Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Balozi wa Marekani aungana na Wamarekani wengine kujitolea kujenga nyumba Korogwe
Januari 11, 2007
Siku ya Jumatano Januari 10 mwaka huu, Balozi wa Marekani nchini Michael L. Retzer aliungana na Mbunge wa Marekani Steven Weickert kutoka Appleton, Wisconsin, pamoja na Wamarekani wengine 14 wa kutoka jimbo la Wisconsin, ambao hivi sasa wanatembelea Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga kusaidia kujenga nyumba kwa watu wanaohitaji makazi. Mradi huu ni sehemu ya mpango wa taasisi ya Habitat for Humanity Tanzania unaolenga kujenga nyumba nzuri zenye gharama nafuu kwa wananchi wa Korogwe, ambao hawana nafasi ya kupata makazi ya kuridhisha.
Kikundi hicho kutoka Marekani kimekuja Tanzania kama sehemu ya mpango wa kimataifa wa Habitat for Humanity unaoitwa Global Village Programme. Washiriki kadhaa wa kikundi hicho wanajishughulisha na miradi ya taasisi ya Habitat for Humanity katika jamii wanazoishi huko Marekani. Wamarekani hao wanafanya kazi bega kwa bega na wananchi watakaofaidika na mradi huo, na wengi wao wamechanga fedha kusaidia miradi ya Habitat for Humanity hapa nchini Tanzania.
Kikundi hicho cha Wamarekani kimekuwa Korogwe kwa muda wa siku kumi na kimesaidia kujenga nyumba tatu. Nyumba zote zina msingi wa zege, zimejemgwa kutumia matofali ya kuchowa na kuezekwa kwa mabati. Kila nyumba ina vyumba vitatu na choo ya kisasa ya shimo.
Taasisi ya Habitat for Humanity Tanzania ilianza kufanya kazi wilayani Kasulu, mkoani Kigoma mwaka wa 1986, na sasa hivi imepanuka na kufikia vituo 18 ambavyo vimehudumia takriban sehemu 50 tofauti, kote nchini. Mpango wa taasisi hiyo umezisaidia jamii kujenga takriban nyumba 2,200 na kujenga makazi ya kudumu kwa Watanzania takriban 12,000. Mpango huo unatoa huduma ya kusimamia ujenzi ili kuhakikisha kuwa nyuma zinajengwa kwa kiwango cha juu, na pia unatoa mikopo kwa familia husika. Hii ina maana kwamba gharama ya ujenzi inakuwa nafuu hata kwa wale wenye kipato cha chini kabisa. Ulipaji wa mikopo hiyo ni wa mzunguko kupitia mfuko wa kijiji unaowapa fursa wananchi wengi zaidi kujijengea nyuma zao wenyewe.
Kila inapowezekana, usanifu wa nyumba zinazojengwa chini ya mradi huo unazingatia matumizi ya nyenzo zinazopatikana katika maeneo hayo. Misingi ya zege ni lazima, pamoja na sakafu za sementi na madirisha yenye wavu wa kuzuia mbu wasiingie. Kwa kawaida nyumba hizo zimepauliwa kwa mbao zilizopakwa mafuta machafu kuzuia wadudu, na kuezekwa kwa mabati. Wamiliki wote wa nyuma hizo wanafaidika pia na vyoo vya kisasa.




