| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Wawakilishi wanawake waungana kupiga vita unyanyapaa
Mei 24, 2006
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawake wamepania kuongeza juhudi zao kuipiga vita unyanyapaa na ubaguzi unaohusiana na UKIMWI, hasa miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI pamoja na watoto walioambukizwa au kuathirika na UKIMWI.
Kwenye mkutano wa hivi karibuni kujadili unyanyapaa unaohusiana na UKIMWI, Wawakilishi hao, ambao wote ni wanachama wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar (UWAWAZA), waliahidi kutumia ushawishi na sauti zao kujenga uelewa katika jamii zao juu ya athari za unyanyapaa kwa familia na jamii kwa ujumla.
“Inatubidi kuanzia majumbani kwetu na baadaye tuwahamasishe majirani,” alisema Mheshimiwa Najma Khalfan. Ni muhimu tuunganishe juhudi zetu; tuweke kando itikadi zetu za kisiasa kwa sababu UKIMWI hauchagui. Sisi wote tuko hatarini, kwa hiyo tunahitaji kupambana kwa pamoja.”
Mheshimiwa Khalfan alikuwa akiongea mwishoni mwa warsha ya siku tatu kuhusu kuelewa na kupiga vita unyanyapaa unaohusiana na UKIMWI. Warsha hiyo iliandaliwa na mpango wa dharura wa Rais Bush wa kupunguza makali ya UKIMWI (PEPFAR), kupitia taasisi ya PACT Tanzania inayofadhiliwa na shirika la misaada la USAID. Hii ni sehemu ya mpango wa miaka mitatu wa ‘Jali Watoto’ na kampeni ya kupiga vita unyanyapaa.
Mpango wa ‘Jali Watoto’ utashirikiana na taasisi mbalimbali; vikundi vya dini na jamii kuwasaidia watoto walioathirika zaidi; kutoa mafunzo kwa vijana, waandishi wa habari na watunga sera pamoja na kupiga vita unyanyapaa unaohusiana na UKIMWI katika jamii zao.
Wawakilishi wanawake walisema kwamba tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya miongoni mwa wanaume na wanawake Wazanzibari ni suala jingine linalohitaji kushughulikiwa kwa dhati. Walikubaliana kuwa utumiaji wa madawa ya kulevya hauwaathiri tu wananchi walio katika umri mzuri wa kuchangia mendeleo ya jamii, bali pia unaongeza kasi ya kueneza UKIMWI.
“Ni wajibu wetu kama wanawake na viongozi kuanzisha vita hivi dhidi ya utumiaji wa madawa ya kulevya,” alisema Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Biashara na Uwekezaji. “Ni lazima tuviambie vyombo vya dola kuwa tumechoka kuwapoteza watoto wetu. Ni lazima waipe kipaumbele vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya.”
Mheshimiwa Hassan alisisitiza kwamba changamoto hii ni wajibu wa kila mtu. Kwa hiyo, alisema, hawana budi kufanya juhudi za pamoja kuwahamasisha wanawake katika sekta zote za jamii kuungana na kuishinikiza serikali kulichukulia tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya kama tishio kubwa kwa maisha ya Watanzania wengi, na hivyo lipewe kipaumbele.
Kwenye warsha hiyo ya siku tatu, Wawakilishi walibadilishana mawazo na kuelezana matukio halisi waliyowahi kuyashuhudia wenyewe kuhusu unyanyapaa. Walibainisha kwamba unyanyapaa na ubaguzi vimekithiri Visiwani, kama ilivyo katika sehemu nyingi duniani, na kwamba wana wajibu mkubwa wa kupiga vita unyanyapaa.



