Kiswahili By-Liner
Mwelekeo Mpya Katika Kuhakikisha Usalama Wa Chakula Na Kukabiliana Na Njaa
15 Oktoba 2009
Na Hillary Rodham Clinton
Kwa takriban watu bilioni moja duniani kote, jitihada za kila siku za kuzalisha, kuuza au kununua chakula ni harakati muhimu sana ambayo sio tu inatambulisha bali pia inakimu maisha yao. Hili ni jambo muhimu kwao, na kwetu sote.
Hebu tafakari kuhusu maisha ya kila siku ya mkulima mdogo wa kawaida.
Ni mwanamke aishie kijijini katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, katika bara Asia au Amerika ya Kusini na analima katika kipande cha ardhi ambacho yeye si mmiliki wake. Anaamka kabla hakujapambazuka na kutembea maili nyingi kwenda kuteka maji. Analima kutwa nzima, wakati mwingine akiwa na mtoto mgongoni.
Akibahatika, ukame, magonjwa au wadudu na wanyama waharibifu hawataharibu mazao yake, hivyo ataweza kupata mavuno ya kutosha kulisha familia yake. Anaweza hata kupata ziada kwa ajili ya kuuza. Lakini hakuna barabara itakayomuwezesha kufikisha mazao yake katika soko lililo karibu na kijijini hapo hakuna anayeweza kumudu kununua mazao hayo.
Hebu sasa tutafakari kuhusu maisha ya kijana aliye katika jiji lililo umbali wa maili 100 kutoka katika kijiji cha mkulima huyo. Kijana huyu hana kazi – au hata akiwa nayo, ni ile yenye ujira mdogo sana usioweza kukimu maisha yake. Anakwenda sokoni – anakuta chakula kimeharibika, au kinauzwa kwa bei ambayo hawezi kuimudu. Ana njaa na mara nyingi anahasira.
Mkulima ana chakula cha ziada cha kuuza, na kijana huyu anataka kukinunua. Lakini biashara hii haiwezi kufanyika kutokana na masuala magumu kadhaa ambayo yapo nje ya uwezo wao.
Kukabiliana na tatizo la njaa duniani ni kitovu au msingi wa kile tunachokiita “usalama wa chakula” — kuwajengea uwezo wakulima kuzalisha na kuvuna mazao mengi, kuihudumia vyema mifugo yao au kuvua samaki wa kutosha— na hatimaye kuhakikisha kuwa chakula wanachokizalisha kinawafikia wale wanaokihitaji.
Usalama wa chakula si suala linalohusu chakula peke yake. Ni suala linalohusisha mambo mengi magumu na yanayofungamana: ukame na mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, huathiri uchumi wa dunia ambao nao huathiri bei za vyakula na kuhatarisha miundombinu muhimu. Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na hivyo kuongezeka kwa gharama za usafirishaji.
Usalama wa chakula ni suala la kiusalama. Njaa huhatarisha utulivu na usalama wa serikali, jamii na hata mahusiano kati ya nchi na nchi. Watu wanaokufa au waliodhoofika kwa njaa na ambao hawana kipato na hivyo kushindwa kuzihudumua familia zao hujikuta katika hali ya kukata tamaa. Kukata tamaa huko huongeza misuguano, migogoro na hata machafuko. Mwaka 2007, tulishuhudia machafuko yaliyosababishwa na ukosefu wa chakula katika zaidi ya nchi 60.
Kuanguka kwa kilimo katika maeneo mengi duniani— na vikwazo vingi vinavyomtenganisha mkulima na kijana mwenye njaa— vina athari kubwa sana katika uchumi wa dunia. Kilimo ni chanzo pekee au chanzo kikuu cha mapato kwa zaidi ya robo tatu ya watu masikini duniani kote. Pale ambapo binadamu hawa wengi wanapofanya kazi ngumu kwa bidii kubwa lakini bado wakashindwa kukidhi mahitaji ya familia zao, basi maendeleo ya dunia nzima hurudi nyuma.
Utawala wa Rais Obama unalichukulia tatizo la njaa iliyokithiri kama suala la kipaumbele katika sera zake za mambo ya nje. Nchi nyingine zinaungana nasi katika jitihada hizi. Nchi zilizopiga maendeleo makubwa ya viwanda zimeahidi kutoa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 22 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kusaidia ukuaji wa uchumi utokanao na kilimo. Hapo tarehe 26 Septemba mimi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa pamoja tuliongoza mkutano wa viongozi kutoka zaidi ya mataifa 130 ili kuhamasisha zaidi misaada ya kimataifa katika suala hili.
Mwelekeo wa Serikali ya Marekani katika kushughulikia suala la uhakika wa chakula unatokana na uzoefu wetu katika kushughulikia maendeleo. Ukweli ni kuwa, tumetumia miaka mingi na fedha nyingi sana katika miradi ambayo haikuweza kuleta matokeo endelevu. Lakini tumejifunza kutokana na jitihada hizo. Tunafahamu kuwa mikakati yenye mafanikio zaidi ni ile inayotoka kwa watu wanaokabiliwa na tatizo husika, na sio ile iliyobuniwa na serikali au taasisi za kigeni zilizo maelfu ya maili kutoka katika eneo husika. Aidha, tunaelewa kuwa jitihada za maendeleo zinakuwa na manufaa zaidi pale ambapo hazichukuliwi kama msaada bali kama uwekezaji.
Tukiwa na mafunzo haya, jitihada zetu za kuhakikisha usalama wa chakula zitaongozwa na misingi mikuu mitano, ambayo itatusaidia kuondoa mizizi ya tatizo hili na kuleta mabadiliko ya kudumu.
Kwanza, tunaelewa kuwa hakuna mfumo mmoja wa namna ya kuendeleza kilimo utakaozifaa nchi zote. Hivyo basi tutafanya kazi na nchi washirika wetu katika kuandaa na kutekeleza mipango yao wenyewe.
Pili, tutashughulikia vyanzo mbalimbali vinavyosababisha njaa kwa kuwekeza zaidi katika maeneo mbalimbali kuanzia mbegu bora hadi programu za kuwalinda wakulima kwa kuchangia sehemu ya hasara inayoweza kujitokeza (risk-sharing programs). Kwa kuwa wakulima wengi zaidi ni wanawake, ni muhimu sana uwekezaji wetu katika kilimo ukalenga katika kuwasaidia kufikia malengo yao na kujenga uwezo wao wa kuhimili shughuli za kilimo.
Tatu, hakuna eneo moja pekee litakaloweza kuondosha tatizo la njaa bila kuhusisha maeneo mengine. Iwapo wadau mbalimbali watafanya kazi pamoja na kuwa na uratibu katika ngazi ya taifa, kanda na kimataifa – basi matokeo ya jitihada zetu yataongezeka maradufu.
Nne, taasisi zisizo za kiserikali za kimataifa zina uwezo na rasilimali zinazovuka mipaka ya nchi. Kwa kusaidia jitihada za taasisi hizi, tutaweza kunufaika kutokana na utaalamu wao.
Mwisho, tunaahidi kuendelea kuunga mkono jitihada hizi kwa kipindi kirefu kijacho na kuhakikisha kuna uwajibikaji katika jitihada hizo. Ili kuthibitisha azma hii, tutawekeza katika kuweka taratibu za ufuatiliaji na tathmini zitakazouwesha umma kufuatilia na kuona nini tulichokifanya.
Jitihada hizi zitachukua miaka mingi, au pengine miongo kadhaa kabla hatujafikia matokeo halisi yanayohitajika, lakini tunaahidi kuendelea kuzichangia kwa hali na mali.
Wakati tukiendelea na jitihada hizi, tutaendelea kutekeleza ahadi yetu ya kutoa misaada ya dharura ya chakula katika maeneo yaliyoathiriwa na majanga – kama ilivyo hivi sasa katika maeneo ya Pembe ya Afrika ambapo ukame, kukosekana kwa mavuno na vita vya wenyewe kwa wenyewe vimesababisha maafa makubwa ya kibinaadamu katika kipindi cha miaka 18.
Kufufua kilimo duniani haitakuwa kazi rahisi. Kwa hakika ni mojawapo kati ya jitihada kubwa zaidi ya kidiplomasia na kimaendeleo kuwahi kuchukuliwa na nchi yetu. Lakini inawezekana na inastahili kuchukuliwa. Iwapo tutafanikiwa, basi maisha yetu ya baadaye yatakuwa na fanaka na amani zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.




