Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Mzee Kawawa atunukiwa tuzo ya kumuenzi Dk. Martin Luther King

Januari 23, 2007

Jumanne Januari 23, 2007 mwanasiasa mkongwe Mzee Rashid Mfaume Kawawa, alitunukiwa tuzo ya kumuenzi Dk. Martin Luther King inayojulikana kama Martin Luther King Jr. Drum Major for Justice Award, kwa mchango wake mkubwa kwa taifa la Tanzania, kabla na baada ya uhuru wa nchi hii.

Mzee Kawawa alitunukiwa tuzo hiyo na Balozi wa Marekani nchini Michael L. Retzer, baada ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii), Mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru kumtambulisha mtunukiwa wa tuzo ya Drum Major for Justice kwa mwaka wa 2007.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani kwa vyombo vya habari, mchango mkubwa wa Mzee Kawawa ulikuwa wakati wa harakati za kupigania uhuru, kwa sababu yeye ndiye alikuwa mtu muhimu aliyemsaidia Mwalimu Nyerere wakati wa harakati hizo za ukombozi.

Mafanikio mengine makubwa yalikuwa ni mchango wake wa kutambua na kusaidia vikundi vidogo vidogo vya wanawake na vijana. Pia alichangia kifedha kusaidia shughuli za chama cha TANU, ambacho ndicho kiliongoza harakati za kupigania uhuru uliopatikana 1961.

Tuzo ya Drum Major for Justice Award ilianzishwa ili kumuenzi Dk. Martin Luther King, Jr. Dk. King alikuwa mtu mashuhuri katika nyakati za historia ya hivi karibuni. Hotuba na mihadhara yake ilichochea dhamira ya kizazi kizima. Harakati na maandamano aliyoyaongoza yalileta mabadiliko muhimu katika mfumo wa maisha nchini Marekani, kupitia ujasiri na msimamo wake thabiti wa kujitoa. Msimamo huu ndio uliongoza harakati za kupigania haki za raia kwa miaka kumi na mitatu. Uongozi wake wenye haiba ya kuvutia uliwatia moyo wanaume na wanawake, vijana na wazee, nchini Marekani na ulimwenguni kote.

Mzee Kawawa anakuwa mtunukiwa wa nane wa tuzo ya kumuenzi Dk. Martin Luther King ya Drum Major for Justice tangu alipotunukiwa Jaji Joseph Sinde Warioba kwa mara ya kwanza mwaka 1999. Mwalimu Julius K. Nyerere alikuwa mtunukiwa wa pili mwaka uliofuata, baada ya kifo chake, na mwaka 2001 tuzo hiyo haikutolewa.

Mheshimiwa Francis Nyalali alitunukiwa tuzo hiyo mwaka 2002, akifuatiwa na Profesa Geoffrey Mmari na Mama Justa Mwaituka, 2003 na 2004. Balozi Gertrude Mongella alitunukiwa tuzo hiyo mwaka 2005, na mwaka jana alitunukiwa Dk. Salim Ahmed Salim.

Mzee Kawawa anaamini juu ya umuhimu wa uhuru wa kuabudu, nguvu ya kujitegemea, pamoja na uwezo wa watu binafsi kutekeleza malengo yao ya kujiletea maendeleo. Hata baada ya kustaafu, Mzee Kawawa bado anaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya Tanzania, huku akitoa ushauri muhimu inapolazimu.