandalia na taasisi inayojitegemea, isiyofungamana na MCC au washirika wake – katika kuamua ni nani wanaweza kuwa wabia wetu wazuri katika kukabiliana na umasikini duniani. Kwa kuelekeza jitihada zetu katika nchi zilizo na dhamira ya dhati ya kufanya vyema katika kutekeleza vigezo hivyo vya kisera, tunaamini kuwa uwekezaji wetu utakuwa na matokeo makubwa sana katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini. Kinyume chake ni kwamba, nchi inaposhindwa kutekeleza kikamilifu sera hizo inapunguza uwezo wake wa kupunguza umasikini na kuinua uchumi wake. Utaratibu wa kushirikiana na nchi kwa misingi ya utekelezaji wake wa sera ni msingi muhimu katika utendaji wa MCC.
Tanzania ni mbia wa MCC ambaye hadi hivi sasa inapokea fungu kubwa zaidi kutoka katika mfuko huu duniani. Mwaka 2008, Tanzania ilifuzu kutoka programu ya mwanzo ya MCC iliyolenga katika shughuli za kukabiliana na rushwa hadi kupatiwa fungu la kiasi cha Dola za Kimarekani 698 milioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika sekta za usafirishaji, nishati na maji. Kama sehemu ya makubaliano ya mkataba, kila nchi inayopokea msaada wa MCC, ikiwemo Tanzania, ina wajibu wa kukazia na kuboresha zaidi utendaji wake katika kutekeleza vigezo 17 vya kisera vinavyotumiwa na MCC. Pale nchi inaposhindwa kufanya hivyo, MCC inaweza (na kwa kweli imeshawahi kufanya hivyo) kusitisha au kukatisha kabisa msaada wake. Tunapongeza jitihada zinazoendelea za Serikali ya Tanzania za kutekeleza na kuboresha zaidi utendaji wake wa masuala ya kisera katika kutawala kwa haki, kuwekeza katika watu wake na kupanua uhuru wa kiuchumi.
Sera nzuri huleta matokeo mazuri katika jitihada za kuleta maendeleo. Iwapo kweli tumedhamiria kuleta mabadiliko ya kudumu katika maisha ya watu masikini duniani, ikiwa ni pamoja wale waliopo hapa Tanzania, ni lazima tuwekeze katika sera zinazosaidia kuimarisha na kudumisha jitihada zetu za kukuza fursa za maendeleo. Utaratibu wa MCC wa kuzingatia masuala ya kisera katika mchakato wa kuleta maendeleo (policy performance-based approach to development) na kuzingatia ni kwa kiwango gani nchi inayoshirikiana nazo — ikiwemo Tanzania, zinavyozingatia na kutekeleza masuala hayo ya kisera – ni uthibitisho mzuri wa nguvu za sera nzuri katika kutimiza azma ya kupunguza umasikini na kuinua uchumi.
Karl Fickenscher ni Mkurugenzi Mkazi wa Millennium Challenge Corporation (MCC), mwenye jukumu la kushirikiana na MCA-Tanzania katika kutekeleza Mkataba baina ya MCC na Tanzania.




