Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Shirika la USAID latoa msaada wa dola 400,000 wa vitabu na vifaa vya shule Zanzibar

Julai 18, 2006

Katika sherehe iliyofanyika Julai 14, 2006 kwenye shule ya msingi ya Mtopepo, Zanzibar, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bwana Michael Retzer alitoa msaada wa vitabu na vifaa vya kufundishia vyenye thamani ya dola 400,000 kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Msaada huu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Visiwani Zanzibar umetolewa kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu Zanzibar (MKEZA) unaofadhiliwa na shirika la misaada la USAID. Mradi huu umekuwa ukitekelezwa tangu Aprili 2004.

Lengo la mradi wa MKEZA ni kuboresha elimu Visiwani Zanzibar kupitia utoaji wa mafunzo kwa waalimu, kuhamasisha elimu shirikishi, kuboresha usimamizi wa shule, pamoja na utoaji wa vifaa vya kufundishia vinavyochangamsha. Kipaumbele cha mradi huu ni kuwahamasisha wanafunzi waweze kufanya vizuri katika masomo ya Sayansi, Elimu ya Uraia, Hisabati na Kiingereza. Marekani ndiye mfadhili mkubwa katika sekta ya elimu Visiwani Zanzibar. Mradi huo ni sehemu ya mpango wa Rais Bush kuboresha elimu barani Afrika – Africa Education Initiative. Mpango huu wa miaka mitano unaogharimu dola milioni 600 unalenga kuboresha sekta ya elimu katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

Misaada iliyotolewa ni pamoja na:

  • Vitabu zaidi ya135,000 vya masomo ya Hisabati na Kiingereza kwa shule za msingi;
  • Vifaa vya darasani kwa vyuo vitano vya elimu Unguja, Kituo cha Waalimu cha Nkrumah, pamoja na darasa moja la majaribio kwenye shule ya sekondari ya Fuoni;
  • Baiskeli 30 za watoto wasiojiweza Visiwani Pemba na Unguja, pamoja na vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa na wanafunzi vipofu;
  • Nakala 160 za vitabu vya madarasa ya 4-7 pamoja na vitabu vya waalimu vya masomo ya Hisabati na Kiingereza;
  • Kompyuta, mashine za photo copy na kuchapisha zitakazotumika kuboresha shughuli za wizara katika upangaji, utekelezaji, usimamizi, na utoaji taarifa wa mpango wa elimu kwa wenye mahitaji maalum (Special Needs Education Program)

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Hamis Jabir Makame, aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu Mwanaidi Abdallah; Mkuu wa Wilaya ya Mjini Magharibi Mussa Takrima; Mkurugenzi Mkazi wa shirika la misaada la USAID Bi. Pamela White; ujumbe kutoka taasisi isiyo ya Kiserikali ya Marekani inayotoa misaada ya vitabu – “Books for Africa” (ambayo ilisaidia upatikanaji wa vitabu vingine vya elimu 25,000 kutoka Marekani kwa manufaa ya wanafunzi wa Zanzibar), wajumbe wa kamati ya usimamizi wa shule, pamoja na wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi ya Mtopepo.
- Translation -
This content is also available in English