Habari Kutoka Ubalozi
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Azuru Tanzania Kukazia Ushirikiano Imara wa Kiserikali uliopo baina ya Marekani na Tanzania na Kufanya Mapitio/Tathmini ya Programu za Misaada
Julai 1, 2009
Dar es Salaam: Afisa wa ngazi ya juu kabisa katika Utawala wa Rais Obama kuwahi kutembelea Tanzania, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anayeshughulikia Utawala na Rasilimali, Bw. Jacob Lew, yupo katika ziara ya siku tatu nchini, kuanzia tarehe 30 Juni hadi 2 Julai, 2009 ambapo atatembelea miji ya Dar es Salaam na Arusha. Baada ya kuwasili nchini, Bw. Lew alipata fursa ya kukutana na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Shein na Waziri wa Fedha Mkulo ambapo walijadili kuhusu ushirikiano imara uliopo baina ya nchi hizi mbili.
Bw. Lew aliwaambia waandishi wa habari kuwa, "Nipo hapa Tanzania kwa niaba ya Rais Obama na Waziri wa Mambo ya Nje Bibi Clinton kwa sababu Tanzania ni mshirika wetu mkuu katika kanda hii na ni mbia wetu muhimu wa maendeleo. Nipo hapa kusikiliza na kukazia dhamira yetu ya dhati ya kufanya kazi na watu na serikali ya Tanzania katika kuendesha programu zenye tija zaidi na zilizo endelevu zinazokidhi mahitaji ya msingi ya watu wa Tanzania."
Ziara ya Bw. Lew nchini, inalenga katika maeneo makuu mawili yanayopatiwa msaada na yanayopewa kipaumbele na Utawala wa Rais Obama pamoja na Tanzania ambayo ni – suala la afya na tatizo la njaa. Katika eneo la afya, Marekani imedhamiria kutumia mafanikio yaliyopatikana katika programu zetu za VVU/UKIMWI katika kujenga mfumo imara na endelevu wa utoaji wa huduma za afya na kuelekeza zaidi jitihada zake katika kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na kukabili maradhi yanayoweza kuzuilika kwa gharama nafuu.
Bw. Lew alibainisha kuwa kwa kupitia jitihada za Utawala wa Rais Obama za kutokomeza njaa duniani, Marekani ingependa kuona kuwa sekta ya kilimo inapanuka na kuwa na ukuaji endelevu ambao utaongeza tija katika uzalishaji mazao, kuongeza upatikanaji wa chakula kwa kuwaunganisha wakulima na masoko na kuongeza kipato ili watu wengi zaidi waweze kumudu gharama za chakula.
Mbali na kukutana na uongozi wa Tanzania Bw. Lew atashiriki pia katika majadiliano na bodi ya Akaunti ya Mfuko wa Millennium Challenge nchini Tanzania (MCA-T) ili kutathmini maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa. Aidha, atakutana na wafadhili wengine wa kimataifa, wanachama wa jumuiya ya wafanya biashara, wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na jumuiya za kiraia wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.
Akiwa jijini Arusha, Bw. Lew atakutana na Mkuu wa Mkoa huo na kutembelea hospitali na vituo vya afya vinavyotoa huduma za kukabiliana na VVU/UKIMWI na malaria. Vile vile atatembelea miradi ya maendeleo ya kilimo inayofadhiliwa na watu wa Marekani ili kuona ni kwa jinsi gani wazalishaji katika sekta ya mboga mboga, matunda na maua wa Tanzania wanaweza kupata na kupanua zaidi wigo wa masoko ya nje ya bidhaa zao.
Bw. Lew alisema, "Tanzania inafanya jitihada kubwa na ipo katika mwelekeo sahihi katika kupunguza umasikini, lakini inakabiliwa na changamoto ngumu kadhaa. Marekani imedhamiria kwa dhati kuendelea kufanya kazi kwa karibu na watu na serikali ya Tanzania ili kupata njia na mbinu mpya za kukabiliana na changamoto hizo na hivyo kupata matokeo yenye tija zaidi."
Kwa maelezo binafsi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, tafadhali tembelea tovuti: http://www.state.gov/r/pa/ei/biog/117944.htm
Kwa taarifa zaidi kuhusu program zinazoendeshwa nchini Tanzania kwa niaba ya watu wa Marekani, tafadhali tembelea tovuti yetu: http://tanzania.usembassy.gov




