Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Rais Karume na Balozi wa Marekani Michael Retzer Wazindua Mradi wa Radio kwa Watoto
May 3, 2007
Watoto wa Kizanzibari wako tayari kujifunza lakini wanahitaji msaada zaidi kutoka kwa familia na skuli ili kufikia lengo hilo. Serikali imekuwa mtetezi mkubwa wa Elimu ya utotoni. Juhudi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), zinaonekana kwani ameidhinisha sera ya Elimu ya Maandalizi na kuweka lengo la kuwa asilimia 50 ya watoto wote wenye umri huu wawe wameandikishwa skuli za maandalizi ifikapo mwaka 2010. Ili kuwafikia watoto wengi kwa haraka zaidi, WEMA pamoja na Shirika la Misaada la Kimataifa la Kimarekani (USAID) linaanzisha Mpango wa Kuimarisha Elimu kwa Njia ya Redio - Radio Instruction to Strengthen Education (RISE) ambayo itatoa fursa ya kuanzishwa vilabu vya kujifunza kwa njia ya redio kwa watoto wa Skuli za Maandalizi pamoja na watoto wengine baada ya skuli. Vilabu hivi vya kujifunza vitakuwa katika jamii. Kwa kutambua umuhimu wa teknolojia ya Redio katika kupeleka mbele Elimu Zanzibar, Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Karume pamoja na Balozi wa Marekani, Michael L. Retzer watakuwa Wageni Rasmi katika sherehe ya uzinduzi wa RISE siku ya tarehe 3 Mei saa nne kamili asubuhi katika Ofisi za RISE zilizopo katika jengo la RISE/WEMA, mtaa wa Vuga uliopo Mji Mkongwe.
Kwa kupitia RISE pamoja na mshirika wake wa kutekeleza Mradi huu, Shirika la Maendeleo la Elimu (Education Development Center - EDC), USAID imejenga Studio ya redio yenye vifaa vya kisasa kabisa vya kurekodia vipindi. Pia inafundisha walimu kutayarisha vipindi 278 vya Elimu kwa Redio. Vipindi vya Tucheze Tujifunze vitakuwa na mambo ya kufurahisha zikiwemo hadithi, michezo ya kuigiza, michezo, na nyimbo ambazo zitasaidia katika kuimarisha mambo ya msingi yanayofundishwa katika miaka ya mwanzo ya skuli. Pia itawasaidia jamii kushiriki zaidi katika kutekeleza jukumu la mafunzo ya watoto wao.
RISE ni mpango shirikishi wa jamii unaozingatia kuwa malezi na mafunzo ya nyumbani huathiri na kukuza watoto wanapokuwa skuli. Mpango huu unajumuisha kufanya kazi na jamii ili kuanzisha vilabu 125 vya Tucheze Tujifunze vitakavyokuwa na watoto 10,200. Wengi wa watoto hao wataweza kufanya vizuri zaidi katika Hesabu, Kiswahili na Stadi za Maisha katika vilabu vya masomo vinavyoendeshwa na Msaidizi/Mzazi aliyepata mafunzo. Kwa kutumia redio zinazoendeshwa kwa kuzungusha tu, wazazi na vijana watakaojitolea kutoka kila jamii wataweza kuwa na mpango bora we elimu, na wakati huo huo wao wenyewe wakijifunza vipi watawasaidia watoto kijamii, kihisia, na kimafunzo, mambo ambayo watoto wanahitaji ili waweze kufanya vizuri wanapokwenda skuli.
Walimu 60 wa madarasa ya awali ya Skuli za Msingi pia watatumia njia ya kujifunza kwa redio na kuyapa nguvu mambo yaliyo katika mtaala wa Serikali na kuyafanya bora zaidi katika mazingira ya kujifunzia ya watoto.
Sauti ya Tanzania Zanzibar, mshiriki muhimu katika suala hili, itaanza kurusha hewani vipindi vya elimu kwa njia ya redio kuanzia mwezi Julai 2007. Vipindi vya Darasa la Kwanza vitaanza kurushwa hewani mwezi wa Januari 2008. Vipindi vya Darasa la Kwanza vitarushwa baada ya saa za skuli katika vilabu vya mafunzo ya elimu na vitafanyiwa majaribio katika madarasa 60 Wilaya za Micheweni na KaskaziniA ili kuleta furaha zaidi katika mchakato wa kujifunza.
RISE pamoja na EDC wanaamini kuwa penye mashirikiano ya dhati baina ya sehemu zote muhimu za maendeleo ikiwamo Serikali na jamii, malengo yote ya Mradi huu yanaweza kufikiwa.
Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana na:
Deborah Llewellyn, RISE Country Director 0754 782 111 au
Bishara Mohamed, RISE Technical Advisor 0777 411 060




