Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Balozi wa Marekani Michael L. Retzer azindua vipindi vya redio ya WAPO

Februari 20, 2007

Balozi wa Marekani Michael L. Retzer amezindua leo Februari 20, 2007 miradi miwili jijini Dar-es-Salaam ambayo imepata msaada wa kiasi cha Sh.32, 582,375 kutoka kwenye mfuko maalum wa Balozi wa kusaidia miradi midogo midogo (Ambassador’s Special Self-Help Fund - ASSHF) na mfuko wa Ubalozi wa kuimarisha demokrasia na haki za binadamu (Embassy’s Democracy and Human Rights Fund - DHRF).

Miradi hiyo ni Shule ya Msingi ya Shalom ambayo ilipewa Sh.9, 386,000 kutoka mfuko maalum wa Balozi wa kusaidia miradi midogo midogo (ASSHF) kugharamia ujenzi wa madarasa mawili, ofisi mbili na choo. Mfuko wa ASSF unahamasisha ari ya kujitegemea kwa kuiwezesha jamii kuchukua hatua za maendeleo. Mfuko huo unajishughulisha na kutoa misaada kwa miradi ambayo manufaa yake yanagusa jamii nzima.

Mradi mwingine ulipokea Sh. 23,196,375 kupitia mfuko wa DHRF, kusaidia utayarishaji wa vipindi vya elimu vya redio vya shirika la WAPO vinavyolenga kuhamasisha masuala ya haki za binadamu na demokrasia.

Akizindua vipindi hivyo vya redio, Balozi Retzer alisema kwamba Ubalozi unafurahi sana kuweza kutoa mchango huu muhimu kwa shirika la WAPO. “Mimi nafikiri ni muhimu zaidi, kwetu sisi kutambua juhudi za pamoja kati ya watu kama ninyi, na Ubalozi wa Marekani kuhusu lengo la uimarishaji wa masuala ya haki za binadamu na demokrasia nchini Tanzania. Juhudi hizi, ambazo wote tunazithamini sana, hazina budi kukumbatiwa na wote - - kuanzia na viongozi wa serikali na biashara, hadi kwa kila mtu binafsi - - kwa lengo la kuimarisha ubora wa elimu na masuala ya haki za binadamu na demokrasia, ili kuhakikisha kuwa taifa linazidi kupiga hatua za kuleta maendeleo,” alisema Balozi Retzer.

Lengo la mfuko wa DHRF ni kuunga mkono haki za binadamu na demokrasia. Mfuko huo unasaidia shughuli ambazo zinahamasisha demokrasia ya vyama vingi, pamoja na kutetea haki za binadamu na raia, badala ya miradi ya maendeleo ambayo utekelezaji wake ni wa muda mrefu. Mfuko wa DHRF unatoa fursa ya kusaidia na kuimarisha taasisi za kidemokrasia na vyama vya kiraia, pamoja na kuzingatia maadili na mikakati ya kidemokrasia katika nchi za Afrika.