Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

USAID yasaidia juhudi za Tanzania kuzuia mafua ya ndege

Februari 9, 2006

Baada ya kuthibitishwa kwa taarifa za kugunduliwa kwa mafua ya ndege nchini Nigeria aina ya H5N1 jana, bara la Afrika liko tena katika hali ya tahadhari. Hata hivyo, Serikali ya Tanzania, kupitia msaada wa shirika la misaada la Marekani USAID, pamoja na GTZ la Ujerumani, imekuwa ikifanya maandalizi ya kukabiliana na janga hilo kama virusi hivyo vitawasili hapa nchini.

Ingawa bado hakuna dalili zozote zinazofahamika kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo katika wanyama au binadamu nchini Tanzania, kuna uwezekano kwamba virusi hivyo vinaweza kuingizwa nchini kupitia kuku au ndege ambao wanahama hama. Baada ya kuku kuambukizwa, virusi hivyo husambaa kwa haraka kutoka kundi hadi kundi. Aina kali za homa hiyo huweza kuangamiza kiasi kikubwa cha kuku na kuleta maafa makubwa ya kiuchumi.

Kuwaua kuku walioathirika, ambayo ndiyo njia thabiti ya kudhibiti ugonjwa huo, pia kunaweza kunaongeza mzigo wa kiuchumi. Watu wanaofanya kazi kwenye sehemu zilizo na kuku walioathirika, wanahesabika kuwa hatarini kuambukizwa na virusi hivyo: Kati ya watu 165 walioambukizwa na virusi vya mafua ya ndege, 88 wameshakufa.

Mafua ya ndege yanaweza kuletwa Tanzania na ndege pori wanaohama hama. Ndege kati ya milioni 3 hadi 5 tayari wamekwishapitia nchini wakiwa katika safari yao ya kila mwaka ya kuhamia kusini wakitokea nchi za Asia na Ulaya ya Kati, ambako inawezekana walikuwa pamoja na ndege walioathirika na virusi hivyo.

Kwa sababu mchakato huu wa kuhama hama unajirudia, ndege hao wanapofunga safari ya kurudi kaskazini wakati wa majira ya kuchipua (spring) wanaweza kuwaambukiza ndege wengine huko Ulaya. Na baadaye, ndege wanaporudi tena kusini wanaweza kuwaambukiza wenzao barani Afrika. Vijiji vingi nchini Tanzania vimo katika eneo la njia inayotumiwa na ndege hao wanapohama. Wanakijiji hawa hufuga kuku wanaotembea huru ambao wako hatarini kuambukizwa virusi na ndege wanaohama hama.

Ni muhimu kuanzisha mfumo wa kuchunguza na kupima ndege pori, kuku, na binadamu ili kuweza kuigundua homa hiyo mapema iwezekanavyo. Tayari Tanzania imeanzisha mfumo thabiti ambao utawawezesha maafisa wa afya na tiba ya mifugo kuchukua hatua zinazofaa kuzuia na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo. Kwa hivi sasa, shughuli za kuchunguza ndege pori zinafanywa na mradi wa Tanzania Bird Atlas Project, ambao unasimamiwa na taasisi ya kutafiti wanyama pori nchini, Tanzania Wildlife Research Institute, iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.

Taasisi ya kutafiti magonjwa ya wanyama, Animal Disease Research Institute, kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo inapanga kufanya uchunguzi wa kuku ili kubainisha kutokuwepo kwa virusi hivyo hapa nchini. Chuo Kikuu cha Minnesota nchini Marekani kimepata ufadhili wa kuanzisha shughuli za kuwapima na kuwachunguza binadamu kwa kushirikiana na taasisi ya kutafiti magonjwa ya taifa, National Medical Research Institute.

Shirika la USAID nchini Tanzania limekuwa likiisaidia Serikali ya Tanzania kujitayarisha kukabiliana na virusi vya mafua ya ndege. Kwa kushirikiana na shirika la misaada la GTZ, USAID inachangia kusaidia shughuli za kuchunguza ndege pori, kuku na binadamu. Shirika la USAID limetoa kiasi cha dola 75,000 kwa mradi wa kuchunguza ndege pori, na shirika la GTZ limeipa USAID dola 70,000 kwa shughuli za kufanya vipimo vya sampuli.

Shirika la USAID nchini Tanzania ni mwanachama hai wa kamati ya ufundi ya kudhibiti mafua ya ndege (Health Sector Avian Influenza Technical Committee), na linasaidia pia katika kuandaa mpango wa dharura wa kudhibiti mafua hayo (Health Sector Emergency Preparedness and Response Plan). USAID pia imepata mwaliko wa kushiriki katika kamati ya pamoja ya taifa ya kuidhibiti mafua hayo (National Joint Task Group on Avian Influenza). Shirika la USAID limeomba msaada zaidi kutoka Washington utakaosaidia katika shughuli za kuchunguza mafua ya ndege. Kiasi kikubwa cha msaada huu kitatumiwa kupanua uwezo wa maabara ili vipimo vya mafua ya ndege viweze kufanyika haraka hapa nchini, na kwa gharama nafuu, badala ya kupeleka vipimo hivyo ng’ambo. Juhudi hizo zitasaidia sana katika kuzuia au kupunguza tishio la kuibuka kwa mafua ya ndege, siyo tu hapa nchini, bali pia ulimwenguni kote.

Virusi vya mafua ya ndege vimesababisha idadi ya ndege na kuku milioni 150 kuchinjwa katika nchi za Asia, Ulaya, Mashariki ya Kati, na Afrika. Hatua hizi zimeathiri maisha ya wakulima katika nchi nyingi. Kufikia tarehe 6 Februari, virusi hivyo vilikuwa vimewaambukiza watu 165 huko Asia na Mashariki ya Kati na kusababisha vifo 88 katika nchi za Cambodia, China, Indonesia, Thailand, Vietnam, Uturuki na Iraq.

Ingawa kwa hivi sasa virusi hivyo havina uwezo wa kuambukizwa kutoka mtu hadi mtu, lakini vina uwezo wa kujibadilisha (mutation), na uwezo huo unaweza kupanuka wakati wowote. Hali hii ikitokea inaweza kuleta janga ambalo linaweza kusababisha vifo vya makumi ya mamilioni ya watu.

- Translation -
This content is also available in English