Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Press Release

Kiongozi wa wanawake wa Kimasai afanya ziara ya mafunzo Marekani

Machi 30, 2006

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya kuendeleza wanawake wa Kimasai, Maasai Women’s Development Organization, Bi Ndinini Kimesera, amechaguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya wiki tatu juu ya viongozi wanawake nchini Marekani, kuanzia Machi 30 mpaka Aprili 20, 2006. Ziara hiyo ni sehemu ya mpango maarufu unaowawezesha viongozi kutoka nchi mbali mbali kutembelea Marekani, International Visitor Leadership Program, ambao unaendeshwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Lengo la mpango huu ni kujenga mawasiliano kati ya wananchi wa Marekani na Tanzania.

Bi. Kimesera ataungana na washiriki wengine 22 kutoka nchi za Bahrain, Botswana, Cameroon, Egypt, Estonia, India, Japan, Zambia, Zimbabwe, n.k., ili kuchunguza wajibu wa viongozi wanawake katika serikali, biashara, na kuangalia suala la mafunzo kwa wananwake. Washiriki pia watapata uelewa mzuri zaidi kuhusu maadili yanayoongoza mafunzo kwa viongozi wanawake katika sekta ya elimu. Pia watachunguza nafasi ya mchango wa wanawake katika jamii ya Kimarekani; pamoja na mbinu za kujenga ushirikiano katika mafunzo miongoni mwa washiriki.

Msemaji wa Ubalozi wa Marekani John Haynes alisema kwamba, washiriki wa ziara hiyo watatembelea miji mbalimbali nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na Washington D.C., Rochester, New York; Seattle, Washington; na Orlando, Florida. Washiriki hao watagawanyika katika makundi mawili na kutembelea vijiji vya Paris na Sterling katika jimbo la Illinois. Wageni hao watafikia kwanza mjini Washington, ambako watapewa maelezo kuhusu mafanikio makubwa na miswada iliyofanikishwa na wafanyakazi wanawake nchini Marekani. Watajionea wenyewe pia jinsi teknolojia inavyotumiwa kuboresha hali ya wanawake katika sehemu za kazi.

Haynes alisema kwamba, akiwa Washington, Bi. Kimesera atakutana na maafisa wa taasisi inayoshughulikia biashara ndogondogo, U.S. Small Business Administration ambao watamwelezea kuhusu programu za uongozi kwa wanawake, pamoja na mafunzo ya uongozi wa kisiasa, kiraia na kibiashara. Kwenye kitengo cha Wizara ya Mambo ya Nje kinachoshughulikia masuala ya wanawake, kikundi hicho kitapewa maelezo kuhusu kazi na miradi ya kitengo hicho.

Halafu washiriki watagawanyika katika makundi mawili na kutembelea vijiji viwili ambako watajionea wenyewe changamoto tofauti zinazowakabili wanawake wanaoishi vijijini na katika miji midogomidogo.

Baada ya hapo, kikundi kitatembelea mji wa Seattle, katika jimbo la Washington, ambako watajifunza kuhusu masuala na programu mbalimbali kuhusu wanawake wanaoishi mijini. Washiriki watafanya mkutano na taasisi ya wapiga kura wanawake, League of Women Voters (LWV) ya jimbo la Washington. Wanawake hao wataelezea jinsi wanavyotayarisha ajenda zao za kutunga sheria na sera juu ya kodi, kudhibiti umilikaji wa bunduki, mabadiliko ya hali ya hewa, usafiri, au matumizi ya ardhi kwa kila mwaka, na jinsi wanawake hao wanavyotekeleza malengo yao.

Baada ya hapo, Bi. Kimesera na kikundi chake watasafiri kuelekea Orlando Florida katika hatua ya mwisho ya safari yao, ambako watakutana na waandishi wa habari, wafanyabiashara wanawake na viongozi wa eneo hilo.

- Translation -
This content is also available in English