Hotuba
Programu ya Mabadilishano kati ya Marekani na Tanzania
Ziara ya Makocha wa Mpira wa Kikapu wa Tanzania kwenda Marekani
Ilipofanyika: Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski
28 Septemba 2009
Hotuba ya Afisa wa Ubalozi Anayeshughulikia Masuala ya Utamaduni - Karen Grissette
Mheshimiwa Kanali Kipingu na wawakilishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo,
Ndugu . Cheyo na Maafisa wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF),
Makocha wa mpira wa Kikapu,
Ndugu Wanahabari,
Mabibi na mabwana,
Habari za asubuhi.
Ninafuraha kubwa kuwakaribisha nyote hapa siku ya leo. Kama ambavyo mnaweza kuwa mnafahamu, Ubalozi wa Marekani umekuwa ukiendesha programu mbalimbali za mabadilishano katika masuala ya utamaduni ambapo mamia ya Watanzania wamekuwa wakienda Marekani kila mwaka. Mwaka huu tumewapaleka Marekani wasanii wanawake, walimu wa Kiswahili, wakulima wa chaza/lulu, maimamu, wakutubi na watu wa kada nyingine nyingi. Watanzania hawa hupata fursa ya kujifunza moja kwa moja mambo mbalimbali kuhusu Marekani. Aidha, hujenga maoni na mtazamo wao wenyewe kuhusu watu wetu, taasisi zetu na serikali yetu. Wengi hurejea wakiwa wameridhika na kile walichojifunza na wakiwa na shauku kubwa ya kuchagia uzoefu na ujuzi walioupata na wengine. Hata hivyo, kwa wale wanaofuatilia masuala ya michezo, ziara ya mabadilishano nitakayoitangaza hivi punde, itakuwa mojawapo ya ziara za kipekee na kusisimua zaidi kwa mwaka huu.
Makocha na wachezaji wa mpira wa kikapu waliopo mbele yetu, wanatarajiwa kuondoka usiku wa leo kwenda Marekani watakapohudhuria warsha ya mafunzo ya ukocha (coaching clinic). Katika wiki mbili zijazo, makocha hawa watatembelea majimbo kadhaa, wakianzia na Washington DC. Watatembelea vyuo vikuu mashuhuri vya Marekani. Wataona programu za michezo kwa watu wenye ulemavu. Watajifunza jinsi ya kuandaa na kuendeleza program za michezo kwa bajeti ndogo. Makocha hawa watacheza mpira wa kikapu dhidi ya timu za watu wazima na kuwatembelea Wamarekani majumbani mwao. Watatembelea viwanja na kumbi za michezo na kujifunza kuhusu namna ya kuanzisha na kuendesha programu za michezo kwa vijana wadogo wa Kitanzania. Ziara hii si ya mapumziko au kutalii. Kwa hakika makocha hawa watafanya kazi, watajifunza na kurejea na ujuzi kwa ajili ya Tanzania.
Mtakumbuka pia kuwa nusu ya kwanza ya program hii ya mabalishano ilifanyika mwaka jana. Sote tulimkaribisha mchezaji mahiri katika ligi ya NBA Matt Bonner na Mchezaji wa kike na mshindi wa medali ya Olimpiki, Jennifer Azzi nchini Tanzania ambapo waliendesha warsha za mafunzo ya ukocha wa mpira wa kikapu. Wamarekani hao walijifunza kuhusu michezo nchini Tanzania na walionyesha hamu kubwa ya kuendeleza mahusiano na nchi hii. Sasa serikali ya Marekani inawapeleka makocha 20 wa Kitanzania nchini Marekani kujionea wenyewe, jinsi tunavyoendesha program za michezo nchini humo.
Baada ya kutembelea Washington DC, makocha hawa watapata fursa ya kutembelea jiji la San Antonio, Texas, nyumbani kwa timu ya San Antonio Spurs anayoichezea Matt Bonner. Kwa mara nyingine, Matt Bonner ataendesha warsha ya mafunzo ya ukocha lakini safari hii akiwa katika uwanja wake wa nyumbani. Baada ya warsha, makocha watapata fursa ya kumuona Matt na timu nzima ya San Antonio Spurs wakicheza na timu pinzani katika uwanja wao wa nyumbani katika mojawapo ya michezo ya awali kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi.
Watu wamekuwa wakiuliza, makocha hawa wamepatikanaje? Ninapenda kuwathibitishia kuwa Ubalozi ulifanya kazi kwa karibu sana na Wizara, Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF), na vyama vya mpira wa kikapu katika mikoa tisa ya Tanzania bara na Zanzibar. Wafanyakazi wenzangu na mimi binafsi tulitembelea mikoa hiyo yote, na nikiwa pamoja na viongozi wa vyama hivyo vya mikoa, niliweza kuzungumza na zaidi ya makocha 100. Kutokana na zoezi hilo tulichagua makocha kumi na tisa (19) na afisa mmoja kutoka wizarani. Tulichagua timu inayojumuisha watu wa aina na kada tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na walimu, watumishi wa umma na wafanya biashara. Timu hiyo ina wanawake saba na wanaume kumi na tatu. Naibu Waziri Bendera ndiye aliyeidhinisha uteuzi wa mwisho. Tunajivunia sana ari na hamasa kubwa ya kuundeleza mchezo huu iliyoonyeshwa na mabalozi wetu hawa wa michezo wakati wa usaili, na tunajua kuwa wana shauku kubwa ya kuitumia kikamilifu fursa hii ili kurejea na utaalamu watakaochangia na makocha wenzao waliobaki nchini.
Ni kweli kwamba kuna makocha wengine wengi wenye sifa ambao hatukuweza kuwachagua. Kutokana na hali hiyo makocha hawa wameahidi kuwa mara watakaporejea nchini na wao wataendesha warsha za mafunzo katika mikoa yao ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Morogoro, Tanga, Unguja, Pemba, Arusha, na Kilimanjaro. Warsha hizo ni sharti mojawapo la wao kushiriki katika ziara hii.
Watu wa Marekani ndio wanaogharimia ziara hii wakilipia gharama zote za ushiriki wa washiriki, ambazo ni zaidi ya dola za Kimarekani laki moja. Tunaamini kuwa kupanua mawazo ya viongozi wa michezo wa Tanzania ni uwekezaji mzuri wa fedha za walipa kodi wetu kwa maendeleo ya michezo katika nchi hii.
Mwisho, Ninapenda kutangaza mojawapo kati ya mambo yatakayosisimua sana katika program hii. Hapo tarehe 6 Oktoba, kikundi hiki cha makocha kitashuhudia mechi maalumu ya awali kabla ya kuanza msimu wa ligi, ambapo timu ya Washington D.C. Wizards itakuwa ikicheza na timu anayochezea Hasheem Thabeet ya Memphis Grizzlies! Tumefurahi sana kuona kwamba kutakuwa na Watanzania wengi watakaomshuhudia Mtanzania mwenzao Hasheem Thabeet katika mchezo wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa!
Ni matumaini yangu kuwa ziara hii ya mafunzo kwa makocha wa mpira wa kikapu itaimarisha mahusiano kati ya watu wa Tanzania na watu wa Marekani. Ubalozi wa Marekani umedhamiria kwa dhati kuhamasisha maendeleo ya michezo kwa vijana nchini Tanzania kwa kupitia mafunzo kwa makocha na wachezaji. Tunatazamia ziara hii ya makocha itahamasisha zaidi vijana wa Kitanzania kuishi maisha yenye afya na uchangamfu kwa kushiriki katika michezo na hivyo kuwa raia wenye afya njema, wakakamavu na walioelimika vyema!
Tuna fahari kubwa kusaidia maendeleo ya michezo kwa vijana nchini Tanzania. Tunapenda kuishukuru Wizara na TBF kwa fursa hii ya kufanya kazi pamoja. Tunaamini ushirikiano huu utaendelea na kuimarika zaidi katika siku zijazo. Asanteni sana.




