Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba ya Larry André, Kaimu Balozi Katika Hafla ya Kumkaribisha Nyumbani Mchezaji wa Memphis Grizzlies, Hasheem Thabeet
Skip Left Section Navigation

Hotuba

Hafla ya Kumkaribisha Nyumbani Mchezaji wa Memphis Grizzlies, Hasheem Thabeet

Ilipofanyika: Nyumbani kwa Kaimu Balozi

Tarehe 17 Agosti 2009

Hotuba ya Larry André, Kaimu Balozi

 

  • Ndugu Leonard Thadeo, Mkurugenzi wa Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, viongozi wa michezo, utamaduni na vyombo vya habari,mabalozi wenzangu, mabibi and mabwana.

  •  

  • Ni furaha na heshima kwangu kuwa mwenyeji wa hadhira hii hapa nyumbani kwangu jioni ya leo. Ninawashukuru kwa kuungana nasi katika kumkaribisha nyumbani Tanzania – mchezaji nyota anayeibukia kwa kasi -- Hasheem Thabeet. Ninapenda kumkaribisha kipekee, Bi. Rukia Thabeet Manka, mama wa Hasheem pamoja na familia yake yote na marafiki wengi waliojumuika pamoja nasi hivi leo.

  •  

  • Tukiungana pamoja na watu wengine wengi kutoka pande zote za Tanzania tuliangalia kwa shauku na matazamio makubwa zoezi la mwaka huu la uchaguzi wa wachezaji wapya wanaojiunga na ligi kubwa na bora zaidi ya mpira wa kikapu duniani, ligi ya NBA nchini Marekani. Usiku ule, mwishoni mwa mwezi Juni, tulilipuka kwa furaha, pale Hasheem alipochaguliwa katika mzunguko wa kwanza kuwa mchezaji wa pili kujiunga na ligi hiyo akichezea timu ya Memphis Grizzlies.

  •  

  • Akiwa ni Mtanzania wa kwanza kuchaguliwa kucheza katika ligi ya NBA, tulifurahishwa sana na mafanikio ya Hasheem. Je kuna balozi mzuri zaidi wa mchezo huu kati ya Marekani na Tanzania kuliko kijana aliyekulia Sinza, jijini Dar es Salaam na aliyekuwa mwanafunzi na Mchezaji katika Chuo Kikuu cha Connecticut akiwa katika programu ya mabadilishano (exchange student program), na sasa akiwa amechaguliwa kuwa mchezaji wa kulipwa wa mpira wa kikapu nchini Marekani?

  •  

  • Kilichoongeza shauku yetu katika kufuatilia maendeleo ya Hasheem, ni jinsi tunavyomfahamu yeye kama mtu binafsi. Kwa miaka mingi Thabeet amekuwa ni rafiki wa ubalozi wetu na amechangia muda na kipaji chake katika kusambaza ujumbe kwamba mafanikio yanawezekana kwa kufanya kazi kwa bidii.

  •  

  • Mojawapo kati ya mifano ya kujitoa kwake kwa dhati akionyesha moyo wa kiuanamichezo, ni pale Hasheem alipotembelea Tanzania mwaka jana ambapo alijitolea kuzungumza na vijana wa Kitanzania waliokuwa wakijiandaa kwenda Marekani kujiunga na vyuo na vyuo vikuu mbalimbali. Alichangia uzoefu wake kuhusu namna ya kuweka uwiano kati ya michezo na masomo ya darasani na kuwapa moyo vijana wa Kitanzania kuweza kufikia upeo wa uwezo wao katika kutumia vyema fursa waliyoipata ya kusoma katika vyuo vikuu vya Marekani.

  •  

  • Mafanikio ya Hasheem yanaonyesha kuwa jitihada na dhamira ya dhati humuwezesha mtu kufikia ndoto zake. Katika jamii huru kama Marekani na Tanzania mafanikio makubwa katika michezo, kama ilivyo kwa muziki, sanaa za ubunifu na kazi nyingine za sanaa hupatikana kwa wale wanaojituma kwa bidii katika kutimiza malengo yao na wala si vinginevyo. Ukweli ni kuwa jamii hustawi kutegemeana na kiwango ambacho mafanikio yanapatikana kwa wote na si watu wachache tu. Katika nyanja zote za maisha katika jamii za Kimarekani na Kitanzania tunaweza kupata funzo muhimu kutoka kwa wanamichezo wetu kwamba kiwango cha mafanikio au tuzo ambayo mtu anaipata hutokana na jitihada binafsi.

  •  

  • Michezo huweza kuleta usawa ikiwawezesha watu kutoka tamaduni, imani au hata hali tofauti za kiuchumi kuwa na fursa sawa ya kufikia viwango vya juu vya umahiri kabisa katika michezo hiyo, kwani wanamichezo hupimwa kwa jinsi wanavyocheza michezo yao na sio kwa kigezo cha mahali wanapotoka au mtu wanayemfahamu. Tunaposhiriki katika michezo kimataifa umoja na kufanana kwetu kunadhihirishwa kwa kiwango kikubwa sana ambacho hakiwezi kuelezewa na hotuba yeyote ya kisiasa. Kwa hakika michezo ni lugha ya kimataifa.

  •  

  • Mafanikio ya Hasheem katika mpira wa kikapu yanamaanisha pia kuwa vijana wengi zaidi wa Kitanzania sasa watakuwa na hamasa zaidi ya kucheza mchezo huu. Ili kusaidia kuuinua zaid mchezo huu nchini, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania unafanya kazi kwa karibu na Chama cha Mpira wa Kikapu cha Tanzania na Chama cha Mpira wa Kikapu cha Dar es Salaam.

  •  

  • Mwezi Septemba mwaka jana, Ubalozi wa Marekani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ulimleta nchini Tanzania Jennifer Azzi, mchezaji mahiri anayechezea ligi kuu ya wanawake ya mpira wa kikapu ya WNBA na Mshindi wa Medali ya Dhahabu katika michezo ya Olimpiki pamoja na Matt Bonner, ambaye ni mchezaji wa timu ya Antonio Spurs inayocheza katika ligi ya NBA. Wachezaji hawa waliendesha warsha kwa ajili ya wachezaji wa vilabu mbalimbali vya mpira wa kikapu, makocha na wanafunzi wa shule za sekondari.

  •  

  • Kutokana na hamasa hii kwa mpira wa kikapu nchini Tanzania na Marekani, ikitiliwa nguvu na mapenzi makubwa ya Marais Barack Obama na Jakaya Kikwete kwa mchezo huu, ninachukua nafasi hii kutangaza fursa nyingine ya kuuendeleza mchezo huu ambayo hivi sasa Ubalozi ukishirikiana na wadau mbalimbali inaishughulikia. Hapo mwezi Septemba tunapanga kuwapeleka makocha kadhaa wa Kitanzania wa mpira wa kikapu kwa ajili ya kuhudhuria warsha kuhusu mchezo huo huku gharama zote zikiwa zimelipiwa na Watu wa Marekani. Tunatarajia kuwa warsha hii ya makocha itakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa miaka mingi ijayo, kwani wachezaji wapya humasishwa zaidi makocha wenye ari na uzoefu mkubwa katika mchezo husika.

  •  

  • Hasheem, mafanikio yako kama Mtanzania wa kwanza kucheza katika ligi ya NBA yamefungua ukurasa mpya katika ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani. Ni heshima kubwa kwangu kukupongeza kwa mafanikio makubwa uliyoyapata kutokana na jitihada na mapenzi yako kwa mchezo huu. Hongera sana.

  •  

     
    Tukio Katika Picha

    Photos: Hafla ya Kumkaribisha Hasheem Thabeet
    [Ingia]

    Article translated in: