Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Makamu Rais wa shirika la misaada la Millenium Challenge Corporation aja Tanzania

January 26, 2006

John Hewko, Makamu Rais wa shirika la misaada la Millenium Challenge Corporation (MCC) atafanya ziara hapa nchini Januari 31-Februari 4 kujadili uwezekano wa Tanzania kupatiwa misaada kutoka mfuko wa Millenium Challenge Account (MCA). Hewko ataambatana na Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia masuala ya Afrika katika shirika la MCC, Maureen Harrington; Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Tanzania kwenye shirika hilo Gretchen Brevnov, pamoja na naibu wake Lucas Black.

Ujumbe huo unaoongozwa na Bwana Hewko utatoa maelezo ya kina kuhusu mchakato wa kuchaguliwa kupata msaada wa Millenium Challenge Account kwa maafisa waandamizi wa Serikali, maafisa wa jumuia za raia (civil society); maafisa kutoka sekta binafsi, wahisani wengine pamoja na vyombo vya habari. Pamoja na kufanya mikutano jijini Dar-es-Salaam, ukiwemo mkutano na Rais Jakaya Kikwete, ujumbe huo wa shirika la MCC pia utatembelea Zanzibar kukutana na Rais Amani Abeid Karume na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi. Ujumbe huo utajionea kwa karibu changamoto ambazo zinawakabili wananchi wa bara na visiwani katika kujiletea maendeleo.

Tanzania ilichaguliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika la MCC mwezi Novemba 2005 kama moja ya nchi 23 zinazostahili kupewa misaada kutoka kwenye mfuko wa MCA. Uchaguzi huu unategemea juhudi za nchi husika kutekeleza mikakati ya kutawala kwa haki, kuwekeza katika wananchi wake, na kuimarisha uhuru wa kiuchumi.

Kabla ya kuchaguliwa kwenye kundi la nchi zinazostahili kupewa msaada huo, Tanzania ilikuwa imechaguliwa kushiriki katika mpango wa kuziwezesha nchi hizo kutimiza masharti ya viwango vinavyotakiwa. Mpango ulioandaliwa na Tanzania na ambao sasa hivi unatathminiwa kabla ya kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika la MCC, unalenga kupunguza vitendo vya rushwa kwa kuboresha uwezo wa sekta isiyo ya kiserikali kutoa usimamizi; kuimarisha utawala wa sheria; kuanzisha kitengo cha kutafiti masuala ya kifedha (Financial Intelligence Unit); na kuimarisha uwazi kwenye shughuli za ununuzi na ugavi katika sekta ya umma (public procurement).

Kama mpango huo ulioandaliwa na Tanzania utapitishwa na Bodi ya Wakurugenzi, na pia baada ya Baraza la Congress kutoa idhini yake, Tanzania itaendelea na hatua ya kuutekeleza mpango huo na kuandaa mapendekezo ya miradi itakayofadhiliwa chini ya mkataba na shirika la MCA.

###

Shirika la misaada la Millenium Challenge Account (MCA) ni shirika la Serikali ya Marekani ambalo lengo lake ni kufanya kazi pamoja na baadhi ya nchi maskini kabisa duninia. Shirika hilo linaamini kwamba misaada ina faida tu kama itatumika kuimarisha sera na mikakati bora ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika juhudi za kupunguza umaskini kwa kuchochea uchumi.

- Translation -
This content is also available in English