Skip Global Navigation to Main Content
Skip Breadcrumb Navigation
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Jenerali Ward Atembelea Tanzania

Januari 6, 2011
Jenerali William 'Kip' Ward (Picha: Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam)

Jenerali William "Kip" Ward (Picha: Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam)

Kamanda Mkuu wa Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani (USAFRICOM) Jenerali William "Kip" Ward, katika mazungumzo yake na viongozi wa Tanzania hapo tarehe 6 Januari, amepongeza ubia imara kati ya Marekani na Tanzania. Katika mazungumzo yake na Rais Kikwete, Jenerali Ward alisisitiza ahadi ya Marekani ya kuisaidia Tanzania katika kupambana na uharamia, kuenea kwa VVU/UKIMWI na kuimarisha utulivu na usalama wa kikanda.

Katika mkutano wake na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jenerali A. A. Shimbo, Jenerali Ward alipongeza weledi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kulisifu Jeshi hilo kwa kusaidia jitihada za kulinda amani katika maeneo mbalimbali na kuwa tayari kushirikiana na Marekani katika masuala ya usalama. Jenerali Ward alisema kuwa matarajio yake ni kuona kuwa ushirikiano kati ya JWTZ na AFRICOM unaimarika zaidi.

Marekani inaisaidia Tanzania katika kuiwezesha kutumia uwezo na ushawishi wake katika kutatua migogoro barani Afrika na kwingineko duniani. Msaada wa Marekani katika kujenga uwezo wa Tanzania wa kulinda amani unajumuisha elimu na mafunzo ya kijeshi. Aidha, Marekani inatambua na kuheshimu nafasi muhimu ya Tanzania katika Umoja wa Afrika na katika jumuiya za ushirikiano Mashariki na Kusini mwa Afrika. Marekani inaisaidia Tanzania katika kuimarisha mipaka yake na kukabiliana na uharamia, usafirishaji haramu wa silaha na madawa ya kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu na changamoto nyingine za kimataifa.

Ziara ya Jenerali Ward nchini Tanzania iliyofanyika tarehe 5 na 6 Januari ni sehemu ya ziara yake katika nchi za Afrika ya Mashariki.