Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa vyombo vya habari

Tanzania kushiriki kwenye tamasha la utamaduni Marekani 2009

Julai 27, 2007

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, aliongoza ujumbe wa ziara nchini Marekani mwezi uliopita, ziara ambayo ilifanikiwa sana. Katika kipindi cha miezi kadhaa, Mama Kikwete amehakikisha kwamba Tanzania itawakilishwa kwenye moja ya maonyesho muhimu ya utamaduni duniani – tamasha la utamaduni linaloandaliwa na taasisi ya Smithsonian (Smithsonian Folklife Festival). Tanzania itakuwa nchi ya kwanza ya Afrika ya Mashariki kushiriki kwenye tamasha hilo la mwaka 2009, na bila shaka hii itaongeza shauku ya Wamarekani kufahamu zaidi kuhusu utamaduni wa Tanzania, utalii, mazao ya kilimo kutoka Tanzanian yanayouzwa nchi za nje, historia, pamoja na kazi za mikono.

Kwa kawaida, nchi nyingine hungoja miaka mingi kabla ya kupata fursa ya kushiriki kwenye tamasha hilo, na ushindani ni mkubwa. Moja ya sababu za umaarufu wa tamasha hilo ni nafasi ya kipekee ya kuitangaza nchi, inayotolewa na maonyesho hayo, ikiwa ni pamoja na fursa ya kukutana na watu mashuhuri kutoka sekta za umma na binafsi. Idadi ya watu wanaohudhuria tamasha hilo ni takriban milioni 1.5, na mwaka 2009 itakuwa ni zamu ya nyota ya Tanzania kung’ara.

Akifuatana na Mkrugenzi wa shirika la misaada la Marekani la USAID, Bi. Pamela White, Mama Salma Kikwete alikutana na wawakilishi wa Tamasha la Utamaduni la Smithsonian mwezi Septemba 2006 na pia mwezi Juni 2007, ili kujifunza kuhusu tamasha hilo, kuonyesha baadhi ya kazi za sanaa za kipekee kutoka Tanzania, pamoja na kazi za mikono, na pia kujadili mikakati ya kuandaa programu ya kufana.

Akiongelea kuhusu ziara yao hiyo ya hivi karibuni, Mkurugenzi wa USAID Bi. Pamela White alisema kwa msisimko, “Mama Salma Kikwete alikuwa nyota kila mahali tulipokwenda… alikuwa amependeza, na aliweza kujieleza kwa ufasaha. Huwezi kuamini idadi ya watu waliokuwa wakimsimamisha kwenye Washington Mall na kutaka wapigwe naye picha ya pamoja. Ilikuwa inasisimua kuona idadi kubwa ya watu waliotaka kupata taarifa zaidi kuhusu Tanzania na Afrika.”

Mama Salma Kikwete alitoa zawadi za picha za kuchora za Tinga Tinga, vinyago vya Wamakonde, shanga za Wamasai na nguo zao za jadi, pamoja na picha iliyochorwa ya Mji Mkongwe, Zanzibar. Waandaaji wa tamasha hilo walifurahishwa na ujuzi aliouonyesha Mama Salma Kikwete, ukarimu na ucheshi wake, na watatuma ujumbe kuja Tanzania baadaye mwaka huu, ili kusukuma mipango mbele na kuchagua washiriki kutoka Tanzania.

Tamasha la Utamaduni la Smithsonian lilianzishwa 1967 na hufanyika kila mwaka kwa kipindi cha siku kumi mwezi Juni na Julai, mjini Washington, D.C. Tamasha hilo limegawanywa katika ratiba mbalimbali zinazohusisha wasanii na sanaa (ikiwa ni pamoja na muziki, chakula, na ngoma) kutoka nchi, majimbo, maeneo au taaluma mbalimbali. Kiingilio ni bure na tamasha hilo liko wazi kwa umma.