Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba ya John Vertefeuille, Mkurugenzi Mkuu, Kituo cha Udhibiti wa Maradhi katika Uzinduzi wa Kituo cha Matibabu na Ushauri Nasaha na Upimaji VVU/UKIMWI
Skip Left Section Navigation

Hotuba

Uzinduzi wa Kituo cha Matibabu na Ushauri Nasaha na Upimaji VVU/UKIMWI
Katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru

Alhamisi 27, Agosti, 2009

Hotuba ya John Vertefeuille, Mkurugenzi Mkuu, Kituo cha Udhibiti wa Maradhi

Mgeni Rasmi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mheshimiwa Professor David Mwakyusa
Viongozi wa Serikali wa Mkoa na Wilaya
Wajumbe wa timu ya EGPAF
Watu Wanaoishi na VVU waliopo hapa hivi leo
Wageni waalikwa
Arusha Oyee!
Mabibi na mabwana, habari za asubuhi!

Ni heshima kubwa kwangu kuungana nanyi asubuhi ya leo katika uzinduzi wa kituo kipya cha Matibabu, Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU/UKIMWI kitakachowahudumia wakazi wa Arusha na Mkoa jirani wa Manyara.

Katika miaka miwili iliyopita, ushirikiano kati ya watu wa Marekani na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na janga la UKIMWI, umewezesha kufunguliwa kwa zaidi ya vituo 80 vya kutoa huduma za matibabu na upimaji. Ni azma yetu ya dhati ya kujenga uwezo wa mfumo wa utoaji huduma za afya nchini Tanzania na nimefurahi kuchangia katika maendeleo mazuri yaliyofikiwa mahali hapa. Ukweli ni kwamba mbali na kusherehekea uzinduzi wa kituo hiki kipya katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Mkoa wa Arusha unaweza pia kusherehekea kukaribia kukamilika kwa vituo vingine viwili vya afya- Kituo cha Afya cha Longido na Zahanati ya Namanga. Ujenzi na ukarabati wa vituo hivi umefadhiliwa na watu wa Marekani kwa kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR). PEPFAR ni mfuko mkubwa kabisa wa kimataifa kuwahi kutengwa na nchi yoyote ile duniani katika kubaliana na maradhi ya aina moja.

Akithibitisha azma ya dhati ya Watu wa Marekani katika kusaidia kuimarisha afya duniani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Rodham Clinton, katika ziara yake katika mataifa saba ya Afrika aliyoifanya hivi karibuni, aliambatana na Mratibu wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI Duniani Bw. Eric Goosby. Katika ziara hiyo, Bibi. Clinton alitembelea vituo mbalimbali vinavyotoa huduma kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI na kukutana na baadhi yao ili kujionea mwenyewe mabadiliko makubwa katika maisha ya watu yanayoweza kuletwa kutokana na ushirikino wetu. Hii inathibitisha umuhimu wa PEPFAR kama nyenzo muhimu katika jitihada za kudhibiti maambukizi ya VVU na kutoa huduma za matibabu kwa Watanzania wanaoishi na VVU/UKIMWI.

Hata hivyo mafanikio hayawezi kupimwa tu na kiasi cha fedha zinazotumika. Mafanikio haya yanapimwa vyema zaidi na mamilioni ya Watanzania ambao wamepatiwa huduma za upimaji wa hiari na ushauri nasaha, mamilioni ambao wamepatiwa huduma za matibabu na mamilioni ambao wameelewa na wamefanyia kazi ujumbe wa kujikinga dhidi ya maambukizo ya UKIMWI.

Kituo cha Matibabu, Upimaji na Ushauri Nasaha kuhusu VVU/UKIMWI katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru imewezesha familia na mtu mmoja mmoja kupata huduma bora za afya kwa urahisi zaidi. Aidha, watumishi wa kituo wanatoa huduma katika mazingira safi, salama nay a kuvutia. Mbali na kutoa dawa za kupunguza makali ya VVU, kituo hiki hutoa pia huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU, upimaji wa VVU kwa watoto wadogo na huduma za maabara.

Tunatoa wito kwenu nyote, kuitumia fursa hii, ambayo inapatikana bila malipo yoyote, kujua hali zenu za maambukizi ya VVU na kuwahamasisha marafiki na watu wa familia zetu kujitokeza ili nao waweze kupima afya zao. Mheshimiwa Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wametuonyesha njia. Hapo Julai 2007 kwa fahari kubwa walijitokeza hadharani na kupima VVU/UKIMWI. Toka wakati huo, zaidi ya Watanzania milioni 4 waliiga mfano wao na kujitokeza kupima. Kaimu Balozi wa Marekani nchini Bw. Larry Andre' aliungana na Rais Kikwete katika kuzindua kampeni mpya ya upimaji inayolenga kuwawezesha watu wengine zaidi ya milioni moja kujua hali ya afya zao.

Ni baada tu ya kupima na kujua hali yako ndipo unapoweza kupanga vyema maisha yako ya baadaye. Iwapo utagundulika kuwa na VVU, basi jiandikishe katika Kituo cha huduma za upimaji, ushauri nasaha na matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru. Iwapo bado hujaambukizwa unaweza kujifunza kuhusu njia za kuepuka maambukizi na hata kuwasaidia wengine kujilinda dhidi ya maambukizi hayo.

Unaweza kabisa kuamua, mustakabali na hatima ya maisha yako ya siku zijazo… na tambua kuwa katika kufanya hivyo tutakuwa pamoja nawe bega kwa bega.

Kwa niaba ya watu wa Marekani, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa jitihada zenu za kuboresha afya katika nchi hii. Tutaendelea, bila kuchoka, kufanya kazi pamoja nanyi na pamoja na taifa lote la Tanzania ili kufikia maono ya Rais Kikwete ya kuwa na “Tanzania bila UKIMWI." Tunaamini inawezekana. Ahsanteni sana.

 
Article translated in: