Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Press Releases > Marekani Yasaidia Ukarabati wa Misikiti ya Kihistoria Pemba
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Close Window Sheikh Nassour wa Msikiti wa Shumba Mjini, wa Micheweni, Pemba, akimuonyesha Kaimu Naibu Balozi wa Marekani Tulinabo Mushingi Korani ya kihistoria ya msikiti huo wakati wa sherehe za kukamilika ukarabati wa msikiti huo uliofadhiliwa na watu wa Marekani.
Sheikh Nassour wa Msikiti wa Shumba Mjini, wa Micheweni, Pemba, akimuonyesha Kaimu Naibu Balozi wa Marekani Tulinabo Mushingi Korani ya kihistoria ya msikiti huo wakati wa sherehe za kukamilika ukarabati wa msikiti huo uliofadhiliwa na watu wa Marekani.

Marekani Yasaidia Ukarabati wa Misikiti ya Kihistoria Pemba

  • Mradi wa Ukarabati wa Misikiti ya Micheweni na Shumba wenye thamani ya Dola za Kimarekani 25,589 Wakamilika

  • Machi 9, 2009

    Kaimu Naibu Balozi wa Marekani nchini, Bw. Tulinabo Mushingi hapo Jumatatu, tarehe 9 Machi 2009 aliwasili kisiwani Pemba, Zanzibar ili kushiriki katika hafla ya kukamilika kwa kazi ya ukarabati wa misikiti miwili mikongwe zaidi kisiwani humo iliyopo katika vijiji vya Micheweni na Shumba. Kazi hiyo ya ukarabati iliyochukua miaka kadhaa, ilifanyika kwa gharama ya zaidi ya Dola za Kimarekeni 25,000, fedha zilizotolewa na Mfuko wa Ubalozi wa Marekani wa Kusaidia Shughuli za Hifadhi ya Utamaduni.

    Katika hotuba yake wakati wa hafla ya kukamilika kwa ukarabati wa misikiti hiyo katika vijiji vya Micheweni na Shumba, Bw. Mushingi alisema, “Pale Idara ya Mambo ya Kale ya Zanzibar ilipobainisha haja na umuhimu wa kukarabati misikiti hii ya kipekee na ya kihistoria na kutujulisha kuhusu jambo hilo tulikuwa tayari kusaidia. Hii ni kwa sababu Marekani na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi zinazothamini na kuheshimu sana tofauti za kiimani katika jamii zetu.”

    Sehemu kubwa ya kazi ya usimamizi na ukarabati huo iliyofanywa kwa miaka kadhaa kwa uhodari na umakini mkubwa, ilifanywa na wanavijiji wenyewe, kwa msaada wa kitaalamu kutoka kwa Idaya ya Mambo ya Kale na msaada wa fedha kutoka kwa watu wa Marekani. “Mitindo na nakshi za kipekee za misikiti hii ambazo zimejumuisha tamaduni za ujenzi za Kiswahili na Kiajemi za Kuanzia karne ya 17 hadi ya 18, zimehifadhiwa vyema na zitatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo vya Micheweni and Shumba.” Alisema Bw. Mushingi.

    Serikali ya Zanzibar ilichukua jukumu la kukarabati misikiti hiyo ili kuhakikisha kuwa hali ya kuharibika kwake inadhibitiwa kwa kuimarisha hali ya majengo na mazingira yake. Lengo la shughuli hii lilikuwa ni kulinda na kuihifadhi misikiti hii muhimu ya kihistoria.

    Mfuko wa Ubalozi wa Marekani wa Kusaidia Shughuli za Hifadhi ya Utamaduni hutoa ruzuku ndogo kwa ajili ya kusaidia hifadhi ya amali mbalimbali za kitamaduni nchini Tanzania na katika nchi nyingine.

    Hadi hivi sasa Mfuko huu umeshasaidia zaidi ya miradi 400 duniani kote, yenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 10. Shughuli zinayoweza kufadhiliwa na mfuko huu ni pamoja na misaada ya kiufundi ya ukarabati wa majengo ya kihistoria; tathmini na uhifadhi wa mambo mbalimbali katika makumbusho; hifadhi ya maeneo yenye historia ya kale; Kuweka kumbukumbu kuhusu kazi za mikono za kitamaduni zilizo katika hatari ya kupotea; kuboresha uhifadhi wa nyaraka na machapisho mengine ya zamani; kurekodi na kutunza historia itolewayo kwa mdomo; na kuweka kumbukumbu za kimaandishi za lugha za kijadi. Miradi iliyopatiwa ruzuku hivi karibuni nchini Tanzania ni pamoja na ule wa Ukarabati wa Magofu ya Kaole huko Bagamoyo, uliofanywa na Idara ya Mambo ya Kale mwaka 2007, kuweka kumbukumbu ya nyaraka kuhusu biashara ya utumbwa Zanzibar, uanzishwaji wa maktaba huko Chake Chake na ukarabati wa msikiti wa kihistoria wa Kizimkazi.

    Mfuko wa Ubalozi wa Marekani wa Kusaidia Shughuli za Hifadhi ya Utamaduni unaendeshwa kwa niaba ya watu wa Marekani kwa ubia na watu wa Tanzania, na ni sehemu ya msaada wa rasmi utolewao na Serikali ya Marekani kwa Tanzania wa zaidi ya Shilingi za Kitanzania bilioni 750 kwa mwaka.

    Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti http://tanzania.usembassy.gov.