Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Mtanzania aenda Marekani kwa ziara ya mafunzo ya waandishi wa habari chini ya mpango wa ‘Edward R. Murrow Programme’

Aprili 4, 2007

Mwandishi wa makala wa gazeti la “The Citizen,” Morris Mwavizo Msavia anaondoka nchini Ijumaa, Aprili 6, 2007 kushiriki kwenye ziara ya mafunzo ya wiki tatu, chini ya mpango wa “Edward R. Murrow Programme for Journalists,” yatakayoanza Aprili 9 na kumalizika Aprili 27, 2007.

Msavia ataungana na waandishi 18 wengine wa habari kutoka nchi za Botswana, Cape Verde, Ethiopia, Ghana, Kenya, Liberia, Malawi, Mauritius, Nigeria, Rwanda, Sierra Leone, Afrika ya Kusini, Sudan na Zimbabwe. Mpango huu unaoendeshwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa niaba ya wananchi wa Marekani, ni sehemu ya mpango maarufu wa kimataifa kuwawezesha wageni kufanya ziara za mafunzo ya uongozi nchini Marekani - International Visitor Leadership Programme (IVLP). Mpango huo ulianzishwa ili kufanikisha mahusiano binafsi na ya kitaaluma kati ya wananchi wa Tanzania na wenzao wa Marekani.

Malengo ya mpango wa ‘Edward Murrow’ ni kuwapa waandishi wa habari fursa ya kuchunguza haki na wajibu wa vyombo huru vya habari nchini Marekani; kupata uelewa wa mifumo ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa ya taifa la Marekani; kushiriki katika semina na kongamano za kuendeleza taaluma; pamoja na kuangalia mwenendo na changamoto katika taaluma ya uandishi wa habari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani, Msavia na washiriki wengine wataanza ziara yao kwa kulitembelea jiji la Washington D.C., na baadaye kupewa taarifa juu ya mfumo wa kisiasa wa Marekani pamoja na mchakato wa kutunga sera ya nje ya taifa hilo. Watapata pia fursa ya kukutana na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, wanachama mashuhuri wa kamati za masuala ya kimataifa za Bunge la Congress, wachambuzi na maprofesa wa vyuo vikuu, ili kujadili mchakato wa maamuzi ya sera ya nje, na kilele chake kitakuwa ni hotuba fupi itakayotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje Condoleezza Rice.

Mpango huo ambao umepewa jina la mwandishi wa habari mashuhuri na mkurugenzi wa zamani wa shirika la habari la Marekani - United States Information Agency (USIA), Bwana Edward R. Murrow, unazingatia misingi mingi ya kidemokrasia ambayo ndiyo iliyoongoza utendaji kazi wa Bwana Murrow: uaminifu, uadilifu, ujasiri, na uwajibikaji kwa jamii.

Baada ya Washington, wandishi wa habari wataelekea Lexington, katika jimbo la Kentucky, kwa wiki moja ya semina ambayo itashirikisha wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Kentucky, waandishi wa habari, pamoja na wanafunzi wa misingi ya uandishi wa habari katika jamii ya kidemokrasia. Kikundi hicho cha waandishi wa habari kitajadili masuala muhimu yanayohusu bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa Darfur na wakimbizi; uandishi wa habari za maeneo ya vijijini, kilimo na jamii; usuluhishi wa migogoro na UKIMWI. Pia watajifunza kuhusu uongozi wa kihariri, vyombo vya habari mbadala, pamoja na utumiaji wa kompyuta katika uandishi wa habari.

Washiriki wa ziara hiyo ya mafunzo pia watatembelea miji ya Albuquerque na Santa Fe, katika jimbo la New Mexico kujionea wenyewe jinsi ya kuandika habari za siasa za serikali kuu na serikali za mitaa; jinsi vyombo vya habari vinavyotumika kuelimisha; vyombo vya habari vinavyojitegemea; ushirikishi wa vyombo vya habari katika masuala ya haki za jamii; uhusiano wa vyombo vya habari; uhamasishaji pamoja na changamoto za kijamii na kiuchumi. Kikundi hicho kitatembelea pia kituo cha redio kinachoendeshwa kwa maslahi ya umma na wananchi waliojitolea. Wataangalia pia kazi ya vyombo vya habari katika kuhamasisha uwazi na utawala bora katika mchakato wa kutunga sheria. Masuala ya ushirikishaji wa jamii katika kupanga mustakabali wake, matumizi ya ardhi, mazingira, na uchumi yatajadiliwa kwenye mazungumzo na wawakilishi wa miradi mitatu inayotekelezwa na serikali kuu, serikali ya jimbo, na serikali ya mitaa.

Baadaye, washiriki wa ziara hiyo watarudi mjini Washington kushiriki kwenye kongamano la kimataifa la waandishi wa habari ambalo limetayarishwa na Wizara ya Mambo ya Nje, ikishirikiana na taasisi ya Aspen Institute. Kongamano hilo litajadili vyombo vya habari vya Marekani na masuala ya kimataifa; wajibu wa mwandishi wa habari, usahihi au uhamasishaji; uhusiano kati ya serikali na vyombo vya habari katika kuandika habari za kimataifa; na jinsi teknolojia mpya ya mawasiliano inavyogusa uandishi wa habari. Washiriki watajadili maadili ya vyombo vya habari na uwajibikaji, wajibu wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma; uwiano katika habari na uchambuzi; maoni anuwai na changamoto zinazowakabili wanataaluma wa habari.

Akiongelea kuhusu ziara hiyo ya mafunzo, Msavia alisema, “Fursa niliyopewa na Serikali ya Marekani kuwa sehemu ya ziara hii ya mpango wa ‘Edward R. Murrow’ kwa waandishi wa habari, siyo tu kwamba itanielimisha kuhusu njia mbalimbali za utendaji wa vyombo vya habari vya Marekani, lakini pia itafungua macho yangu na kunipa uelewa wa mifumo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ya taifa la Marekani.”

Alisema, “Wakati huohuo, itanipa fursa ya kuchunguza na kuchambua haki na wajibu wa vyombo huru vya habari, hasa wakati huu Tanzania tunapojadili maudhui ya muswada mpya wa habari.” Aliongezea kwamba, ziara hiyo itakuwa “fursa muafaka ya kulinganisha tofauti za kitamaduni zilizopo kati ya nchi zetu mbili.”