Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Balozi wa Marekani afungua warsha ya AWA Pemba
Februari 27, 2007
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael L. Retzer, leo Februari 27, 2007, alifungua warsha kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi kwa Ajili ya Kuhamasisha Amani, ambayo imeandaliwa na taasisi ya kutetea wanawake barani Afrika - Advocacy for Women in Africa (AWA), kisiwani Pemba. Warsha hiyo itamalizika Machi 4, 2007.
Katika hotuba yake, Balozi Retzer alisema kwamba anaona fahari kwamba Serikali ya Marekani imeweza kutoa msaada utakaochangia kufanikisha malengo ya mkutano huo. “Lengo la warsha hii ni rahisi, lakini ni muhimu sana. Pamoja na wanawake wa Pemba, taasisi ya AWA inatarajia kujenga msingi unaohitajika kutokomeza umaskini, kupitia maendeleo ya kiuchumi,” alisema Balozi Retzer.
Alisema kwamba kupitia warsha hiyo, washiriki watapata uzoefu muhimu katika uwezeshaji wa kiuchumi, wataimarisha ujuzi wao wa kutoa maamuzi, na watajishughulisha katika kuhamasisha amani, jambo ambalo litachangia kuleta maendeleo zaidi ya kiuchumi.
“Ningependa kuchukua muda kidogo kuwapeni taarifa zaidi kuhusu mfuko wa DHRF. Mfuko huo una historia ya mafanikio mengi katika juhudi zake za kushirikiana na jumuia za Kitanzania. Mpango huu wa kipekee ulianzishwa miaka saba iliyopita, kuunga mkono mchakato wa kujenga demokrasia barani Afrika,” alisema Balozi Retzer.
Taasisi ya AWA ilipata ufadhili wa mfuko wa Ubalozi wa Marekani wa DHRF kusaidia kuandaa warsha hii kwa wanawake wa Pemba kutoka vyama mbalimbali vya siasa, ili kuondoa tofauti zilizopo kati yao na kuwajengea ujuzi wa kupanga, kutetea haki zao na kufanya maamuzi.
Rais wa taasisi ya AWA na Bunge la Afrika, Balozi Gertrude Mongella, alitoa hotuba rasmi ya kufungua warsha hiyo. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, taasisi ya AWA imekuwa ikifanya kazi pamoja na wanawake katika nchi mbalimbali barani Afrika kuhamasisha amani, kupitia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. Uzoefu wa taasisi ya AWA kupitia shughuli kama hizo unaonyesha kwamba, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni msingi wa kupunguza umaskini, jambo ambalo linahamasisha upatikanaji wa amani.
Taasisi ya AWA ina uzoefu katika nyanja za kuhamasisha amani ili kuleta maendeleo ya kiuchumi. Uzoefu ilioupata AWA katika kuhamasisha amani unaonyesha kwamba kuna uwiano wa karibui kati ya uwezeshaji wa kiuchumi, kufanya maamuzi, na ushiriki wa wanawake katika kuhamasisha amani na maendeleo ya kiuchumi katika ngazi zote. Wanawake wamejitoa kuhamasisha amani katika jamii, familia, na taifa. Ni lengo la taasisi ya AWA kuendelea kuhamasisha amani, kupitia miradi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.




