Hotuba
Hotuba ya Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Larry André (Kama ilivyotayarishwa)
Katika Hafla ya Kuwaapisha Wafanyakazi Wapya wa Kujitolea - Peace Corps Nchini Tanzania
Mahali: Nyumbani Kwa Balozi wa Marekani Nchini Tanzania
Tarehe 19 Agosti 2009
Kaimu Katibu Mkuu, Eric Shitindi, Mgeni Rasmi, Mwakilishi wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Viongozi wa Serikali,
Wageni Waalikwa,
Wawakilishi wa taasisi zinazotoa huduma,
Waajiriwa na Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps
Mabibi na Mabwana,
Ninajisikia mwenye furaha kubwa, na kwa hakika ninaona fahari ninapojiandaa kuwaapisha Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps 32 watakaofanya kazi katika sekta za Afya na Mazingira waliopo mbele yetu hivi leo. Aidha, tukio hili linanikumbusha mbali. Ninafurahi kuona kuwa wafanyakazi wa Kujitolea na taasisi ya Peace Corps inaendelea kushamiri, ikiendelea kuimarisha mahusiano kati ya Wamarekani na Watanzania katika moyo wa utoaji huduma. Nina fahari kuuwakilisha Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na kwa hiyo kupewa heshima ya kuwaapisha wahitimu hawa wanaokwenda kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea. Tukio hili linanikumbusha mbali – wakati mimi mwenyewe nilipokuwa Mfanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps.
Nilikuwa Mfanyakazi wa Kujitolewa wa Peace Corps katika nchi ya Senegal huko Afrika Magharibi. Uzoefu nilioupata huko ulibadilisha maisha yangu kwa kiwango ambacho sikukitarajia. Kabla ya kuhudumu kama Mfanyakazi wa Kujitolewa wa Peace Corps sikuwa na shauku sana kuhusu masuala ya Afrika. Lakini baada ya kuhudumu kama Mfanyakazi wa Kujitolea, niliamua kuishi na kujenga maisha yangu Afrika. Katika maisha yangu yote ya kikazi, nchini Chad, Nigeria, Cameroon, Guinea, Kenya na Tanzania, nimefurahi sana kubadilishana uzoefu na wafanyakazi wa kujitolea. Mimi na Balozi wa Marekani nchini Sierra Leone, (ambaye pia aliwahi kuwa mfanyakazi wa kujitolea) pamoja nami, tulipeleka ombi kwa uongozi wa Peace Corps tukitaka kurejeshwa kwa wafanyakazi wa kujitolewa wa Peace Corps nchini humo, tukieleza jinsi Rais wa nchi hiyo alivyoeleza huku machozi yakilengalenga wema aliofanyiwa akiwa mvulana mdogo na Mwalimu aliyekuwa mfanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps. Mkiwa Wafanyakazi wa Kujitolewa wa Peace Corps mnaweza msipate picha kamili ya ukubwa wa mabadiliko mnayoweza kuyafanya katika maisha ya watu wengine.
Ninapenda kutoa shukrani za kipekee kwa wawakilishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Afya na TAMISEMI. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu wa karibu na Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps, kama hawa watakaohitimu hivi leo.
Mafanikio ya wafanyakazi wetu wa kujitolea katika sekta za afya na mazingira yanatokana na ushauri na mwongozo wa busara mliowapatia. Asanteni sana.
Wahitimu 32 ambao wataapishwa hivi punde kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea wameamua kutoa miaka miwili ya maisha yao katika kuwahudumia watu wa Tanzania na kuimarisha urafiki baina ya nchi zetu mbili. Katika kipindi cha wiki tisa wamefanya jitihada kubwa kwa kujifunza lugha na masuala mengine ya kiufundi wanayohitajika kuyafahamu kabla ya kuhitimu na kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea nchini Tanzania.
Aidha, napenda kutoa shukrani za dhati kwa wakufunzi wa lugha na wale wa masuala ya kiufundi, wafanyakazi wa Peace Corps na familia za Kitanzania wilayani Muheza ambazo vijana hawa waliishi nazo katika kipindi chao cha mafunzo, kwa uvumilivu na kujitoa kwao katika kutekeleza kazi ya kuwaandaa kwa ajili ya kazi yao mpya. Hali kadhalika, napenda kutoa shukrani kwa wazazi, familia, marafiki, walimu na hata washauri wa vijana hawa kwa kuwapa moyo, hamasa na kiu ya kutoa huduma katika nchi nyingine.
Ndugu Wafanyakazi wa Kujitolea watarajiwa, wakati mkiwa hapa, mtachangia na marafiki wenu wapya katika jamii mtakazoishi nazo amali kubwa na tamaduni mbalimbali za Kimarekani. Ninyi, kama ilivyo kwa raia wengine wa Marekani wanaosafiri nje ya nchi, mnawawakilisha watu wa Marekani kwa wale wote mnaokutana nao. Watu hao watawafikia ninyi na maneno na matendo yenu pale watakapokuwa wanawawazia watu wa Marekani. Kwa watu wengi NINYI ndio mtakaokuwa sura ya Marekani. Ukweli huu unawapa wajibu, fursa lakini pia heshima.
Ninaweza kuwaeleza kutokana na uzoefu wangu kuwa jamii ambazo ninyi na wafanyakazi wengine wa kujitolea mtazihudumia zitakuwa na nafasi ya kipekee mioyoni mwenu. Mtarejea nyumbani Marekani mkiwa na uhusiano wa kudumu na jamii hizo. Mtabeba sehemu ya Tanzania mioyoni mwenu huku mkiwa wawakilishi wa Tanzania kwa Wamarekani wengine. Binti yangu mwenye umri wa miaka 17 ambaye amekulia Afrika ameandika katika mojawapo ya insha zake kama sehemu ya maombi ya kujiunga na chuo kuwa “Nikiwa Mmarekani, ninaipenda nchi yangu. Lakini ninazipenda pia nchi za Kiafrika ambapo nimekulia. Sioni mgongano wowote katika jambo hili.” Kwa hakika hata mimi sioni kama kuna mgongano wowote hapo.
Nikirejea katika kumbukumbu zangu kama Mfanyakazi wa Kujitolea, naomba mniruhusu niwape ushauri. Kwanza mtakapofika katika jamii zenu mpya, mjitahidi kuelewa mambo na si kuhukumu. Angalieni, mjifunze na muishi. Wakati mwingine unaweza tu kuelewa baadhi ya mambo yanayofanyika katika jamii fulani baada ya kueleza mazingira na maisha ya jumla ya jamii husika.
Pili, wakati ambapo ninasita kutoa tamko la jumla jumla, ninaweza kusema kuwa sisi Wamarekani tunamuangalia zaidi mtu mmoja mmoja wakati Watanzania huweka kipaumbele zaidi kwa familia na jamii au jumuiya kwa ujumla. Sisemi kwamba utaratibu mmoja ni mzuri zaidi ya mwingine. Wala si muhimu au vyema kuwabadilisha watu ili wafuate utaratibu unaoamini wewe kuwa ndio sahihi. La muhimu ni kwamba ni vyema mkaelewa tofauti hizo na uelewa huo uwasaidie katika kufanya maamuzi kuhusu hali na masuala mbalimbali yatakayokuwa yanajitokeza.
Mwisho, ni muhimu muelewe kujifunza utamaduni na lugha nyingine linaweza kuwa jambo gumu sana. Hivyo ni lazima mjitihidi sana kutumia miezi michache ya mwanzo katika kujifunza na kuelewa vizuri lugha na kujenga urafiki na Watanzania. Msijikwamishe kwa kutumia muda wenu mwingi kusoma hadithi au kutafuta kujenga urafiki na wageni wengine. Mtakuwa na uzoefu mzuri sana pale mtakapoondoa kikwazo cha lugha na utamaduni na kuwa sehemu kamili ya jamii mtakayoishi nazo. Njia rahisi na ya haraka ni kuchangamana na watu. Ninawahakikishia kuwa, kwa kadri muda unavyokwenda jambo hili huwa rahisi zaidi na mafanikio yake ni makubwa sana.
Leo hii, mbali na ninyi, kuna jumla ya Wafanyakazi wa Kujitolea 8,000 walio katika nchi zipatazo 75. Kabla yenu, tayari zaidi ya Wafanyakazi wa Kujitolea 2000 wameshahudumu hapa Tanzania. Miongoni mwa wale waliowahi kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea nchini Tanzania ni kiongozi wangu, Johnnie Carson, ambaye ni Mwanadiplomasia wa Kimarekani wa ngazi ya juu kabisa kwa bara la Afrika. Toka mwaka 1961, zaidi ya wafanyakazi wa kujitolewa 189,000 wamehudumu katika nchi 138. Baadhi yao wapo hapa miongoni mwetu hivi leo. Ninaomba wasimame ili tuweze kuwatambua.
Wafanyakazi hawa wa kujitolea wanawapatia urithi mzuri wa huduma ambayo wao waliianza. Mtakapokula Kiapo cha Utumishi, tafadhali muwafikirie wao na kutafakari kuhusu urithi na hazina kubwa wanayowapatia. Japokuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo mtakumbana na mambo mengi yatakayowafurahisha na hata kuwachukiza na kuwakatisha tamaa kama mtu mmoja mmoja, Kiapo mtakachoapa leo ni kiapo cha umma. Kiapo hichi kitawaunganisha na jambo lililokubwa kuliko ninyi, lakini ambalo kufanikiwa kwake kutategemea kujitoa kwenu na bidii zenu binafsi katika kutekeleza kwa uaminifu majukumu yenu kama wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps.
Tafadhali wale Wafanyakazi wa Kujitolea Watarajiwa msimame.
Mmetoka mbali hadi kufika hatua hii. Kwa busara mmetumia kipindi chenu cha mafunzo kuweka nadhiri na ahadi ya kutoa huduma kwa miaka miwili nchini Tanzania na kutekeleza malengo matatu ya Peace Corps:
-
Kutoa msaada wa kitaalamu kwa watu wa Tanzania;
-
Kuchangia katika kuimarisha uelewa wa Watanzania kuhusu Wamarekani; na
-
Kuchangia katika kuimarisha uelewa wa Wamarekani kuhusu Watanzania.
Tafadhali nyanyueni mikono ya kuume na mfuatishe nitakachosema
Kiapo
Mimi, (taja jina lako), naahidi kutoa miaka yangu miwili katika kuwasaidia watu wa Tanzania, na kwa moyo wa amani, urafiki na ushirikiano wa kimataifa nitafanya kila niwezavyo kuiwakilisha nchi yangu huku nikiheshimu mila, utamaduni na maadili ya Tanzania, na kwamba ninachukua jukumu hili kwa ridhaa yangu mwenyewe, nikiwa na akili timamu kabisa bila kusudio la kwenda kinyume na kwamba nitatekeleza vyema na kwa uaminifu majukumu yangu kama Mfanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps.
Ninaamini mtakuwa na maisha na uzoefu mzuri nchini Tanzania. Nawatakia kila la Kheri.
Hongereni sana!




