Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Mpango wa PEPFAR kufadhili huduma za tohara kwa wanaume
Machi 29, 2007
Mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupunguza makali ya UKIMWI unaojulikana kama PEPFAR umeafiki tangazo lililotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shrika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti UKIMWI (UNAIDS), la kuunga mkono huduma salama za tohara kwa wanaume. Kwa mujibu wa WHO/UNAIDS, uwezekano wa wanaume waliotahiriwa kuambukizwa na virusi vya UKIMWI ni mdogo, ikilinganishwa na wanaume ambao bado hawajatahiriwa.
Mratibu wa Marekani wa masuala ya UKIMWI duniani, Balozi Mark Dybul, alisema kwamba mpango wa PEPFAR unatambua ushahidi wa kisayansi unaozidi kuongezeka, pamoja na mwongozo mpya kutoka WHO/UNAIDS ambao unaunga mkono tohara kwa wanaume, kwa lengo la kuzuia maambukizi ya UKIMWI. Kwa hiyo, mpango wa PEPFAR utafuata mapendekezo ya WHO/UNAIDS kuhusu tohara kwa wanaume, kwa lengo la kuzuia maambukizi ya UKIMWI na kuzingatia msimamo wa sera na tamaduni za serikali ya kila nchi husika.
“Mpango wa PEPFAR utafadhili huduma ya tohara salama kwa wanaume, ikiwa serikali za nchi husika zitakubali pendekezo hili jipya la kinga dhidi ya UKIMWI kama sehemu ya mkakati mkubwa wa kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema Balozi Dybul.
Aliongezea, “Mpango wa PEPFAR una shauku kuendeleza ushirikiano na serikali za nchi husika; Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti UKIMWI (UNAIDS); pamoja na wadau wengine, ili kuitikia ushahidi wa kisayansi na mwongozo unaounga mkono tohara salama kwa wanaume, kwa lengo la kudhibiti UKIMWI.”
Msaada wa kifedha kutoka PEPFAR utatumiwa kusaidia utekelezaji wa huduma ya tohara salama kwa wanaume, chini ya uongozi wa serikali ya nchi husika, kwa kuzingatia sera na taratibu za nchi hiyo. Lakini mpango wa PEPFAR unasisitiza kwamba tohara zifanywe katika mazingira ya hospitali na ngariba waliopata mafunzo. Huduma hizo zitafanyiwa tathmini mara kwa mara.
Mafunzo ya kitabibu yafanywe huku mikakati ya mawasiliamo na kutoa ushauri nasaha ikiendelezwa. Serikali za nchi husika zitaweka viwango vya ubora na huduma za afya. Hii itaenda sambamba na kuwekwa kwa huduma za tohara kwa wanaume katika mfumo wa utafiti na usimamizi wa ugavi.
Kwa kutambua kwamba tohara kwa wanaume si kinga kamili ya asilimia 100, ni muhimu kwa nchi zinazofikiria kuanzisha huduma hii kuiweka kama sehemu ya mikakati mingine ya kinga dhidi ya UKIMWI, ambayo inazingatia mkakati wa ABC [Abstinence (subiri), Be faithful (uwe mwaminifu), and correct and consistent Condom use (tumia kondomu kwa usahihi daima)].
Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kwamba huduma ya tohara kwa wanaume itolewe tu kwa wanaume ambao hawajaathirka na UKIMWI. Huduma hii siyo kwa wanaume ambao tayari wamekwishaathirika na UKIMWI.]




