Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Wizara ya Ulinzi ya Marekani yatoa dola 89,000 kusaidia ujenzi wa miradi miwili ya maji katika visiwa vya Unguja na Pemba

Julai 14, 2006

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetoa msaada wa dola 89,000 kusaidia ujenzi wa miradi miwili ya maji Zanzibar, mmoja kisiwani Unguja na mwingine kisiwani Pemba. Hafla ya kutia saini mikataba ya ujenzi wa miradi hii miwili ilifanyika Julai 14, 2006 huko Mji Mkongwe, Unguja.

Mkataba wa mradi kisiwani Unguja utakaotekelezwa Umbuji, Uzini, Wilaya ya Kati, ambao utagharimu dola 44,000 ulitiwa saini na Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Marekani, Luteni Kanali Laura Varhola, na mkandarasi wa mradi huo, Bw. Masoud K. Masoud wa kampuni ya Millennium Engineering and Construction Consultants Ltd.

Mkataba wa mradi wa Mkoa wa Pemba Kusini utakaotekelezwa katika kijiji cha Mjimbini, Mtambile, Wilaya ya Mkoani, na ambao utagharimu dola 45,000 ulitiwa saini na Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Marekani Luteni Kanali Laura Varhola, na mkandarasi wa mradi huo, Bw. Hemed N. Al Hilal wa kampuni ya Al Hilal General Trading Company, Ltd. Mheshimiwa Mansoor Yusuf Himid, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi Zanzibar, pamoja na Mkurugenzi wa Maji, Bw. Hemed Salim, walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini kwa vyombo vya habari, mradi wa maji kisiwani Unguja utawapa maji safi na salama wakazi 4,000 wa vijiji vya Umbuji na Pagali. Mradi wa maji kisiwani Pemba utawapa maji safi wakazi 3,545 wa vijiji vine vya Mjimbini, Tasini, Tondooni, Mtakakaa na Tanga.

Mikataba yote miwili inajumuisha nyenzo zote zinazohitajika kufanikisha ujenzi wa miradi hii. Serikali ya Zanzibar itagharimia malipo ya wafanyakazi na mafundi wote.

- Translation -
This content is also available in English