Speeches
Maadhimisho ya Miaka 233 ya Uhuru wa Marekani
Mahali: Ubalozi wa Marekani , Dar es Salaam
Jumamosi, Julai 4, 2009
Hotuba ya Kaimu Balozi wa Marekani Larry André (Kama ilivyotayarishwa)
Tarehe 4 Julai ya kila mwaka tunasherehekea siku ya kuzaliwa kwa taifa letu kwa kukumbuka maadili na amali muhimu ambazo kwayo taifa letu limejengwa. Utambulisho wetu wa kitaifa umejengwa katika misingi ambayo tunatumia maisha yetu yote na maisha ya taifa letu, kujitahidi kuitekeleza. Hatujaweza kuyatekeleza kikamilifu maadili hayo makuu. Mara kwa mara tumeanguka na hivyo kushindwa kuyatekeleza kikamilifu. Lakini tumedhamiria kwa nadhiri ya dhati kujitahidi kuyafuata na kuyatekeleza. Maadili ambayo kwayo misingi ya taifa letu imewekwa, yameorodhesha katika Hati Rasmi ya Uhuru kutoka kwa Waingereza. Hati hiyo inasisitizia uhuru na haki kwa wote. Kwa hakika, katika mwaka 1776, ambapo bado utumwa na tawala za kimabavu na ubabe vilikuwa ni sehemu ya kawaida ya maisha ya watu duniani kote, maadili haya yalikuwa ni ya kimapinduzi hasa.
Kauli nzito katika Hati ya Uhuru— kwamba “watu wote wameumbwa sawa” na kwamba kuna “haki fulani ambazo haziwezi kuachanishwa na mtu” ikiwa ni pamoja na “Haki ya Kuishi, Uhuru na kupata Furaha”— ni mambo ambayo yanachangiwa na watu wa tamaduni na imani tofauti. Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Nyerere, aliwahi kuzungumzia “lugha isiyochujuka katika Hati ya Uhuru” na kuiita hati hiyo kuwa “mojawapo kati ya nyaraka muhimu kabisa zilizopata kutolewa duniani.”
Ninafurahi kwamba mmeungana nasi katika kusherehekea maadili haya ambayo Wamarekani na Watanzania wanayaamini na kuyathamini sana. Tunapotekeleza jukumu letu lisilo na mwisho la kuyaweka maadili haya katika vitendo halisi pale tunaposhughulikia masuala mbalimbali yanayowakabili watu wetu hivi leo, tunaendelea kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu. Ubia kati ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umejengwa katika maadili haya ya pamoja. Ubia huu unaendelea kukua, kuimarika na kuleta matokeo mazuri kwa watu wa nchi zetu mbili.
Mwezi Mei, Rais Obama alimwalika Rais Kikwete, kukutana naye katika Ikulu ya Marekani (White House), akiwa ni Rais wa kwanza kutoka Afrika kupokea mwaliko huo. Kwa unyenyekevu, Rais Kikwete alikubali mwaliko huo. Rais Obama anafuatilia kwa karibu sana na kuguswa na matatizo makubwa yanayowakabili watu katika bara hili. Hivyo alikuwa akitafuta ushauri kwa Kiongozi wa Kiafrika aliyefahamu kuwa ni kiongozi mwenye busara, uzoefu mkubwa na anayehamasishwa na maadili ya pamoja ya uhuru, haki na uvumilivu. Viongozi hawa wawili walikubaliana kufanya kazi pamoja ili kutatua matatizo ya pamoja. Walibadilishana mawazo kuhusu njia nzuri zaidi ya kuimarisha ushirikiano wetu, ikiwa ni pamoja na njia za kuboresha sekta za afya, elimu na kilimo. Aidha, walijadili kuhusu namna ya kufanya kazi na wabia wengine mbalimbali katika kanda hii ili kutatua baadhi ya migogoro mikubwa inayoendelea hivi sasa barani Afrika. Tanzania ina historia iliyotukuka ya kuwasaidia Waafrika wengine ambao nchi zao zipo katika migogoro. Sisi Wamarekani tunathamini sana ushauri wa viongozi wa Tanzania katika jitihada zetu za kusaidia kutafuta ufumbuzi wa amani wa migogoro mingi inayoendelea hivi leo ambayo kwa kiwango kikubwa inakwamisha na kurudisha nyuma maendeleo.
Katika miaka ya karibuni, Marekani na Tanzania zimeshirikiana kwa karibu sana katika kuboresha maisha ya mamilioni ya watu nchini kote na kujenga tumaini la maisha bora ya baadaye. Orodha ya mafanikio yetu ni ndefu. Nitaeleza machache tu kati ya yale ambayo kwa pamoja tumeweza kuyafanikisha.
Mwaka huu, Serikali ya Marekani itachangia zaidi ya Dola za Kimarekani nusu bilioni kama msaada rasmi wa kiserikali. Wiki hii, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bw. Jacob Lew, alikuwa na ziara rasmi nchini Tanzania ili kujionea mwenyewe mafanikio ya ushirikiano wetu. Aidha, alidadisi kuhusu mapungufu katika utekelezaji miradi mbalimbali tunayoishughulikia, akiamini kuwa tunaweza kuboresha zaidi. Kuendelea kufanikiwa kwa shughuli zetu za ubia kutategemea sana azma ya dhati ya pande zote mbili ya kujitahidi bila kuchoka kupata matokeo mazuri zaidi.
Mbali na msaada rasmi wa kiserikali, ni muhimu pia tukatambua na kuheshimu kazi nzuri inayofanywa na raia wa kawaida wa Marekani wanaotoa mchango wao wa kitaalamu na hata fedha ili kusaidia jitihada za Watanzania za kujenga taifa imara, lenye afya na ustawi. Hali kadhalika, ni muhimu kutambua mchango wa wafanyabiashara wa Marekani ambao wamekuwa wakiwekeza katika vitega uchumi mbalimbali vinavyohitajika sana katika uchumi wa Tanzania.
Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Malaria (PMI), kwa ushirikiano na wabia wengine wa Kitanzania na wa Kimataifa, umewezesha kuondolewa kwa ugonjwa wa malaria kama tatizo kuu la kiafya kwa watu wa visiwa vya Zanzibar. Kazi iliyopo sasa ni kudumisha mafanikio yaliyopatikana na kuendeleza jitihada hizo katika jamii za Tanzania Bara zinazokabiliwa na tatizo kubwa la ugonjwa huu. Tumenunua vyandarua vyenye viatilifu zaidi ya milioni nne na kuvigawa kwa akinamama wajawazito na watoto walio katika chini ya umri wa miaka mitano. Aidha, rafiki zetu hapa bara wameweza kwa mafanikio makubwa kuanzisha mfumo wa hati-punguzo kwa kupitia ubia maalumu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Tunausaidia mfumo huu kwa lengo la kusaidia kufikisha mamilioni ya vyandarua kwa wananchi kwa njia endelevu.
Uzinduzi wa zaidi ya vituo 80 vya Ushauri Nasaha, Upimaji na Matibabu ya VVU/UKIMWI unaendelea nchini kote, huku kukiwa na kituo kimoja kinachozinduliwa karibu kila wiki. Vituo hivi vinatoa bure matibabu ya VVU/UKIMWI ambayo yameweza kuokoa maisha ya wagonjwa wengi kwa kutoa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs). Vituo hivi vinatoa pia huduma za kudhibiti maambukizo kwa kutoa ushauri nasaha na upimaji wa hiari vikiwatumia wataalamu wa afya wenye taaluma ya kutosha katika fani zao. Jitihada hizi kubwa za kukabiliana na janga hili la VVU/UKIMWI linalotishia maisha na ustawi wa jamii hii ni matokeo ya dira ya Rais wa sasa wa Tanzania na Rais wetu aliyepita. Rais Obama na Waziri wa Mambo ya Nje, Bibi Clinton wametambua mafanikio na umuhimu wa jitihada zetu za pamoja za kukabiliana na janga hili. Amri yao kwangu na kwa wenzangu ni kuendelea bila kuchoka na kazi nzuri ambayo tumeifanya hadi sasa.
Mwezi Septemba, kazi ya miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango/Mkataba wa Millennium Challenge ilianza. Mkataba huu wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 698— ambao ni mkataba wa Mpango wa Millenium Challenge wenye thamani kubwa zaidi duniani— utawezesha kuboreshwa kwa miundombinu ya usafirishaji, maji na nishati nchini Tanzania.
Wafanyakazi wetu wa Kujitolea wana historia ndefu ya kutoa huduma katika nchi hii nzuri. Tanzania ilikuwa nchi ya pili kuwapokea wafanyakazi wa kujitolea kutoka Marekani. Toka mwaka 1962, zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 2000 wamefanya kazi nchini Tanzania, wengi wao wakiwa ni walimu katika shule zilizo katika maeneo ya vijijini. Wafanyakazi wote wa kujitolea wanachangia kuzileta karibu zaidi nchi zetu mbili kwa kupitia mabadilishano ya kitamaduni. Ukweli ni kwamba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulika Masuala ya Afrika, Balozi Johnnie Carson – ambaye ni mwanadiplomasia wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kwa bara la Afrika – aliwahi kufanya kazi kama mfanyakazi wa kujitolea katika maeneo ya nyanda za juu kusini. Uzoefu wake nchini Tanzania ndiyo uliomuwezesha kukwea ngazi za uongozi katika kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Afrika.
Katika historia yenu yote, mmedhihirisha kwa vitendo kwamba mnajali sana na kuguswa na tabu na shida ambazo Waafrika wengine wanakabiliwa nazo kutokana na kunyimwa haki zao na machafuko. Tunaheshimu sana historia yenu iliyotukuka ya mshikamano na Waafrika wengine wenye shida mbalimbali, hususan, mchango wenu katika harakati dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi. Wakati raia wa Msumbiji, Burundi na Kongo walipozikimbia nchi zao, Tanzania iliwapa hifadhi. Isitoshe, kama ishara ya nia yake njema, Tanzania imewapa makumi ya maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi fursa ya kupata uraia wake. Mwaka jana, Tanzania iliongoza jitihada za Umoja wa Afrika za kurejesha mamlaka ya serikali ya Komoro katika kisiwa cha Anjouan.
Leo hii, kwa mara nyingine, watu wanaokabiliwa na taabu na mateso wametoa kilio chao, na Watanzania wamekisikia. Kwa pamoja, Marekani na Tanzania wanataka kuwasaidia watu wa Sudan ili kumaliza mateso makubwa yanayowapata watu huko Darfur. Uingereza na Marekani tulitoa vifaa na mafunzo kwa kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania cha kulinda amani huko Darfur. Tunaipongeza sana Tanzania kwa kujitoa kwake kikamilifu katika kuusaidia Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Sudan kwa kutoa askari wake kujiunga na Kikosi Maalumu cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika cha Kulinda Amani Darfur (UNAMID). Kwa niaba ya watu wa Marekani, ninapenda kutoa pongezi za dhati kwa uongozi wa kiraia na kijeshi wa Tanzania kwa azma yao ya dhati ya kutatua migogoro barani Afrika kwa amani. Kwa hakika hii ni kazi kubwa na nzito. Askari wa Tanzania huko Darfur wanastahili heshima na pongezi zetu za kiwango cha juu.
Hivi sasa Wamarekani wanajadiliana kuhusu mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta za elimu, afya na fedha. Hali kadhalika, Tanzania inapita katika kipindi cha majadiliano makali na mageuzi. Huko Marekani, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tumeshuhudia kesi kubwa kubwa za rushwa. Vivyo hivyo hapa Tanzania. Kwa kuwa maafisa wa serikali na wanasiasa wanateuliwa au kuchaguliwa miongoni mwa wanadamu ambao si malaika, ni wazi kwamba baadhi yao wanaweza kushawishika na kusaliti imani na dhamana ambayo umma imewapatia kutokana na tamaa. Kwa kiwango fulani serikali zote duniani zinakabiliwa na ugonjwa huu. Tofauti ni kwamba katika baadhi ya nchi maafisa waandamizi wanaonekana kuwa wapo juu ya sheria na hivyo kuwa huru kuwaibia wananchi kwa kadri wapendavyo. Katika miezi 12 iliyopita, watu mashuhuri huko Marekani na hapa Tanzania wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za rushwa. Nchi zetu mbili zinaamini kwa dhati katika utawala wa sheria na kusisitizia msingi wa uadilifu kwamba serikali ni mtumishi wa watu na sio njia ya watu wachache waroho na wasio waaminifu kujitajirisha. Sote tunaweza kuboresha zaidi mapambano dhidi ya hali hii.
Mwaka mmoja kutoka sasa Tanzania itakuwa katika homa na vugu vugu la uchaguzi. Hivi punde tu, nasi tumetoka katika homa hiyo! Ni maoni yetu kuwa, ushindani wa kisiasa umewezesha kuboreshwa kwa utawala katika Tanzania bara. Hata hivyo huko Zanzibar, kama ambavyo uzoefu wa chaguzi zilizopita unavyotuonyesha, dhana kwamba raia wapo huru kuchagua viongozi wao bila hofu ya vitisho, matumizi ya nguvu na udanganyifu haijaweza kuheshimiwa na kutekelezwa kwa vitendo. Rais Kikwete ametangaza bayana azma yake ya kuona kuwa maridhiano yanafikiwa huko Zanzibar kwa kupitia Mwafaka wa Kisiasa unaolinda maslahi halali ya kambi zote kuu za kisiasa visiwani humo. Tunatoa wito wa kuharakishwa kwa jitihada hizi ili uchaguzi mkuu wa Tanzania usigubikwe tena na matukio ya kusikitisha huko Zanzibar kama yale tuliyoyashuhudia mwaka 2000 na 2005.
Kama mnavyofahamu, Rais Obama amemteua Jenerali Alfonso Lenhardt kuwa Balozi wake- mteuliwa nchini Tanzania. Iwapo uteuzi huu wa Rais utaidhinishwa na Bunge la Seneti la Marekani, Balozi Lenhardt atakuja nchini Tanzania akiwa na hazina kubwa ya uzoefu wa utendaji na uongozi katika ngazi za juu. Hivi sasa yeye ni Rais wa Baraza la Taifa la Kuzuia Uhalifu. Aidha, amewahi kuhudumu kama Mkuu wa Usalama wa Bunge la Seneti la Marekani, katika kipindi cha mashambulizi ya kigaidi ya 9/11 na mashambulizi ya kimeta. Utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu kwa miaka 31akiwa katika Jeshi la Marekani unajumuisha uongozi katika vikosi vyetu vya polisi wa kijeshi. Nimepata heshima ya kukutana na Jenerali Lenhardt. Ana shauku kubwa sana ya kuja kuuongoza Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na kushirikiana na uongozi wa juu wa nchi hii pamoja na wanadiplomasia wenzake wengine. Aidha ameelezea nia yake ya kutembelea kila pembe ya Tanzania ili aweze moja kwa moja kusikia maoni ya wananchi kuhusu namna tunavyoweza kuimarisha zaidi ubia wetu.
Tarehe 4 Julai 1776 waasisi wetu walisherehekea mwanzo wa safari ya taifa letu wakati taifa hilo changa likiwa bado linapigania uhai wake. Hivi leo, tarehe 4 Julai, miaka mia mbili na thelathini na tatu baadaye, kama Wamarekani, Watanzania na marafiki wetu wote, basi tusherehekee safari yetu pamoja: safari ya urafiki, ushirikiano na heshima inayojengwa katika msingi wa maadili ya pamoja. Sote kwa dhamira ya dhati tukubaline kudumisha na kuongeza jitihada zetu za kuboresha ubia wetu kwa niaba ya watu wa nchi zetu mbili.
Asanteni sana!




