| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Warsha ya AGOA yatambulisha mpango mpya wa Marekani kuboresha ushindani
Mei 11, 2006
Balozi wa Marekani Michael Retzer pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nazir Karamagi, walifungua Mei 11, 2006 warsha ya siku mbili ya AGOA kwenye hoteli ya Kempinski Kilimanjaro kujadili jinsi ya kuboresha ushindani na uwezo wa Tanzania katika biashara.
Warsha hii ambayo imeandaliwa na shirika la misaada la USAID pamoja na kituo cha kuhamasisha biashara katika nchi za Afrika Mashariki na Kati – East and Central African Trade Hub - itaangalia juhudi za hivi karibuni zinazofanywa na Tanzania kupenya katika soko la Marekani, na pia jinsi ya kuimarisha shughuli za mpango wa AGOA. Wawakilishi kutoka USAID watautambulisha mpango mpya wa Rais wa Marekani wa kuboresha ushindani, ambao umetengewa dola miloni 200 katika miaka mitano ijayo. Mpango huu utajenga uwezo wa sekta ya biashara wa nchi za Kiafrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
Matatizo wanayokumbana nayo wafanyabiashara wa Tanzania wanaotaka kuuza bidhaa zao nje ni pamoja na kukosekana kwa mikopo, masharti magumu ya kukidhi viwango vilivyowekwa, mbinu za kupata wateja, na usafirishaji wa bidhaa. Matatizo haya yanaathiri uwezo wa Tanzania katika biashara.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuongeza kiwango cha mauzo yake katika masoko ya nchi jirani na kimataifa. Hata hivyo, Tanzania ina fursa kubwa sana ya kupanua biashara yake - fursa ambayo haijatumiwa kikamilifu.
Tanzania ilijiunga na mpango wa AGOA mwaka wa 2002. Mpango huu unatoa fursa kwa aina nyingi za bidhaa kutoka hapa nchini kuingia katika soko la Marekani – soko kubwa kuliko yote ulimwenguni – kwa kiasi chochote na bila ya kutozwa ushuru. Mafanikio ya Tanzania katika kuitumia fursa hii inayotolewa na mpango wa AGOA yamekuwa madogo. Ingawa pamekuwepo na mafanikio machache, mauzo ya Tanzania nchini Marekani yalifikia dola milioni 33.7 katika mwaka wa 2005.
Pamoja na kwamba Tanzania na Marekani hazina historia ya uhusiano wa kibiashara, mpango wa AGOA ni muhimu katika kuimarisha uhusiano wa biashara baina ya nchi hizi mbili. Mpango mpya wa kuboresha ushindani - African Growth and Competitiveness Initiative - unaendeleza malengo ya AGOA, na hivyo kudhihirisha juhudi madhubuti za Serikali ya Marekani kuboresha uwezo wa Tanzania katika biashara. Msingi wa mipango hii ni imani ya watunga sera nchini Marekani kwamba, biashara ndiyo chachu muhimu ya kuimarisha ukuaji endelevu wa uchumi.
Kwa kuwaleta pamoja maafisa wa Serikali ya Tanzania, wadau wa sekta binafsi, wafadhili, pamoja na watunga sera, warsha hii itatumia utaalamu na uzoefu wao kutafuta njia za kuimarisha uwezo wa Tanzania katika bishara. Warsha hii pia itahakikisha kwamba wadau wote wanafanya kazi kwa pamoja, wakitumia fursa zinazotolewa na mipango iliyopo ili Tanzania iweze kushindana kwa ufanisi katika uchumi wa dunia.



