Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Shirika la USAID latoa msaada wa dawa na vifaa kusaidia kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa malaria katika wilaya za Muleba na Karagwe

July 25, 2006

Shirika la misaada la Marekani USAID, kupitia mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na malaria, (U.S. President’s Malaria Initiative) limetoa msaada wa zaidi ya dola 50,000 kununulia dawa na vifaa vya dharura kwa ajili ya kuwatibu watoto na akina mama wajawazito ambao wanaugua malaria baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kuzikumba wilaya za Muleba na Karagwe. Msaada huo ambao unatokana na ombi lililotolewa na mpango wa taifa wa kudhibiti malaria (National Malaria Control Program) kupitia Wizara ya Afya, utasaidia kuziba pengo la dawa zinazohitajika kutokana na upungufu uliojitokeza katika wilaya hizo mbili. Shehena ya dawa hizo iliondoka Dar-es-Salaam Alhamisi Julai 20 na ilitegemewa kuwasili Muleba Jumapili Julai 23. Baada ya kuwasili, dawa hizo zitakabidhiwa kwa waganga wakuu wa wilaya, halafu timu za afya za wilaya zitawafanyia uchunguzi wagonjwa na kutibu waathirika kwa kuzingatia mwongozo wa taifa wa kutibu malaria (National Malaria Treatment Guidelines).

Milipuko ya ugonjwa wa malaria hutokea mara kwa mara nchini Tanzania kwa sababu kinga ya wananchi dhidi ya ugonjwa huo ni ndogo. Wilaya 12 nchini huwa zinapatwa na milipuko ya ugonjwa wa malaria mara kwa mara, zikiwemo wilaya za Muleba na Karagwe. Zaidi ya watu 160 wamefariki dunia katika maeneo hayo kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Upatikanaji wa dawa hizi utasaidia kuokoa maisha ya binadamu na kuwaponya wengi walioathirika na malaria.

Taasisi ya maendeleo ya Mennonite (Mennonite Economic Development Associates - MEDA), kupitia mpango wa kudhibiti malaria wa PMI, kwa kushirikiana na shirika la misaada la USAID katika kutekeleza mpango wa hati punguzo, imetoa msaada mkubwa kufanikisha upatikanaji wa dawa kupitia Bohari Kuu ya Madawa. Taasisi ya MEDA pia inasaidia kuratibu usambazaji wa haraka wa dawa kwenda kwenye wilaya zilizoathirika.

Lengo la mpango wa Rais wa kupambana na malaria PMI ni kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo kwa asilimia 50 katika nchi kadhaa. Tanzania ni moja ya nchi tatu zilizochaguliwa mwanzoni kufaidika na mpango huu ambao miradi yake inatekelezwa Tanzania bara na visiwani Zanzibar.

- Translation -
This content is also available in English