Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

USAID yaongeza msaada wa Shs 847,700,000 kuzuia homa ya ndege

Machi 24, 2006

Shirika la misaada la USAID nchini Tanzania limetoa Shs 847,700,000 kwa Chuo Kikuu cha Minnesota na tasisi mbalimbali, zikiwemo taasisi ya kutafiti magonjwa ya wanyama, Animal Disease Research Institute (ADRI), taasisi ya taifa ya kutafiti masuala ya tiba, National Medical Research Institute (NIMR), taasisi ya kutafiti wanyama pori, Tanzanian Wildlife Research Institute (TAWIRI) na mradi wa kutafiti ndege nchini, Tanzania Bird Atlas Project (TBAP).

Fedha hizi zitatumiwa kuboresha shughuli za uchunguzi wa wanyama na binadamu ili kubainisha kuwepo kwa homa ya mafua nchini Tanzania. Mpango huo pia utajenga uwezo wa maabara kuweza kuchunguza kuwepo kwa homa ya mafua, ili vipimo kuhusu homa ya mafua ya ndege viweze kufanyika nchini hapa kwa gharama ndogo, badala ya kupeleka vipimo hivyo nchi za nje. Juhudi hizi zitasaidia kuzuia au kupunguza tishio la homa ya ndege siyo tu nchini Tanzania, bali ulimwenguni kote.

Kiasi hiki cha Shs. 847,700,000 kinachotolewa kwa taasisi hizo ni nyongeza kwa Shs. 236,145,000 zilizotolewa kupitia shirika la USAID katika miezi michache iliyopita, kuisaidia serikali ya Tanzania kujiandaa na uwezekano wa kuingia kwa homa ya ndege hapa nchini:

  • Shirika la USAID lilitoa Shs. 90,825,000 kufanya uchunguzi juu ya ndege pori nchini Tanzania kuanzia Desemba mpaka Machi. Uchunguzi huu unafanywa na mradi wa Tanzania Bird Atlas Project unaosimamiwa na taasisi ya kutafiti wanyama pori, Tanzania Wildlife Research Institute (hii ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii), pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo. Uchunguzi wa vipimo bado unaendelea. Mradi wa Tanzania Bird Atlas Project nao unaendelea na uchunguzi wa ndege pori katika miezi ijayo.
  • Shirika la misaada la Ujerumani, Deutsche Gesellschaft für Technische Zusammenarbeit (GTZ, German Agency for Technical Development), lilitoa Shs. 84,770,000 kusaidia shughuli za kufanya vipimo.
  • Shirika la USAID limetoa Shs. 60,550,000 kwa kampuni ya Abt Associates kutoka Marekani kuboresha mfumo wa kuchunguza kuwepo kwa homa ya mafua katika binadamu nchini Tanzania, Integrated Disease Surveillance and Response System. <

Shirika la misaada la Marekani nchini Tanzania, USAID/Tanzania, ni mwanachama hai wa kamati ya kiufundi ya sekta ya afya kuhusu homa ya ndege, Health Sector Avian Influenza Technical Committee, na linasaidia kuandaa mpango wa dharura wa sekta ya afya kukabiliana na tishio hilo, Health Sector Emergency Preparedness and Response Plan. USAID/Tanzania pia inashiriki katika kamati ya taifa ya kukabiliana na homa ya mafua ya ndege, National Joint Task Group on Avian Influenza.

Hivi sasa, aina ya homa ya ndege H5N1 imebainika kuwakumba ndege na kuku barani Afrika. Kufikia mwezi Machi, homa hiyo ilikuwa imegunduliwa katika nchi za Misri, Niger, Nigeria, na Cameroon, na ni suala la muda kidogo tu kabla haijafika katika eneo la Afrika ya Mashariki. Hata hivyo, serikali ya Tanzania, kupitia msaada wa mashirika ya USAID na GTZ imekuwa ikijitayarisha kukabiliana na homa hiyo pindi itakapowasili.

Ingawa hakuna ushahidi wa kuwepo kwa homa ya mafua ya ndege katika kuku na binadamu nchini Tanzania, kuna uwezekano kwamba virusi vya ugonjwa huo vitaingia nchini kupitia kuku, au ndege pori wanaohamahama. Kuku wakishaambukizwa, virusi huenea haraka sana kutoka eneo hadi eneo. Aina kali ya virusi hivyo inaweza kuangamiza makundi mazima ya kuku na hivyo kusababisha hasara kubwa kiuchumi. Njia nzuri ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo ni kuua makundi ya kuku, lakini hii pia huongeza madhara kwa uchumi wa nchi. Watu wanaofanya kazi kwenye mazingira yaliyo na kuku walioathrika wako hatarini kuambukizwa na virusi hivyo, na matokeo yake ni mabaya: Kati ya watu 177 ambao mpaka sasa wameshawahi kuambukizwa duniani, 98 wamefariki. Ingawa kwa hivi sasa virusi hivyo havina uwezo wa kuambukizwa kutoka binadamu mmoja hadi mwingine, vina nguvu ya kujibadilisha, na vinaweza kupata uwezo huo wakati wowote. Kama mabadiliko hayo yatatokea, hali hii itasababisha janga kubwa ambalo linaweza kuangamiza mamilioni mengi ya binadamu.

Kuhamahama kwa ndege pori kunaweza pia kuingiza homa ya mafua ya ndege nchini Tanzania. Tayari idadi ya ndege milioni tatu hadi tano wamekwishaifikia Tanzania katika safari yao ya kuhama kila mwaka kutoka Asia na Ulaya ya Kati, ambako inawezekana waliambukizwa na ndege walioathirika. Kwa sababu kuhamahama huku ni safari ya mzunguko inayoendelea wakati wote, ndege hawa wanaporudi kaskazini wanaweza kuambukiza ndege wengine huko Ulaya. Baadaye, ndege hao watakaporudi kusini wataambukiza wengine barani Afrika.

Vijiji vingi nchini Tanzania viko kwenye njia inayotumiwa na ndege hao wanaohamahama. Wanavijiji wanafuga kuku ambao hutembea nje na hivyo kuweza kuangukiwa na kinyesi cha ndege wanaoruka juu yao, ambao huenda wameambukizwa na virusi vya homa ya ndege. Ni muhimu kuanzisha mfumo wa kuchunguza ndege pori, kuku, pamoja na binadamu ili kuweza kugundua kuwepo kwa homa ya mafua ya ndege haraka iwezekanavyo.

- Translation -
This content is also available in English