Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Press Release

Wajasiriamali Watanzania 15 kuhudhuria maonyesho ya kimataifa ya biashara ya ‘franchise’ nchini Marekani

May 26, 2006

Ujumbe wa wafanyabiashara Watanzania 15 unaenda Marekani kushiriki kwenye maonyesho ya 15 ya kila mwaka kuhusu biashara ya franchise (Annual International Franchise Expo - IFE 2006) yatakayofanyika mjini Washington D.C. Juni 2-4, 2006. Maonyesho hayo ni mashuhuri duniani na yanaonyesha mamia ya aina mbalimbali za mfumo wa biashara hii ya franchise.

Biashara ya franchise ni makubaliano ya kununua ruksa na haki ya kutumia mfumo na nembo ya biashara ya usambazaji wa bidhaa au huduma kati ya pande mbili, ambapo mnunuzi hulipa ada ya awali na mirahaba kwa muuzaji wakati biashara inaendelea. Mifano mizuri ya biashara ya franchise ni migahawa ya McDonalds, Steers, SUBWAY, pamoja na kampuni ya Coca Cola.

Maonyesho hayo ya IFE yatawasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kuelewa zaidi biashara za franchise nchini Marekani, na pengine kupata franchise, au kuanzisha uhusiano wa kibiashara na franchise za Marekani. Maonyesho ya IFE yatawapa pia fursa ya kuhudhuria semina za kuwaelimisha, ili waweze kuleta nyumbani mifumo ya biashara iliyokwisha thibitishwa na kufanyiwa majaribio.

Kaulimbiu ya maonyesho ya IFE ya mwaka huu ni “Franchise kama zana ya kuendeleza biashara ndogo na za kati,” na ujumbe wa Tanzania unawakilisha makampuni madogo na ya kati kutoka nchini kote. Watanzania 15 wanaokwenda Marekani ni Rosemary Kitilya, Mkurugenzi Mtendaji wa H & R Consultants; Dk. Judith Mhina, Mkurugenzi Mtendaji wa McJuro Holdings; Dk. Pius Ng’wandu, Mwenyekiti Mtendaji wa YASEKON International; Peter Ngongoseke, Mkurugenzi Mtendaji wa COSEKE; Evarist Maembe, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Meat Products; pamoja na Ruckya na Omar Basseporte, Mkurugenzi Mtendaji na Mkurugenzi wa Hoteli ya Le Jacaranda, Arusha.

Washiriki wengine ni Charles Singili, Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bancorp; Ally Madikah, Mkurugenzi Mtendaji wa Atma Electronics; Lukonge Mhandagani, Mkurugenzi Mtendaji wa Philip & Co; Amadeus Chacky, Mkurugenzi Mtendaji wa Ametech Tanzania; Constantine Mnzeru wa Atma Electronics; Dk. Jabu Mwasha, Mkurugenzi Mtendaji wa TANVET; Malik Alani, Mkurugenzi Mtendaji wa Topic 64 Computers; na Kulwa Mapigano, Meneja Uendeshaji wa Planetel Communications.

Maonyesho ya IFE 2006 yatawapa wajumbe wa Tanzania pia fursa ya kukutana na wafanyabiashara kutoka nchi zingine ulimwenguni kote. Maonyesho hayo yameidhinishwa na Wizara ya Biashara ya Marekani (US Department of Commerce) na yanatangazwa duniani kote kama sehemu ya mpango wa kuvutia wanunuzi wa kimataifa (International Buyers Programme). Kwa hiyo, Balozi za Marekani zinafanya juhudi kubwa kuyatangaza maonyesho ya IFE katika nchi zinakowakilisha na kuleta wajumbe kutoka duniani kote kushiriki kwenye maonyesho hayo. Mwaka huu, Balozi za Marekani katika nchi zingine 57 zinafadhili ujumbe wa kibiashara kwenye maonyesho ya IFE.

Maonyesho ya IFE hufanyika kila mwaka na yanaandaliwa na muungano wa kimataifa wa biashara za franchise (International Franchise Association), na huonyesha aina nyingi za biashara ya franchise kwa viwango mbalimbali vya uwekezaji. Kwa zaidi ya miaka kumi, maonyesho ya IFE yamekuwa ni sehemu ya kukutana wafanyabiashara wa franchise kutoka ndani na nje ya nchi kwa madhumuni ya kushiriki katika biashara hiyo.

- Translation -
This content is also available in English