Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Tamthilia ya Mama Ushauri kuwaelimisha wanawake juu ya njia za kisasa za kupanga uzazi

Machi 7, 2007

Mradi wa T-MARC, ukishirikiana na Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii utazindua Machi 9, 2007 saa nne asubuhi kipindi cha redio cha tamthilia kuhusu afya ya uzazi kinachoitwa Mama Ushauri, ambacho kitakuwa kinarushwa hewani kwa muda wa miezi sita. Uzinduzi huo utafanyika kwa ushirikiano wa jamii inayoizunguka Zahanati ya Tandale wilayani Kinondoni. Mama Ushauri anafamika na Watanzania wengi kama mtu ambaye anaongea kwa uwazi na hafichi kitu. Mama Ushauri siyo mtaalamu wa masuala ya uzazi wa mpango, lakini ni mtetezi aliyebobea wa wanawake na familia zao, kuhusu masuala ya afya ya uzazi. Lengo lake ni kusaidia kuondoa dhana potofu kuhusu afya ya uzazi, na anawahamasisha wanawake kutafuta ushauri wa watoa huduma za uzazi wa mpango ili waweze kuchagua njia ambayo inawafaa wao.

Wageni wa heshima kwenye uzinduzi huo watakuwa ni Mama Regina Lowassa, mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Pamela White, Mkurugenzi Mkazi wa shirika la misaada la Marekani USAID, pamoja na Mama Ushauri mwenyewe.

Kipindi hicho cha tamthilia cha Mama Ushauri cha dakika 10 kitakuwa hewani kila wiki na kurudiwa kwenye vituo vya utangazaji vya Radio Tanzania, Radio Free Africa na Radio One. Baada ya vipindi 6-10, shirika la T-MARC pia litafadhili kipindi cha dakika 10 cha maswali na majibu, ili kuwapa wasikilizaji fursa ya kuuliza maswali juu ya mpango wa uzazi na kusisitiza taarifa muhimu.

Tamthilia hiyo inazingatia maisha ya kila siku ya familia tatu na marafiki zao wanaoishi katika mtaa wa kubuni wa Goromonzi. Kila kipindi kina zingatia juu ya hali ya wanawake wakiwa katika awamu mbalimbali za maisha yao ya uzazi. Mama Ushauri anaishi Goromonzi. Ni mama mwenye busara na ujasiri, na anatumia uzoefu wake wa maisha kuhamasisha matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi. Pia anawahamasisha wanawake na waume zao kujadili nyumbani masuala ya kupanga uzazi, na kuwatembelea watoa huduma za mpango wa uzazi ili wapate taarifa na huduma zaidi.

“Mama Ushauri anapendwa na wasikilizaji wengi,” anasema Keziah Kapesa, rais wa chama cha wauguzi na wakunga binafsi (Private Nurse/Midwives Association of Tanzania - PRINMAT). “Watoa huduma wa kliniki za Wizara ya afya, pamoja na taasisi ya PRINMAT wako tayari kuwasaidia wasikilizaji wa kipindi cha Mama Ushauri kuchagua njia inayokidhi mahitaji yao - kwa wale wanaotumia kwa mara ya kwanza, pamoja na wazoefu.”

Pamela White, Mkurugenzi Mkazi wa shirika la misaada la Marekani USAID alidokeza kwamba, “ingawa uzazi wa mpango umeonyesha dhahiri kwamba unaweza kupunguza vifo vya akina mama vinavyohusiana na matatizo ya uzazi, hata hivyo idadi ya wanawake wanaotunga mimba na wale wanaokufa kwa matatizo ya uzazi bado ni kubwa sana nchini Tanzania. Asilimia 22 ya wanawake walio katika ndoa wana mahitaji ambayo hayajakidhiwa kuhusu mpango wa uzazi. Kitaifa, ni mwanamke mmoja tu aliyeolewa, kati ya watano wanaotumia njia za kisasa za kupanga uzazi, na hali ni mbaya zaidi vijijini. Kuna mabadiliko machache sana katika takwimu za matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi tangu mwaka wa 1999.” Bi. White aliendelea kusema, “Wanawake Watanzania wenye nguvu na afya njema ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi, na mwanamke mwenye uwezo wa kuamua ukubwa wa familia yake ana fursa kubwa zaidi ya kuchangia katika maendeleo ya jamii, kuwalisha na kuwaelimisha watoto wake, pamoja na kuitunza familia yake. Shirika la misaada la Marekani la USAID linatarajia kwamba, mchezo wa kuigiza wa Mama Ushauri utawahamasisha wanawake kutafuta huduma wanazohitaji kutoka kwa watoa huduma za mpango wa uzazi, na kutokomeza dhana potofu zinazowanyima wanawake afya bora. Wanawake wana haki na wajibu wa kuchagua.”

Kwa jumla, ujumbe wa Mama Ushauri ni kwamba, kuna njia muafaka kwa kila mtu. Mama Ushauri anawahamasisha wanawake kwenda peke yao au na waume zao kwa mtoa huduma ya mpango wa uzazi aliye karibu ili kutafuta taarifa. Kupitia msaada wa USAID na Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, shirika la T-MARC litaendelea na kampeni za kusaidia jamii, ili kuhakikisha kwamba wanawake nchini Tanzania wanaweza kufanya maamuzi muafaka kukidhi mahitaji yao ya kupanga uzazi.

Mradi wa T-MARC Project unafadhiliwa na Serikali ya Marekani, kupitia shirika la misaada la Marekani la USAID, na unashughulikia masuala ya kuzuia UIMWI, afya ya uzazi, na kuzuia vifo vya watoto.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Abdulrazak Badru
Communications Director
T-MARC Project
Simu: 0754-280048
Barua pepe: abadru@tmarc.or.tz