Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba ya Zahra Mkomwa kwenye Uzinduzi wa Jengo Kuu la Hospitali ya Wilaya ya Mafia Lililokarabatiwa Upya
Skip Left Section Navigation

Hotuba

Uzinduzi wa Jengo Kuu la Hospitali ya Wilaya ya Mafia Lililokarabatiwa Upya

24 Agosti, 2009

Hotuba ya Zahra Mkomwa, Kituo cha Udhibiti wa Maradhi (CDC)

Mheshimiwa Bi. Hajjat Amina Mrisho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,

Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Ndugu Manzie Mangochie,

Ndugu wajumbe wa timu ya ICAP

Mafia Oyee!

Mabibi na mabwana, habari za asubuhi!

Ni heshima kubwa kwangu kuungana nanyi asubuhi ya leo katika uzinduzi wa jengo kuu la Hospitali ya Wilaya ya Mafia lililokarabatiwa upya, ambalo litajumuisha Kituo cha Huduma na Matibabu ya VVU na UKIMWI kwa wakazi wa wilaya ya Mafia.

Katika miaka miwili iliyopita, ushirikiano kati ya watu wa Marekani na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na janga la UKIMWI, umewezesha kufunguliwa kwa zaidi ya vituo 80 vya kutoa huduma za matibabu na upimaji. Kama sehemu ya azma yetu ya dhati ya kujenga uwezo wa mfumo wa utoaji huduma za afya nchini Tanzania, tumefurahi kuchangia katika kuifanya hospitali hii muhimu kuwa ya kisasa zaidi. Kazi ya ukarabati wa hospitali hii ilifadhiliwa na watu wa Marekani kwa kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR). PEPFAR ni mfuko mkubwa kabisa wa kimataifa kuwahi kutengwa na nchi yoyote ile duniani katika kukabaliana na maradhi ya aina moja.

Akithibitisha azma ya dhati ya Watu wa Marekani katika kusaidia kuimarisha afya duniani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Rodham Clinton, katika ziara yake katika mataifa saba ya Afrika aliyoifanya hivi karibuni, aliambatana na Mratibu wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI Duniani Bw. Eric Goosby. Katika ziara hiyo, Bibi Clinton alitembelea vituo mbalimbali vinavyotoa huduma kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI na kukutana na baadhi yao ili kujionea mwenyewe mabadiliko makubwa katika maisha ya watu yanayoweza kuletwa kutokana na ushirikino wetu. Hii inathibitisha umuhimu wa PEPFAR kama nyenzo muhimu katika jitihada za kudhibiti maambukizi ya VVU na kutoa huduma za matibabu kwa Watanzania wanaoishi na VVU/UKIMWI.

Ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Mafia utaziwezesha familia na watu mmoja mmoja hapa Mafia kupata huduma bora za afya kwa urahisi zaidi. Aidha, utawawezesha wahudumu wa afya kutoa huduma yao katika mazingira safi, salama na ya kuvutia. Mbali na kutoa dawa za kupunguza makali ya VVU (Anti-Retroviral Treatment services), hospitali hii itatoa pia huduma nyingine mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU, huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, upimaji wa VVU kwa watoto na huduma nyingine za maabara.

Tunatoa wito kwenu nyote, kuitumia fursa hii, ambayo inapatikana bila malipo yoyote, kujua hali zenu za maambukizi ya VVU na kuwahamasisha marafiki na watu wa familia zetu kujitokeza ili nao waweze kupima afya zao. Mheshimiwa Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wametuonyesha njia. Hapo Julai 2007 kwa fahari kubwa walijitokeza hadharani na kupima VVU/UKIMWI. Toka wakati huo, zaidi ya Watanzania milioni 4 waliiga mfano wao na kujitokeza kupima.

Ni baada tu ya kupima na kujua hali yako ndipo unapoweza kupanga vyema maisha yako ya baadaye. Iwapo utagundulika kuwa na VVU, basi jiandikishe katika Kituo cha huduma za upimaji, ushauri nasaha na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia. Iwapo bado hujaambukizwa unaweza kujifunza kuhusu njia za kuepuka maambukizi na hata kuwasaidia wengine kujilinda dhidi ya maambukizi hayo.

Unaweza kabisa kuamua, mustakabali na hatima ya maisha yako ya siku zijazo… na tambua kuwa katika kufanya hivyo tutakuwa pamoja nawe bega kwa bega.

Kwa niaba ya watu wa Marekani, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa jitihada zenu za kuboresha afya katika nchi hii. Tutaendelea, bila kuchoka, kufanya kazi pamoja nanyi na pamoja na taifa lote la Tanzania ili kufikia maono ya Rais Kikwete ya kuwa na “Tanzania bila UKIMWI." Tunaamini inawezekana. Ahsanteni sana.

 
Article translated in: