Kiswahili Press Release
USAID yasaidia kuandaa warsha ya kupitia upya mpango wa usimamizi wa hifadhi za wanyama za Grumeti-Ikorongo
Aprili 24, 2006
Warsha ya kupitia upya mpango wa zamani (1998-2002) wa usimamizi wa hifadhi za wanyama za Grumeti-Ikorongo imepangwa kufanyika mjini Musoma April 25-27 chini ya ufadhili wa shirika la misaada la USAID. Warsha hiyo ni sehemu ya mradi mkubwa wa USAID kuhifadhi mazingira unaotekelezwa na mfuko wa African Wildlife Foundation, kwa kushirikiana na Idara ya Wanyama Pori katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hifadhi za wanyama za Grumeti na Ikorongo ni sehemu muhimu ya mfumo mkubwa wa ikolojia ya Serengeti. Hifadhi hizi ni ukanda wa magharibi unaotumiwa kila mwaka na mamilioni ya nyumbu wanapohama na kuvuka mbuga za Serengeti. Serengeti ilitangazwa kuwa eneo la urithi wa dunia baada ya kupata umaarufu wakati wa miaka ya 60 kupitia kitabu cha Dkt. Bernard Grizmek: “Serengeti Kamwe Haitakufa.” Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni moja ya hazina kubwa za Tanzania na pia ni kivutio kikubwa kwa watalii. Mwaka wa 2005 takriban watalii 155,000 kutoka nchi mbalimbali walitembelea hifadhi hiyo na kuliletea taifa kiasi cha dola milioni 7. Hifadhi yaTaifa ya Kilimanjaro ndiyo peke yake inayoizidi Serengeti kwa kiwango cha mapato.
Shirika la USAID linafadhili warsha hiyo kwa sababu linaamini kwamba, maisha ya wananchi wanaoizunguka hifadhi yataboreshwa ikiwa wadau mbalimbali watashirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kuandaa mipango ya kusimamia hifadhi hiyo. Wadau hawa ni pamoja na jumuia za taasisi za kiraia (civil society), sekta binafsi, pamoja na serikali. Malengo ya USAID yanahusiana: kuhifadhi mifumo ya ikolojia, na ikiwa uwekezaji pamoja na maendeleo yatapatikana – kuandaa mikakati ya kuhakikisha kwamba jamii inafaidika na miradi hiyo ya kibiashara. Lengo kuu ni kuwahamasisha wadau wote kuunga mkono juhudi madhubuti za kutunza baioanuwai (biodiversity).
Wawakilishi kutoka makampuni ya uwindaji, hoteli, pamoja na utalii, yanayofanya shughuli zake katika eneo la Serengeti Magharibi, ikiwemo hoteli ya kisasa ya Sasakwa iliyogharimu dola milioni 16, wamekaribishwa kushiriki katika warsha hii itakayojadili mipango ya maendeleo na mikakati ya kuhakikisha kwamba jamii inayozunguka hifadhi hiyo inafaidika na biashara zao. Jumla ya wajumbe 65 wanatarajiwa kushiriki, wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wabunge kutoka Wilaya za Mugumu na Serengeti, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya, Wenyeviti wa Halimashauri za Wilaya, Madiwani, Watendaji wa Kata, wawakilishi wa vijiji, pamoja na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa, TANAPA.
Wakati wa warsha hiyo, washiriki watajadili mada mbalimbali zikiwa ni pamoja na malengo ya mikakati ya utunzaji wa hifadhi, vipingamizi, shughuli za kijamii na kiuchumi. Masuala ya migongano kati ya binadamu na wanyama kuhusu malisho, kilimo, maji, na maeneo ya utamaduni pia yatajadiliwa. Mpango huo wa kusimamia hifadhi utabainisha maeneo ambayo rasilimali zake zitatumiwa na kuandaa mikakati ya kuyatunza maeneo hayo ili kuhakikisha kwamba kweli “Serengeti Kamwe Haitakufa,” na kwamba jamii zilizo jirani zinafaidika na biashara ya utalii. Baada ya shughuli za ukusanyaji wa takwimu na utayarishaji wa mpango huo kumalizika, warsha ya pili itafanyika ili kufanya tathmini na kukamilisha mpango huo.



