Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba ya Dr. Mohamed Mfaume, Afisa Programu – Matibabu, Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Marekani (CDC) (Kama ilivyoandaliwa) Kukabidhi Magari kwa Hospitali za Wilaya
Skip Left Section Navigation

Hotuba

Kukabidhi Magari kwa Hospitali za Wilaya

22 Julai, 2009

Hotuba ya Dr. Mohamed Mfaume, Afisa Programu – Matibabu, Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Marekani (CDC) (Kama ilivyoandaliwa)

Nina furaha kubwa kuwa nanyi hivi leo, katika hafla hii fupi ya kukabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Hospitali ya Wilaya ya Ngorongoro na Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga funguo za magari matatu mapya kabisa, aina ya Toyota Land Cruiser ya mwaka 2009, yaliyotolewa kwa ufadhili wa watu wa Marekani.

Hata hivyo, funguo hizi hazitafungua tu milango ya magari haya, bali pia zitafungua milango ya huduma bora za afya kwa maelfu ya wananchi wanaohudumiwa na taasisi hizi za afya.

Msaada huu unatokana na ufadhili wa watu wa Marekani kwa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) na ni sehemu ya jitihada za kutekeleza ahadi ya kuimarisha uwezo wa Tanzania katika kutoa matibabu na huduma nyingine kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI.

PEPFAR inagharimia pia miradi ya kuboresha na kupanua huduma za ushauri nasaha, upimaji na matibabu kwa watu wanaoishi na VVU nchini kote Tanzania, ambapo zaidi ya vituo 80 vinavyotoa huduma hizo vimefunguliwa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita. Lakini shughuli za uboreshaji wa huduma hizo haziishii tu kwa kumalizika kujengwa kwa majengo ya vituo hivyo au baada ya kukata utepe ili kuyazindua.

Magari haya yatasaidia sana katika kutoa huduma ya usafiri hasa kwa wagonjwa waishio mbali na vituo. Aidha, wagonjwa ambao wanahitaji huduma za rufaa hivi sasa wataweza kufika katika vituo vya afya watakapoweza kupata huduma hizo kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Hali kadhalika, magari haya yatasaidia katika kusafirisha madawa na vifaa vingine vya kitabibu na kuwezesha utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa walio majumbani na kusaidia shughuli za mafunzo miongoni mwa wahudumu wa afya wa vituo mbalimbali.

Ninapenda kuishukuru na kuipongeza taasisi ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) kwa kazi kubwa inayoifanya. Wakiwa ni watekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na PEPFAR, na wenyeji wetu hii leo, EGPAF imefanya kazi kubwa ya kutayarisha na kuendesha programu za matunzo na matibabu.

Mwisho, napenda kuwashukuru wafanyakazi na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga na Hospitali ya Wilaya ya Ngorongoro. Ni heshima kwangu kuwakabidhi funguo na umiliki kamili wa magari haya. Kwa niaba ya watu wa Marekani, napenda niwapongeze kwa kujitoa kwenu kwa moyo wote, bila kuchoka kuboresha maisha na afya ya nchi hii.

Tutaendelea kufanya kazi pamoja nanyi na taifa lote la Tanzania katika kuhakikisha tunafikia maono ya Rais Kikwete ya kuwa na “Tanzania bila UKIMWI". Tunaamini inawezekana. Ahsanteni Sana.

 
Article translated in: