Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Marekani Yamtambua Bi. Malecela kama Mwanamke Jasiri wa Kitanzania kwa Mwaka 2009
Machi 26, 2009
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Larry André leo amemkabidhi cheti Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, ambaye amechaguliwa na Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam kama Mwanamke Jasiri wa Kitanzania kwa Mwaka 2009.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika Ubalozi wa Marekani, tuzo hiyo ya mwaka ilianzishwa kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa mwanamke aliyeonyesha ujasiri wa kiwango cha juu na uongozi mzuri.
Aidha, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulimteua Bi. Malecela kuwa mmojawapo kati ya washiriki waliowania Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri ya Mwaka 2009, kutokana na ujasiri aliounyesha katika kukosoa na kuupa changamoto uongozi wa chama chake ili uweze kushughulikia kikamilifu suala la rushwa. Kwa kufanya hivyo alivunja utamaduni wa kisiasa uliokuwa umejengeka bila kujali vitisho kwa usalama wake binafsi. Bila kuchoka wala kutetereka, Bi Malecela alishikilia azma yake ya kupiga vita rushwa na kuuliza maswali mazito yaliyoibua mijadala iliyochangia sana katika jitihada za kuongeza uwazi na utawala bora ndani ya chama tawala.
Akimkabidhi Bi. Malecela tuzo hiyo, katika hafla fupi iliyoandaliwa kwa heshima yake na kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwezi wa Historia ya Wanawake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Bw. André alisema, “Azma ya Marekani ya kukuza demokrasia, ustawi na usalama duniani kote haiwezi kufikiwa bila ya kuwajengea uwezo wanawake. Iwapo wanawake hawawezi kushiriki katika michakato ya kisiasa, basi hapawezi kuwa na demokrasia ya kweli. Iwapo wanawake wananyimwa fursa za kiuchumi, maendeleo yatakwama. Iwapo wanawake hawana elimu hawawezi kuwaelimisha pia watoto wao na hakutakuwa na usalama wa kweli kwa kizazi kijacho. Kwa kupitia tuzo hii inayotolewa kila mwaka Marekani inatambua na kuheshimu ujasiri wa wanawake waliotoa mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ya nafasi zao katika jamii.”
Katika mwaka 2009 Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri wa Afrika ilienda kwa Bi Hadizatou Mani wa Niger, ambaye aliuzwa utumwani akiwa na umri wa miaka 12 kwa kiasi cha kama dola 500. Bi Mani ambaye ni mmoja kati ya mashujaa waliosimama kidete katika mapambano ya kutokomeza utumwa mamboleo, alipigania bila kuchoka uhuru wake na hivi sasa anawasaidia watu wengine wanaopitia hali kama aliyopitia yeye kutafuta haki na uhuru wao.
Wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ya 2009, Rais Barack Obama wa Marekani alisema, “Changamoto zinazotukabili ni nyingi, kutoka mabadiliko ya hali ya hewa duniani, umasikini na hata migogoro na vita. Wanawake ni watu muhimu sana katika ufumbuzi wa matatizo yote hayo na kwamba hatutakuwa tumepanda mbegu ya mustakabali mwema wala kunufaika na mabadiliko tunayoyahitaji bila ya ushiriki kamilifu wa wanawake. Duniani kote wanawake wana nafasi na jukumu muhimu katika kusimamia afya na elimu ya familia zetu, ni wasimamizi wa mashamba yetu, viwanda vyetu, madarasa yetu, maabara zetu na hata katika bodi zetu. Bila kujali iwapo wanapata tuzo na shukrani au la au, wanawake wametufundisha kuhusu imani, ujasiri na kuhusu kutumia fursa zilizopo. Marekani inatumaini kubwa kuwa binti zetu na binti wa mataifa yote wataendelea kuhudumia jamii zetu kama viongozi katika jitihada zetu za pamoja za kuinua ustawi wetu na kwamba watakuwa na fursa za kujiendeleza kwa kadri ya upeo wa uwezo wao. Leo hii Michelle na mimi, tunakumbuka, tunasherehekea na kuheshimu kujitoa, vipaji na uongozi wa wanawake duniani kote.
Tuzo ya kwanza ya Mwanamke Mtanzania Jasiri ilitolewa mwaka 2008 kwa Bi. Helen Kijo-Bisimba, kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kazi yake ya kusaidia na kuimarisha haki za wanawake.




