Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Mwandishi wa habari Mtanzania afanya ziara ya mafunzo Marekani kuhusu magonjwa ya kuambukizwa
Januari 17, 2007
Mwandishi wa habari mwandamizi wa kampuni ya The Guardian Limited, anayeandika kuhusu masuala ya afya na maendeleo, Adolph Simon Kivamwo, ataondoka nchini hivi karibuni kushiriki kwenye ziara ya wiki tatu nchini Marekani kuhusu magonjwa ya kuambukiza na UKIMWI. Ziara hii ni sehemu ya mpango maarufu inayopeleka viongozi wageni kuitembelea Marekani - International Visitor Leadership Programme – ulio chini ya Wizara ya Mambo ya Nje. Ziara hiyo itawapa washiriki fursa makini ya kujifunza na pia kujenga uhusiano binafsi na rasmi kati ya wananchi wa Marekani na Tanzania.
Mpango huo unalenga kuchunguza athari za magojwa ya kuambukiza na UKIMWI kwa maendeleo ya jamii; kukua kwa uchumi; sera ya afya ya umma; mshikamano ndani ya jamii na utengamano wa kitaifa na kikanda. Washiriki watapata fursa ya kufanya tathmini ya sera za janga la UKIMWI za Marekani na kujifunza kuhusu juhudi za Marekani kusaidia nchi zingine kupambana na magonjwa ya kuambukiza kama kifua kikuu, hepatitis, na homa ya ndege.
Akiwa nchini Marekani, Kivamwo na washiriki wengine 22 kutoka nchi mbalimbali kote ulimwenguni watatembelea majimbo ya Washington, D.C., California, Colorado, Georgia na Florida. Mikutano itakayofanyika jijini Washington itahusisha maafisa mbalimbali wa serikali, ikiwemo wale wa Wizara ya Mambo ya Nje ili kupata picha nzuri ya shughuli za mpango wa Rais wa kupunguza makali ya UKIMWI - President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR).
Huko California, washiriki wamepangiwa kutembelea kituo cha kutafiti magonjwa ya kuambukiza, na UKIMWI cha Chuo Kikuu cha San Diego - University of San Diego’s Division of Infectious Diseases HIV/AIDS Research and Adult HIV/AIDS Clinical Trial Unit. Huko Colorado wanatarajiwa kukutana na maafisa kutoka ofisi ya Meya inayogawa fedha kwa vikundi vinavyoshughulikia masuala ya UKIMWI. Katika majimbo ya Georgia na Florida watatembelea kituo cha kutibu magonjwa ya kuambukiza na ofisi za Chama cha Msalaba Mwekundi cha Marekani.
“Ninaamini ziara hii itanipa mwanga zaidi na ufahamu wa kina kuhusus masuala ya afya,” alisema Kivamwo, na kuongeza: “Nitakaporudi nyumbani, ninaahidi kwamba kupitia makala nitakazoandika na majadiliano mbalimbali nitakayoshiriki, nitawashirikisha Watanzania ujuzi ambao nitaupata katika ziara hii.”




