Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Sauti ya Amerika kuzindua matangazo ya redio Somalia
Februari 5, 2007
Washington, D.C., - Kuanzia Februari 12, Sauti ya Amerika (VOA) itaanza kutangaza vipindi vya redio kila siku katika lugha ya Kisomali kwa nchi zilizo katika Pembe ya Afrika.
Kikundi cha watangazaji wa Kisomali walio kwenye makao makuu ya Sauti ya Amerika mjini Washington D.C. wataungana na waandishi wa habari wakujitegemea barani Afrika na ulimwenguni kote, ili kuwapa mamilioni ya watu wanaoongea lugha ya Kisomali habari na taarifa sahihi na za wakati.
“Tuna shauku kubwa ya kuungana na jamii ya wanahabari nchini Somalia,” alisema Mkurugenzi wa Sauti ya Amerika, Dan Austin. “Utoaji wa habari na taarifa sahihi, za wakati, na zisizopendelea upande wowote kwa wananchi wa Somalia ni muhimu sana hasa katika muda huu mugumu kwenye historia ya ukanda huo,” aliongeza.
Kipindi hicho kipya cha Sauti ya Amerika cha nusu saa kitakuwa hewani siku saba kwa wiki, na kitakuwa kikitangaza taarifa za habari za ulimwengu, pamoja na taarifa za habari za Somalia na ukanda mzima wa nchi za Pembe ya Afrika. Matangazo hayo yatahusisha pia vipindi vya muziki na majadiliano, ambavyo vitawapa viongozi na wasikilizaji wa kawaida fursa ya kueleza maoni yao juu ya mada mbalimbali.
Idhaa ya Kisomali ya Sauti ya Amerika inafadhiliwa kupitia ruzuku iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Idhaa hiyo mpya ni nyongeza kwa vipindi vinavyotangazwa sasa hivi na Sauti ya Amerika kwa nchi za Pembe ya Afrika katika lugha za Amharic, Afan Oromo na Tigrigna. Huko nyuma, Sauti ya Amerika ilikuwa ikitangaza katika lugha ya Kisomali kati ya 1992 na 1994.
Matangazo ya Sauti ya Amerika yatakuwa hewani kwenye masafa ya AM, FM na masafa mafupi (Shortwave) saa moja usiku saa za Somalia na kurudiwa saa mbili usiku. Kipindi cha saa mbili usiku pia kitarushwa hewani na kituo cha HornAfrik (88.8 FM), ambacho kinashirikiana na Sauti ya Amerika. Vipindi hivyo vinapatikana pia kwenye tovuti ya idhaa hiyo.
Masafa: Saa 1:00 - 1:30 usiku: 13580 Khz, 15620 Khz, 1431 Khz
Saa 2:00 - 2:30 usiku: 13580 Khz, 15620 Khz
Sauti ya Amerika, ambayo ilianza matangazo yake mwaka wa 1942, ni idhaa ya utangazaji ya kimataifa inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Bodi ya Magavana ya Utangazaji (Broadcasting Board of Governors). Sauti ya Amerika hutangaza zaidi ya masaa 1,000 za habari, taarifa, na vipindi vya elimu na utamaduni kila wiki kwa wasikilizaji na watazamaji zaidi ya milioni 115. Vipindi hutayarishwa katika lugha 44.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Masuala ya Umma ya Sauti ya Amerika – Simu: (202) 203-4959 au kwa barua pepe: publicaffairs@voa.gov.




