Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Kitengo cha kuimarisha uchumi na biashara cha USAID kinatathmini fursa za ushirikiano nchini Tanzania
Februari 16, 2006
Jacqueline E. Schaefer, mkuu wa kitengo kinachoshughulikia masuala ya uchumi, kilimo na biashara - Bureau for Economic Growth, Agriculture and Trade (EGAT) - katika shirika la misaada la USAID anatembelea Tanzania wiki hii kujifunza zaidi jinsi uchumi wa nchi hii unavyokua kwa nguvu.
Kama mmoja wa mameneja watatu waandamizi katika shirika la USAID (mmoja anaongoza kitengo kinachoshughulikia masuala ya afya na demokrasia duniani, na mwingine ni mkuu wa kitengo cha kusuluhisha migogoro na kutoa misaada ya dharura), Bi Schafer anasimamia idadi kubwa ya miradi inayoshughulikia sekta ya kilimo; mikopo na uwekezaji katika sekta binafsi; uimarishaji wa uchumi; elimu; nishati na teknolojia ya mawasiliano; sera ya mazingira na sayansi; usimamizi wa maliasili; upunguzaji wa umaskini; na masuala yanayohusu wanawake na jinsia.
Bi. Schafer ana uzoefu wa miaka zaidi ya 30 katika masuala ya sera na usimamizi wa miradi ya mazingira na maliasili serikalini. Yuko hapa nchini kujifunza jinsi ya kujenga uhusiano kati ya Washington na miradi mipya pamoja na ya zamani inayotekelezwa katika nchi za Afrika ya Mashariki, ikiwemo Tanzania.
Bi. Schafer pia atafanya tathmini ya uwezekano wa kutekeleza hapa nchini mipango miwili ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais wa Marekani – Mpango wa Kutokomeza Njaa Barani Afrika na Mpango wa Kuimarisha Ushindani na Biashara. Akiwa nchini Tanzania, Bi. Schafer atakutana na wadau wanaoshirikiana na USAID, maafisa wa Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa setka binafsi katika miji ya Arusha, Dar-es-Salaam, Morogoro, na Zanzibar ili kubainisha aina ya uhusiano unaofaa, na wadau wapi washirikishwe katika shughuli mbalimbali zitakazoanzishwa hapo baadaye.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini Tanzania, Bi. Pamela White, “jukumu la kitengo cha EGAT ni kuhakikisha kwamba miradi ya USAID inashughulikia kikamilifu changamoto za kuwaunganisha wazalishaji na masoko husika, kuanzisha mifumo ya kutengeneza chakula na lishe, kuinua kiwango cha tija katika sekta ya kilimo, na kuhakikisha kwamba kuna usimamizi madhubuti wa maliasili zinazohitajika kuimarisha kilimo endelevu.”
Bi. Schafer pia atahudhuria warsha juu ya utalii endelevu ambayo imefadhiliwa na EGAT, itakayoanza Jumapili Februari 19 kwenye hoteli ya Ngurdoto Lodge mkoani Arusha. Warsha hiyo itaimarisha utalii endelevu kwa kujadili mbinu za kubaini mwelekeo mzima wa sekta ya utalii, kuepuka hatari zinazoathiri sekta hiyo, na jinsi ya kutathmini miradi inayofaa kwa utalii.



