Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Mama Shadya mgeni rasmi katika sherehe ya kukabidhi mashine ya kuhesabu CD4 kwenye hospitali ya Chake Chake

Februari 14, 2007

Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Shadya Karume ameishukuru Serikali ya Marekani, kupitia Vituo vya Kudhibiti Magonjwa (Centers for Disease Control and Prevention - CDC) na Chuo Kikuu cha Columbia (Columbia University - CU) kwa juhudi zao kubwa za kuisaidia Wizara ya Afya na Huduma za Jamii Zanzibar kuweza kutoa huduma za matunzo na tiba kwa watu wanaoishi na UKIMWI visiwani humo.

Mama Shadya alikuwa akiongea February 14, 2007 katika sherehe ya kukabidhi mashine ya kuhesabu chembechembe za kinga ya mwili (CD4 count machine) kwenye hospitali ya Chake Chake. Mke wa Rais alikuwa amefuatana na Mkurugenzi Mkazi wa Vituo vya Kudhibiti Magonjwa (CDC), Dkt. Stefan Wiktor na Bi. Amy Cunningham wa Chuo Kikuu cha Columbia (CU) alipoitembelea hospitali hiyo kujionea mwenyewe mradi ulioanzishwa hivi karibuni wa kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (Prevention of Mother to Child Transmission - PMTCT), pamoja na mradi wa kutoa huduma ya matunzo na tiba (Care and Treatment - C&T).

Ili kuhakikisha kwamba huduma madhubuti za matunzo na tiba zinatolewa kwa watu wanaoishi na UKIMWI kisiwani Pemba, vituo vya CDC na Chuo Kikuu cha CU vilitoa msaada wa kununua na kufunga mashine ya CD4 yenye thamani ya dola 50,000 pamoja na vitendanishi (reagents). Chuo Kikuu cha CU kimetoa mafunzo kwa wahudumu wa maabara wawili juu ya jinsi ya kuitumia mashine hiyo mpya. Mashine hiyo itapunguza mzigo wa kusafirisha sampuli za damu kuzipeleka kwenye hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja, ambayo ndiyo hutumiwa na maabara ya hospitali ya Chake Chake kubainisha kwa haraka vipimo vya watu wanaoishi na UKIMWI.

“Tangu 2004, Serikali ya Marekani kupitia vituo vya CDC imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Zanzibar kusaidia juhudi za kitaifa za kupambana na janga la UKIMWI. Lengo la ushirikiano huo ni kupanga mpango endelevu wa taifa wa kupambana na UKIMWI, kuimarisha miundombinu kupitia ukarabati wa kliniki na vifaa kwenye vituo vya afya na maabara, na pia kutoa mafunzo kwa watoa huduma,” alisema Dkt. Wiktor.

Mipango ya kutoa huduma za matunzo na tiba (C&T) na kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) ilianzishwa mjini Chake Chake mwaka wa 2005. Hivi sasa wateja 128 walio na virusi vya UKIMWI wameandikishwa kupata huduma ya matunzo na tiba (C&T), na 57 kati yao wanapata tiba ya kupunguza makali ya UKIMWI. Aidha, akina mama wajawazito 2197 walipata huduma za kupima na ushauri nasaha kwenye kliniki ya akina mama wajawazito ya hospitali hiyo.

Dk. Wiktor alisema, “Serikali ya Marekani na washiriki wake, wakishirikiana kwa karibu na Serikali ya Zanzibar wanafanya juhudi za dhati kupanua utoaji wa huduma za kinga, matunzo na tiba, ili kupambana na kuenea kwa maambukizi ya UKIMWI, pamoja na kutoa tiba halisi visiwani humo. Serikali ya Marekani inajivunia kupata fursa ya kusimama pamoja bega kwa bega na Serikali ya Zanzibar wakati wote wa maandalizi na uanzishaji wa Mpango wa Taifa wa Tiba na Matunzo (National Care and Treatment Plan). Serikali ya Mrekani imedhamiria kwa dhati kuunga mkono Mpango wa Taifa wa Huduma ya Matunzo na Tiba Zanzibar, na itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali pamoja na wadau wake ili kufanikisha miradi ya kupambana na UKIMWI.”

Kabla ya ushirikiano huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikuwa na uwezo mdogo wa kutoa huduma za matunzo na tiba kwa watu wanaoishi na UKIMWI visiwani Zanzibar. Lakini, kupitia misaada inayotolewa na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupunguza Makali ya UKIMWI – PEPFAR, na misaada ya kiufundi inayotolewa na vituo vya CDC na Chuo Kikuu cha CU, wizara imeanzisha mipango madhubuti ya kurefusha na kuboresha maisha ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Kupitia msaada huu, akina mama wajawazito sasa wanaweza kufaidika na huduma pamoja na dawa zinazoweza kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wake. Aidha, waathirika wa UKIMWI wanaohitaji tiba wanaweza kupata tiba ya bure ya kupunguza makali ya UKIMWI.