Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Risala Ya Rais Barack Obama Katika Kuukaribisha Mwezi Wa Ramadhan
Skip Left Section Navigation

Risala

Close Window Barack Obama<br>Rais wa Marekani
Barack Obama
Rais wa Marekani

IKULU YA MAREKANI


21 Agosti, 2009

RISALA YA RAIS BARACK OBAMA
KATIKA KUUKARIBISHA MWEZI WA RAMADHAN

Kwa niaba ya watu wa Marekani – ikiwa ni pamoja na jumuiya za Waislamu katika majimbo yote hamsini ya Marekani – ninapenda kuwatakia kheri Waislamu wote wa Marekani na duniani kote. Ramadhan Kareem.

Ramadhan ndio mwezi ambao Waislamu wanaamini kuwa Korani ilifunuliwa kwa Mtume Muhammad, ikianzia na neno rahisi – iqra. Hivyo huu ni wakati ambao Waislamu hutafakari kwa kina kuhusu hekima, miongozo na mafundisho ya imani yao na wajibu ambao wanadamu wanao kwa wanadamu wenzao na kwa Mungu.

Kama ilivyo kwa watu wengi wa imani tofauti ambao wameshuhudia Ramadhani katika jamii na familia zetu, ninafahamu kuwa huu ni wakati wa furaha – wakati ambapo familia hukusanyika na kula pamoja. Lakini ninajua pia kuwa Ramadhan ni wakati wa ibada, tafakari na maombi ya kina – ni wakati ambao Waislamu hufunga wakati wa mchana na usiku wakisali tarawih, wakisoma na kusikiliza Korani yote katika kipindi chote cha mwezi huu mtukufu.

Ibada hizi zinatukumbusha misingi inayotuunganisha pamoja na nafasi muhimu ya Uislamu katika kujenga na kuimarisha haki, maendeleo, hali ya kuvumiliana na heshima kwa wanadamu wote.

Mathalani, dhana ya kufunga inapatikana katika imani nyingi – ikiwa ni pamoja na imani yangu ya Kikristo – ikitambuliwa kama njia ya kuwaweka karibu waja na Mola wao na kuwakumbuka wale miongoni mwetu wenye njaa. Aidha, msaada ambao Waislamu wanautoa kwa wengine katika kipindi hiki, unatukumbusha wajibu wetu katika kutoa fursa na kuwezesha ustawi wa watu wengine mahali pote. Kwani ni muhumu kwetu kukumbuka kuwa dunia tunayotaka kuijenga – na mabadiliko tunayotaka kuyafanya – ni lazima yaanzie ndani ya mioyo yetu na katika jamii zetu wenyewe.

Katika kipindi hiki cha majira ya joto, watu wengi hapa Marekani wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za kusaidia jamii zao – ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watoto, kuhudumia wagonjwa, na kuwasaidia wale wenye shida mbalimbali. Taasisi za kidini, ikiwa ni pamoja na taasisi za Kiislamu, zimekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma hizi za kijamii. Katika kipindi hiki ambapo tunakabiliwa na changamoto nyingi, ni lazima tuuendeleza moyo huu wa kujitolea na kuwahudumia wengine, si katika mwezi huu tu bali pia katika miezi na miaka ijayo.

Ni azma yetu kutekeleza kwa dhati wajibu wetu wa kujenga dunia yenye amani na usalama zaidi sio tu ndani bali hata nje ya mipaka ya Marekani. Ni kwa sababu hiyo ndiyo tunahitimisha vita nchini Irak kwa namna nzuri inayohakikisha uwajibikaji. Ni kwa sababu hiyo ndiyo tunayatenga makundi yenye msimamo mkali na ya kigaidi huku tukijenga uwezo wa watu katika maeneo kama Afghanistan na Pakistan. Hii ndiyo sababu tunaunga mkono kwa dhati haki ya Waisraeli na Wapalestina kuishi kwa amani na usalama. Na ni kwa sababu hiyo ndipo wakati wote tutasimama kidete kulinda na kutetea haki ya watu wote kutoa maoni yao, kuabudu na kutekeleza mafundisho ya dini yao, kuchangia kikamilifu katika jamii zao na kuwa na imani katika utawala wa sheria.

Jitihada zote hizi ni sehemu ya dhamira ya dhati ya Marekani ya kushirikiana na Waislamu na nchi za Kiislamu kwa misingi ya kuheshimiana na kujali maslahi ya pande zote. Katika kipindi hiki muhimu cha ibada na kujiimarisha kiimani, ninapenda kusisitizia dhamira yangu ya dhati ya kuwa na mwanzo mpya kati ya Marekani na Waislamu duniani kote.

Kama nilivyosema katika hotuba yangu ya Cairo, ni lazima mwanzo mpya utokane na jitihada za kudumu za kila upande kusikiliza na kujifunza kutoka kwa upande mwingine. Aidha, ni lazima mwanzo huu ujengwe katika misingi ya kuheshimiana na kutafuta mambo yanayotuunganisha. Ninaamini kuwa kusikiliza ni sehemu muhimu ya jitihada hizi. Katika miezi miwili iliyopita Balozi za Marekani duniani kote zimekuwa zikikutana sio to na serikali bali pia moja kwa moja na wananchi katika nchi za Kiislamu ili kupata maoni yao. Na kutoka duniani kote, tumepata maoni mengi kuhusu namna ambavyo Marekani inaweza kushirikiana na nchi hizo kwa kuzingatia matarajio ya watu.

Tumesikiliza. Na kama ilivyo kwenu, tunaelekeza jitihada zetu katika kuanza kuchukua hatua mahsusi - kuhusu masuala ya kisiasa na kiusalama niliyoyaelezea hapo awali, na katika maeneo ambayo mmetuambia yataleta mabadiliko yenye manufaa zaidi katika maisha ya watu. Tunaamini kuwa baada ya muda jitihada hizi zitaanza kuleta mabadiliko.

Mashauriano haya yanatusaidia kutekeleza ubia ambao niliupendekeza mjini Cairo – ili kupanua program za mabadilishano ya kielimu; kuimarisha ujasiriamali na kukuza ajira; na kuongeza ushirikiano katika nyanja ya sayansi na teknolojia huku tukisaidia mafunzo ya ufundi. Tunaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) na nchi wanachama wa OIC ili kutokomeza polio. Aidha, tunashirikiana kwa karibu na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na changamoto za pamoja kuhusu masuala ya afya kama vile Mafua ya Nguruwe – ambayo najua ni kitisho kwa Waislamu wengi wanaojiandaa kwenda kushiriki ibada ya hija.

Jitihada zote hizi zinalenga katika kutimiza matarajio yetu ya pamoja ambayo ni pamoja na kuishi kwa amani na usalama; kupata elimu na kazi zenye heshima, kupenda familia, jamii na imani zetu. Haya yote yatahitaji muda, jitihada na subira kubwa. Hatuwezi kubadilisha mambo kwa siku moja, lakini tunaweza kuazimia kwa dhati kufanya yale yanayotupasa kufanya, wakati tukijielekeza katika mwelekeo mpya – tukielea kule ambako tungependa kuelekea sisi na watoto wetu. Hii ni safari ambayo ni lazima tusafiri pamoja.

Ninatarajia kuendelea na mjadala huu muhimu na kuubadilisha kuwa hatua mahsusi za utekelezaji. Na leo ninapenda kuwatakia Waislamu wote wa Marekani na duniani kote mwezi wenye Baraka mnapoupokea mwezi mtukufu wa Ramadhan. Amani ya Mwenyezi Mungu iwe nanyi.

 
Article translated in: