Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Utafiti wabainisha Watanzania walio wengi wanasubiri, lakini wachache ni waaminifu katika ndoa zao

Machi 17, 2006

Kwa mujibu wa utafiti wa serikali juu ya takwimu zinazohusu masuala ya afya na jamii, Demographic and Health Survey (DHS) uliofanywa hivi karibuni, uwezo wa Watanzania kusubiri kufanya ngono mpaka baada ya ndoa ni mkubwa zaidi kuliko wa Wamarekani. Hata hivyo, ni asilimia ndogo tu ya watu waliohojiwa wanaamini kwamba Watanzania walio katika ndoa ni waaminifu kwa wenzi wao.

Utafiti huo ulibainisha kwamba, asilimia 85 ya watu waliohojiwa wanaamini kuwa watu walio kwenye ndoa ni vizuri wakashiriki ngono na wenzi wao tu, lakini pia wakasema asilimia 85 ya wanandoa wanaowafahamu wana wapenzi nje ya ndoa.

Asilimia inayokubaliana na kauli zilizotolewa kuhusu uaminifu

Pam White, Mkurugenzi Mkazi wa shirika la misaada USAID ambalo lilishiriki katika utafiti huo anasema, “hali hii ni kama ule msemo wa zamani kuhusu mgahawa maarufu: ‘Hakuna anayeenda huko tena – watu huwa wanajaa mno!’ Kuna hitilafu ya kimsingi kama kila mtu anakubaliana na umuhimu wa kuwa mwaminifu, lakini wanaopaswa kuwa waaminifu ni watu wengine.”

Utafiti huo pia unaonyesha kwamba, kulinganisha na Marekani, asilimia kubwa zaidi ya Watanzania wanasubiri kabla ya kujihusisha na vitendo vya ngono. Uwezekano wa Watanzania walio chini ya umri wa miaka ishirini na ambao bado hawajafunga ndoa, kusubiri kufanya ngono ni mkubwa kwa asilimia 35 kuliko wa wenzao huko Marekani. Hii ni kweli hususan kwa wanawake wa Kitanzania, ambao asilimia 70 huwa wanasubiri, ikilinganishwa na asilimia 50 ya wanawake walio na umri wa miaka chini ya ishirini nchini Marekani.

Matokeo ya utafiti huu yametolewa wakati mmoja na kufanyika kwa mkutano maalumu wa taasisi ya YouthNet uliofanyika jana jijini Dar-es-Salaam. Mkutano huo ulijadili kuhusu mbinu za kusambaza ujumbe wa “Uwe Mwaminifu,” pamoja na umuhimu wa kupunguza idadi ya wapenzi. Wataalamu na vijana walioshiriki kwenye mkutano huo walijadili hisia za Watanzania kuhusu uaminifu katika mahusiano. Pamoja na kuwa mwaminifu na kutumia kondomu kila mara, Kamisheni ya Kuzuia Ukimwi Tanzania (TACAIDS) inasema uaminifu ni njia ya msingi katika mikakati ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI nchini.

Aidha utafiti huo ulionyesha pia kwamba kuna mikoa mitatu nchini ambayo ina zaidi ya asilimia kumi ya wanawake walioolewa, ambao waume zao wana wake zaidi ya mmoja. Zaidi ya asilimia 10 ya wanawake walioolewa katika mikoa ya Arusha, Mara, na Manyara wanachangia mume pamoja na mke wa pili - na mara nyingine wa tatu na hata wa nne. Matokeo haya yaliwafanya watafiti wanaoangalia suala la uaminifu katika ndoa nchini Tanzania kujiuliza – “Je, uaminifu unamaanisha ni lazima ‘kuwa na mwenzi mmoja tu’?”

Mkurugenzi Mkazi wa taasisi inayoshughulikia masuala ya afya kwa familia na vijana, FHI/YouthNet, Matthew Tiedemann, alijibu na kusema: “Katika ndoa yenye wake wengi, uaminifu unaweza kumaanisha kwamba mtu anakuwa mwaminifu kwa wenzi wake wote… Kama watu wote katika ndoa kama hiyo hawana virusi vya UKIMWI, na wote ni waaminifu kwa ndoa hiyo, basi hakuna mtu kati yao atakayepata virusi vya UKIMWI.

Mada zilizotolewa mara kwa mara na washiriki wa mkutano huo maalum zilisisitiza kwamba, mikakati bora kabisa ya kutunza afya inategemea juhudi za kuhamasisha watu kuendelea kusubiri kufanya ngono mpaka baada ya ndoa; kuthibitisha hali ya afya yako kwa kupima UKIMWI mara kwa mara; pamoja na kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako – hata kama mila na desturi zinakuruhusu kuwa na mke zaidi ya mmoja.

Taasisi ya YouthNet inafadhiliwa na mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI, PEPFAR. Mwaka huu, mpango huo utatoa zaidi ya Shilingi bilioni 30 kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI nchini Tanzania. Fedha zilizotengwa kwa shughuli za kinga zitatumiwa kuhamasisha ujumbe wa kusubiri na ‘kuwa mwaminifu,’ pamoja na kununua kondomu na promosheni. Maafisa wa USAID walisema kwamba wataanza kufanya promosheni ya aina mpya ya kondomu nchini Tanzania mwishoni mwa mwezi huu.

- Translation -
This content is also available in English