| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Saba Saba 2006: Banda la Marekani kubwa zaidi, bora zaidi na thabiti zaidi
Juni 28, 2006
Teknolojia ya kisasa, uthabiti, ubora wa hali ya juu. Hizi ni sifa za makampuni ya Kimarekani yanayofanya biashara karibu katika nchi zote ulimwenguni, ikiwemo Tanzania. Banda la Marekani kwenye maonyesho ya 30 ya Sabasaba mwaka huu litaonyesha makampuni ya Kimarekani, taasisi pamoja na bidhaa zinazotumia teknolojia ya kisasa kabisa na zinazotoa huduma za kiwango cha juu nchini Tanzania na nje. Bidhaa hizo ni pamoja na kompyuta, mitambo ya usalama, matairi na hata dawa za meno.
Banda la Marekani mwaka huu lina ukubwa maradufu ya ule wa banda la 2005 (vitengo 21), na litakuwa na washiriki wapya kutoka sekta binafsi. Makampuni hayo mapya ni pamoja na SSTL, Colgate-Palmolive, Caltex, Elite Computers, Nufaika Distributors na Goodyear Tyre. Wadau wa shirika la misaada la USAID ni pamoja na TechnoServe, DAI Pesa na Kickstart. Ubalozi wa Marekani pia utaonyesha shughuli mbalimbali, zikiwemo huduma za biashara, fursa za masomo nchini Marekani, na mpango wa AGOA.
Balozi Michael Retzer amefurahishwa na kuongezeka kwa idadi ya makampuni kutoka sekta binafsi ya Marekani, pamoja na wadau wa sekta ya maendeleo kwenye maonyesho ya Saba Saba ya mwaka huu. “Kukua kwa banda letu kunadhihirisha kuimarika kwa uhusiano wa kibiashara na maendeleo kati ya Marekani na Tanzania. Tunafurahi kushiriki katika maonyesho haya, na tunafanya hivyo ili kuonyesha sehemu nyingi ambazo tunaweza kushirikiana kwa faida ya nchi zetu mbili.”
Hakika, kiwango kikubwa cha ushiriki wa Marekani kwenye maonyesho ya Saba Saba ya mwaka huu kinadhihirisha kukua kwa ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania katika miaka ya hivi karibuni. Katika mwaka wa 2005, Marekani ilitoa misaada yenye thamani zaidi ya dola 100 kusaidia maendeleo ya Tanzania kupitia miradi kadhaa, ukiwamo mpango wa dharura wa Rais Bush wa kukabiliana na janga la UKIMWI – PEPFAR. Mwaka wa 2006, kiwango cha misaada kwa Tanzania chini ya mpango wa PEPFAR, mpango wa kudhibiti malaria wa President’s anti-Malaria Initiative (PMI), pamoja na Millennium Challenge Account (MCA) kitaongezeka zaidi.



