| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Mhariri wa ‘Mtanzania Jumapili’ Aende Marekani Kwenye Mafunzo ya Uandishi wa Magazeti
Januari 27, 2006
Mhariri wa gazeti la Mtanzania Jumapili, Badra Masoud, anaondoka Jumatatu Januari 30 kuelekea Marekani kuhudhuria mafunzo ya wiki tatu ya Uandishi wa Habari za Magazeti, yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, imesema kwamba Bi Masoud na waandishi wengine wa habari 18 kutoka nchi mbalimbali watatembelea Washington, D.C.; New York; na Columbia, Missouri. Baada ya hapo washiriki hao watagawanywa katika makundi ambayo yataelekea katika mojawapo kati ya miji ya Scottsdale, Arizona; Denver, Colorado; Seattle, Washington; Houston, Texas; au San Diego, California, kabla ya kuungana tena Tapa Bay, Florida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, malengo ya mafunzo hayo ni kuona viwango, uwajibikaji pamoja na taasisi za magazeti nchini Marekani, na kuelezea haki na wajibu wa waandishi wa habari katika demokrasia.
Kadhalika, mafunzo hayo yatatoa mwanya kwa washiriki kuwasiliana na waandishi wa habari wa Marekani na watu waliobobea katika fani ya habari kutoka asasi ndogo na kubwa za uchapishaji.
Kati ya mambo ambayo washiriki watajihusisha nayo wakati wa mafunzo yao, ni kutembelea asasi zinazojihusisha zaidi na uandishi wa habari unaofuata miiko kitaifa na kimataifa.
Kupitia mikutano mbalimbali na waajiriwa wa serikali na Bunge, watakuwa na uwezo wa kutathmini mahusiano yaliyopo baina ya serikali na waandishi wa habari, na umuhimu wa vyombo vya habari kusisitiza mawasiliano kati ya serikali na wananchi. Watakutana pia na waandishi pamoja na wahariri wa magazeti ya kitaifa kutathmini sera za ndani na nje zinazopewa kipaumbele na vyombo vya habari.
Akizungumzia safari yake hiyo, Bi Masoud amesema kwamba atakuwa na uwezo wa kuona na kujadili mada mbalimbali zinazohusu uandishi wa magazetini nchini Marekani, na kuzilinganisha na uwajibikaji uliopo hapa Tanzania. Amewema, anatarajia kuweka katika vitendo baadhi ya mambo atakayojifunza Marekani, pindi arudipo nchini.
Mafunzo haya ni sehemu ya mpango unaojulikana kama International Visitor Leadership Programme ambao unafadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa niaba ya wananchi wa Marekani, yakiwa na lengo la kuendeleza mahusiano binafsi na ya kitaaluma kati ya wananchi wa Marekani na wa Tanzania.



